Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unamna-Namna wa Viumbe Katika Msitu wa Amazoni

Unamna-Namna wa Viumbe Katika Msitu wa Amazoni

Unamna-Namna wa Viumbe Katika Msitu wa Amazoni

KUANZIA chini ya Milima Andes ya Peru, kuna utando wa matawi na majani ulioenea kuelekea mashariki ya Amerika Kusini na wenye ukubwa wa kilomita 3,700 hivi. Utando huo wa kijani kibichi umeenea hadi kwenye fuo za Bahari ya Atlantiki.

Asilimia 60 hivi ya nchi ya Peru imefunikwa na msitu huo wa Amazoni. Ingawa ni watu wachache wanaoishi katika eneo hili, kuna mimea na wanyama wengi chini ya hiyo miti mikubwa yenye urefu wa mita 35. Inasemekana kwamba msitu huo wa Amazoni una viumbe vingi vya aina mbalimbali. Kuna zaidi ya aina 3,000 za vipepeo. Pia kuna aina 4,000 hivi za okidi zinazotoa maua yenye kupendeza. Zaidi ya aina 90 za nyoka hutambaa juu ya matawi yaliyoanguka. Ndani ya mito na vijito kuna aina 2,500 hivi ya samaki kutia ndani mkunga na piranha.

Mbali na chemchemi zote hizo za maji kuna ule Mto Amazoni. Katika sehemu fulani, kila mwaka mvua hunyesha na kufikia kipimo kati ya mita 2.5 hadi 3. Maji hayo mengi sana hufanya Mto Amazoni pamoja na vijito vyake 1,100 kufurika kote-kote msituni. Hali-joto iliyochanganyika na unyevunyevu ulio hewani hutokeza mvuke ambao hufanya mimea isitawi. Jambo la kushangaza ni kwamba mimea hiyo hunawiri sana kwenye udongo wenye kunata, ambao hauna rutuba.

Historia ya Jamii Zilizoishi Katika Msitu Huo

Huenda ukajiuliza hivi, ni nani angependa kuishi mahali kama hapo? Wachimbuaji wa vitu vya kale wanaamini kwamba kwa karne zilizopita, mamilioni ya watu waliishi kwenye bonde la Mto Amazoni. Kufikia sasa, idadi ya watu 300,000 hivi—waliogawanywa katika zaidi ya makabila 40—wanaishi kwenye eneo la Amazoni ya Peru. Pia inasemekana kwamba vikundi 14 kati ya makabila hayo ya wenyeji wa asili ya Peru vimejitenga kabisa na watu wengine. Kwa mfano, baada ya kushirikiana kwa muda mfupi na watu kutoka maeneo yenye ustaarabu zaidi, watu wa makabila hayo waliondoka kabisa na kujificha katikati ya msitu huo na hawakutaka tena kushirikiana na yeyote.

Wakaaji hao wa msitu walitoka wapi, nao walianza kuishi huko lini? Wataalamu wanakisia kuwa karne kadhaa kabla ya Wakati wa Kawaida, wahamiaji wa kwanza kufika huko walitoka upande wa kaskazini. Watu wa kabila la Jivaro (wanaojulikana kwa kuhifadhi vichwa vya maadui wao) walitoka kwenye Visiwa vya Karibea; nao wale wa kabila la Arawak, walitoka Venezuela. Makabila mengine yanasemekana kuwa yalitoka Brazili iliyo mashariki ya Peru na Paraguai iliyo kusini.

Baada ya vikundi hivyo kuchagua maeneo waliyotaka kuishi, huenda baadhi yao walizunguka-zunguka sehemu fulani, wakiwinda na kukusanya matunda. Pia walipanda mimea kadhaa iliyoweza kukua kwenye udongo wenye asidi, kama vile mihogo, pilipili, ndizi, na mahindi. Waandishi Wahispania waliandika kuwa baadhi ya watu hao walikuwa na mpangilio mzuri, kwani walijenga maghala ya kuhifadhi chakula, na pia mbinu mbalimbali za kufuga wanyama wa mwituni.

Tamaduni Zahitilafiana

Katika karne za 16 na 17, Wahispania walivamia msitu wa Amazoni. Muda mfupi baadaye, wamishonari Wajesuti na wale wa Mtakatifu Francis walifika wakiwa na nia ya kuwabadili wenyeji wawe Wakatoliki. Wamishonari hao walichora ramani kwa ustadi zilizofanya wakazi wa Ulaya waufahamu vizuri msitu huo wa Amazoni. Lakini pia wamishonari hao walileta magonjwa na uharibifu katika msitu huo.

Kwa mfano, mwaka wa 1638 walianzisha kituo cha Kikatoliki katika eneo linalojulikana sasa kama Mkoa wa Maynas. Wamishonari waliwakusanya wenyeji na kuwalazimisha kuishi pamoja kama jamii, hata makabila yaliyokuwa na uhasama. Kwa kusudi gani? Kwa kuwa wenyeji walionwa kuwa wasio na akili na watu wa hali ya chini, walilazimishwa kuwafanyia kazi wamishonari na Wahispania waliokuwa wakoloni. Kwa sababu ya kuishi kwa ukaribu na watu hao kutoka Ulaya, maelfu ya wenyeji walikufa kutokana na surua, ndui, dondakoo, na ukoma. Maelfu ya wengine walikufa kwa sababu ya njaa.

Wenyeji wengi wa Asili wa Amerika walitoroka kambi zilizokuwa zimeanzishwa na vikundi mbalimbali vya kidini na wamishonari wengi waliuawa wakati wa ghasia. Wakati mmoja katika miaka ya mapema ya karne ya 19, ni kasisi mmoja tu aliyebaki katika eneo la Amazoni.

Jinsi Wanavyoishi Leo

Leo, wenyeji wengi wanaendelea kuishi kitamaduni. Kwa mfano, wao hujenga nyumba zao kama ambavyo wamefanya tangu zamani—zikiwa na nguzo za miti iliyokatwa kutoka msituni na kufunikwa kwa majani ya mitende na majani mengine yasiyoweza kupenya maji. Kwa kuwa nyumba zao zimeinuliwa juu ya ardhi kwa kutumia miti, hawatatizwi na mafuriko ya kila mwaka wala wanyama hatari hawawavamii.

Watu wa makabila mbalimbali huvalia na kujipamba kwa njia tofauti-tofauti. Wanaume na wanawake wanaoishi ndani sana ya msitu huvalia nguo zinazofunika kiuno pekee au vitambaa vifupi vilivyofumwa, na watoto wao hutembea uchi. Wale wanaoishi karibu na miji wanavalia kama watu wanaotoka Ulaya. Wenyeji fulani hutoboa pua au masikio yao na kujipamba kwa vipuli, vijiti, mifupa, au manyoya. Wengine, kama vile kabila la Mayoruna hutoboa mashavu yao. Watu fulani wa makabila ya Tucuna na Jivaro huchonga meno yao. Wengi kati ya makabila hayo hunyoa nywele zote na kutia miili yao alama ya chanjo.

Watu wa Amazoni wanajua maelfu ya mimea nao hutoa dawa msituni. Wao hutoa dawa kama zile za kumtibu mtu anapoumwa na nyoka, anayehara damu, aliye na matatizo ya ngozi, na kadhalika. Muda mrefu kabla ya watu wengine kugundua mpira, watu wa Amazoni walitoa mpira kutoka kwenye miti ya mpira, na kuipaka kwenye vikapu vyao visipenye maji na pia kutengeneza mipira ya kuchezea. Pia msitu huwapa vifaa wanavyohitaji kwa ajili ya usafiri na mawasiliano ya mbali. Kwa mfano, wanaume hukata miti na kuchonga mitumbwi ambayo wao hutumia katika mito, nao huchonga mashimo ndani ya magogo makubwa na kutengeneza ngoma ambazo wao hutumia kutuma ujumbe unaoweza kusikika mbali sana!

Kutawaliwa na Waganga na Ushirikina

Wakazi wa msitu wa Amazoni huamini kwamba msitu huo umejaa nafsi zinazozurura usiku, roho zinazosababisha magonjwa, na miungu inayojificha ndani ya mito ikisubiri kuwanasa watu. Fikiria kuhusu Aguaruna, moja kati ya makabila makubwa zaidi nchini Peru. Wanaabudu miungu mitano tofauti: “Baba Shujaa wa Vita,” “Baba wa Maji,” “Mama wa Dunia,” “Baba wa Jua,” na “Baba wa uganga.” Wengi wanaamini kwamba wanadamu wanabadilishwa kuwa mimea na wanyama. Kwa kuwa wanaogopa kuwakasirisha viumbe wa roho, wenyeji huepuka kuwaua wanyama fulani nao huwawinda wengine inapohitajika tu.

Waganga ndio husimamia maisha ya kidini na ya kijamii. Wao hutumia mimea kujipumbaza akili. Watu fulani katika maeneo hayo huwatazamia waganga hao watibu magonjwa, watabiri jinsi uwindaji na mavuno yatakavyokuwa, na kutabiri matukio ya wakati ujao.

Je, Msitu Huo Utatoweka?

Msitu wa Amazoni unaangamia kwa kasi sana. Barabara kubwa zinapasuliwa katika misitu. Mashamba ya chakula na ya kokeini yanachukua mahali pa msitu. Kila siku miti inakatwa katika sehemu ya msitu inayotoshana na viwanja 1,200 vya mpira! Uchimbaji wa migodi na kutokezwa kwa kokeini kunachafua vijito vinavyoingia katika Mto Amazoni.

Kwa kweli, watu wanaoishi katika msitu wa Amazoni wanapatwa na madhara ya kuishi katika siku ambazo Biblia ilitabiri zingekuwa “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” (2 Timotheo 3:1-5) Je, msitu wa Amazoni utaharibiwa kabisa? Biblia inatuhakikishia kwamba haitakuwa hivyo. Chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, dunia nzima itageuzwa kuwa paradiso, kama Muumba wetu alivyokusudia iwe.—Isaya 35:1, 2; 2 Petro 3:13.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mto Amazoni

[Picha katika ukurasa wa 17]

Watu wa kabila la Aguaruna wanaabudu miungu mitano tofauti

[Picha katika ukurasa wa 17]

Wanawake wa kabila la Lamas

[Picha katika ukurasa wa 18, 19]

Mwanamume wa kabila la Loreto akiwinda

[Hisani]

© Renzo Uccelli/PromPerú

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nyumba ya kitamaduni

[Picha katika ukurasa wa 19]

Miti inakatwa kila siku katika sehemu inayotoshana na viwanja 1,200 vya mpira

[Hisani]

© José Enrique Molina/age fotostock

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

© Alfredo Maiquez/age fotostock

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Top: © Terra Incógnita/PromPerú; bottom: © Walter Silvera/PromPerú