Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Moyo Unavyopiga

Jinsi Moyo Unavyopiga

Jinsi Moyo Unavyopiga

● Moyo ndio kitovu cha mfumo wako wa kuzungusha damu, nao hufanya kazi kwa bidii sana. Ikiwa wewe ni mtu mzima, huenda moyo wako hupiga zaidi ya mara 100,000 kwa siku. Hata unapopumzika, misuli ya moyo wako hufanya kazi kwa bidii sana—mara mbili zaidi ya kawaida, kama vile tu misuli ya miguu yako inavyofanya unapokimbia kwa kasi sana. Pia inapohitajika, katika muda wa sekunde tano tu, moyo wako unaweza kuongeza mipigo yake mara mbili zaidi ya kawaida. Moyo wa mtu mzima hupiga kati ya lita 5 [painti 10] za damu kwa dakika hadi lita 20 kwa dakika anapofanya mazoezi. Inakadiriwa kwamba mwili wa mwanadamu una lita 5 za damu.

Mpigo wa moyo wako huongozwa na mfumo wa neva uliobuniwa kwa njia ya ajabu sana. Mfumo huu huhakikisha kwamba vile vyumba viwili vya juu vya moyo (atria) hufunga sekunde moja hivi kabla ya vile vya chini (ventricles). Mlio wa moyo ambao madaktari husikia wanapotumia stetoskopu, hutokana na valvu za moyo zinazofunga na si misuli ya moyo inayodunda.

Mipigo Bilioni Moja

Kwa ujumla, mwendo ambao moyo wa mnyama hupiga, hutofautiana kulingana na ukubwa wake—hilo linamaanisha ikiwa mnyama ana mwili mkubwa, moyo wake hupiga polepole sana. Kwa mfano, moyo wa ndovu hupiga kwa wastani mara 25 kwa dakika moja ilhali moyo wa ndege anayeitwa canary, hupiga mara 1,000 kwa dakika! Mwanadamu anapozaliwa moyo wake hupiga mara 130 kwa dakika na baadaye unapunguza kasi kufikia mara 70 hivi anapokuwa mtu mzima.

Inaonekana kwamba wanyama wengi wanaonyonyesha hufa baada ya mioyo yao kupiga wastani wa mara bilioni moja. Hivyo, kwa kuwa moyo wa panya hupiga mara 550 kwa dakika, anatarajiwa kuishi miaka 3 hivi; ilhali nyangumi-samawati anatarajiwa kuishi zaidi ya miaka 50 kwani moyo wake hupiga mara 20 hivi kwa dakika. Lakini wanadamu ni tofauti. Ikiwa urefu wa maisha yetu utakadiriwa kulingana na mipigo ya moyo basi tunapaswa kuishi miaka 20 hivi. Hata hivyo, moyo wa mwanadamu mwenye afya nzuri unaweza kupiga mara bilioni tatu au hata zaidi na hivyo kumfanya aishi miaka 70 au 80! *

Hata hivyo, hakuna yeyote ambaye angependa kukadiria miaka atakayoishi kwa kulinganisha mara ambazo moyo wake hupiga, kwani wanadamu wana tamaa yenye nguvu sana ya kuishi milele. Kwa kweli, tamaa hiyo ni ya asili kwa sababu Mungu ndiye aliyetupa. Zaidi ya hilo, wakati unakaribia ambapo dhambi—chanzo cha kifo—itaondolewa kabisa. (Waroma 5:12) Hilo linamaanisha kwamba “kifo hakitakuwapo tena,” kama Ufunuo 21:3, 4 inavyosema.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Tarakimu zilizo juu ni makadirio tu. Mwendo ambao moyo hupiga na pia miaka ambayo kila kiumbe anaishi inaweza kuwa tofauti na makadirio hayo.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 29]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MUUNDO WA MOYO

Chumba cha juu kulia

Chumba cha juu kushoto

Chumba cha chini kulia

Chumba cha chini kushoto