Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutana na Makabila ya Milimani ya Thailand

Kutana na Makabila ya Milimani ya Thailand

Kutana na Makabila ya Milimani ya Thailand

Masoko ya jiji la Chiang Mai yamejaa shamrashamra. Umati wa watu unatembea upesi kwenye barabara yenye vibanda vinavyouza bidhaa za kienyeji. Wanunuzi wanajadiliana bei na wauzaji huku kukiwa kelele nyingi za magari. Katika hekaheka hizo kaskazini mwa Thailand, wageni wanaweza kukutana na makabila ya milimani ya Thailand.

WATU milioni 65 wanaoishi Thailand wanatia ndani watu kutoka makabila madogo 23 ambayo husemwa kuwa ni makabila ya milimani. Mengi ya makabila hayo huishi kaskazini mwa Thailand, eneo lenye milima, mito, na mabonde yenye rutuba, eneo linaloingia Myanmar na Laos.

Mengi kati ya makabila hayo ya milimani yalihamia katika eneo hilo miaka 200 iliyopita. Kabila la Karen, ambalo ndilo kabila lenye watu wengi kati ya yale makabila sita makuu, lilitoka Myanmar. Makabila ya Lahu, Lisu, na Akha yalitoka mkoa wa Yunnan, ulio kwenye nyanda za juu kusini-magharibi mwa China. Na makabila ya Hmong na Mien yalitoka katikati mwa China. *

Makabila hayo yalihama hasa kwa sababu ya vita, mikazo ya kijamii, na ukosefu wa mashamba yenye rutuba. * Eneo la Thailand Kaskazini lilikuwa mahali panapofaa kwao kwa sababu halifikiki kwa urahisi, lina milima, na halina watu wengi. Na serikali ya Thailand iliwaruhusu wahamiaji hao kuishi huko. Punde si punde kukawa na vijiji vingi vya makabila hayo ya milimani, kabila moja likipakana na mengine na kutokeza mchanganyiko wenye kuvutia wa utamaduni na lugha.

Mavazi ya Pekee na Desturi Zenye Kuvutia

Unaweza kutambua kila kabila la milimani kwa mavazi yake ya pekee. Kwa mfano, wanawake wa kabila la Akha huvalia kofia za fedha, zinazofanana na minara iliyopambwa kwa shada, mishono yenye kupendeza, na sarafu. Baadhi ya kofia hizo zinafanana na kofia ngumu zilizotengenezwa kwa chuma na kupambwa kwa vifungo, shanga, na vitu vya mviringo vinavyong’aa. Wanawake wa Mien wanavutia sana wakiwa wamevalia suruali ndefu zilizorembeshwa kwa nyuzi, ambazo huenda zikachukua miaka mitano hivi kutengenezwa. Zaidi ya mavazi hayo, wao huvaa vilemba, mavazi marefu yenye kola nyekundu iliyochanika-chanika, na mishipi ya rangi ya bluu iliyoiva.

Zaidi ya mavazi yao maridadi, wanawake wa makabila hayo ya milimani huvalia mapambo ya fedha ambayo hutoa milio na kumetameta. Hilo huwafanya watu wanaowatazama au wanaotaka kuanzisha uchumba nao watambue utajiri wao. Wanaweza pia kuvalia mapambo ya glasi, mbao, au nyuzi.

Watu wengi wa milimani hujivunia tamaduni zao. Kwa mfano, vijana wa kabila la Karen huvalia mavazi yenye kupendeza zaidi wakati wa mazishi kuliko wanavyofanya wakati wa tukio lingine lolote. Kwa nini? Vijana wengi huhudhuria mazishi wakitazamia kukutana na wachumba wao. Baada ya jua kushuka, vijana—wa kiume na wa kike—hushikana mikono, wakiuzunguka polepole mwili wa aliyekufa, na kuimba nyimbo za kienyeji za mapenzi usiku wote.

Vijana wa kabila la Hmong huchumbiana huku wakicheza mchezo fulani wa pekee wakati wa sherehe ya Mwaka Mpya. Wavulana husimama kwenye mstari mmoja wakimtazama yule msichana waliyevutiwa naye kimapenzi akiwa kwenye mstari mwingine. Kisha mvulana na msichana hurushiana mpira ulitengenezwa kwa nguo. Mmoja wao anapoangusha mpira huo—iwe ni kimakosa au kwa kupenda—analazimika kumpa mpenzi wake pambo moja. Baadaye jioni hiyo, mtu anaweza kujipatia tena mapambo hayo kwa kumwimbia wimbo. Akiimba vizuri, watu wengi wanaweza kukaribia kumsikiliza na hilo linaweza kumfanya mpenzi wake avutiwe naye zaidi.

Jinsi Wanavyokabiliana na Kubadilika kwa Hali

Zamani makabila mengi ya milimani yalikata miti na kuteketeza vichaka ili kulima na kulisha mifugo. Zoea hilo liliharibu sana mazingira. Lakini sasa wanatumia mbinu nzuri zaidi na hilo linawaletea manufaa.

Makabila mengi ya milimani yanayoishi katika maeneo ya Thailand, Laos, na Myanmar yalikuza kasumba. Hata hivyo, familia ya kifalme ya Thailand na mashirika ya kimataifa ya kutoa msaada yamedhamini mipango ya kukuza kahawa, mboga, matunda, na maua. Pia, wakazi wengi wa milimani huuza bidhaa, vinyago, na kutoa huduma mbalimbali kwa biashara ya utalii inayozidi kukua.

Hata hivyo, umaskini, ukosefu wa usafi, na kutojua kusoma na kuandika kunafanya maisha yawe magumu kwa watu wengi. Matatizo mengine yanasababishwa na kupungua kwa mali za asili, kubadilika kwa tamaduni, ubaguzi, na matumizi mabaya ya kileo na dawa za kulevya. Mababu wa makabila hayo ya milimani walihamia Thailand ili kuepuka matatizo kama hayo. Lakini wanaweza kukimbilia wapi leo?

Mahali pa Kukimbilia Panapotegemeka

Wakazi wengi wa milimani wamepata mahali panapofaa zaidi pa kukimbilia, yaani, kwa Mungu wa kweli, Yehova. Kwenye Zaburi 34:8 Biblia inasema hivi: “Onjeni mwone ya kuwa Yehova ni mwema; mwenye furaha ni mwanamume ambaye humkimbilia.” Jawlay, wa kabila la Lahu, anasema hivi: “Kufikia wakati nilipooa nikiwa na umri wa miaka 19, nilikuwa mlevi na mraibu wa dawa za kulevya. Singeweza kufanya kazi bila kutumia dawa za kulevya, na bila kufanya kazi sikuwa na pesa. Mke wangu, Anothai, alijihisi akiwa mpweke na hapendwi. Tulibishana kila wakati.

“Binti yetu, Suphawadee, alipozaliwa, Anothai alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Lakini mimi ningekimbilia msituni kila mara Mashahidi walipokuja nyumbani. Hata hivyo, mwenendo wa mke wangu ulianza kubadilika na kuwa mzuri. Alizungumza nami kwa heshima na alishughulikia majukumu yake nyumbani kwa njia nzuri zaidi. Kwa hiyo, aliponitia moyo nijifunze Biblia, nilikubali.

“Mafundisho ya Biblia yaliponigusa moyo, nilifanya maendeleo hatua kwa hatua. Mwishowe, kwa msaada wa Mungu, nilishinda uraibu wangu. Sasa familia yangu ina furaha ya kweli kwa kuwa tumepata njia bora zaidi ya maisha! Pia tunafurahi kuwaeleza kweli za Biblia watu wengine wa makabila ya milimani.”

Maneno ya Jawlay yanatukumbusha unabii katika kitabu cha Ufunuo, unaosema kwamba katika siku za mwisho za mfumo huu mwovu wa sasa, “habari njema ya milele” itatangazwa kwa “kila taifa na kabila na lugha na watu.” (Ufunuo 14:6) Mashahidi wa Yehova wanaliona kuwa pendeleo kushiriki katika kazi hiyo, kazi ambayo inathibitisha kuwa Mungu anawapenda watu wote, kutia ndani makabila maridadi ya milimani ya Thailand.—Yohana 3:16.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Huenda makabila yakawa na majina mbalimbali. Kwa mfano, katika nchi nyingine, kabila la Mien huitwa Lu Mien, Mian, Yao, Dao, Zao, au Man.

^ fu. 5 Idadi kubwa ya makabila hayo ya milimani bado huishi China, na pia Vietnam, Laos, na Myanmar. Katika miaka ya hivi karibuni, idadi kubwa ya makabila ya milimani imehamia Australia, Marekani, Ufaransa, na nchi nyingine.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

JE, BANGILI HUREFUSHA SHINGO?

Wanawake wengi wa Kayan hujaribu kurefusha shingo zao kwa kuvalia bangili nyingi za shaba nyeupe zinazoenea shingoni pote kufikia urefu wa sentimita 38. * Wao huanza kufanya hivyo wakiwa wasichana wenye umri wa miaka mitano. Baada ya miaka kadhaa bangili hizo hubadilishwa na nyingine kubwa na nzito zaidi, hivi kwamba wakiwa watu wazima, wanawake hao huvalia bangili 25 hivi zenye uzito wa kilogramu 13! Tofauti na inavyodhaniwa bangili hizo hazirefushi shingo zao. Badala yake, zinafinya mtulinga na kushindilia mbavu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 25 Watu wa kabila la Kayan walihamia Thailand kutoka Myanmar, ambako watu 50,000 kati yao bado wako. Wanaitwa Padaung, jina linalomaanisha “Shingo Ndefu.”

[Hisani]

Hilltribe Museum, Chiang Mai

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

HEKAYA KUHUSU FURIKO KUBWA

Makabila ya Lisu na Hmong yana hekaya kuhusu furiko kubwa. Katika hekaya moja ya kabila la Hmong, “Bwana wa Anga” anawaonya ndugu wawili kuwa furiko kubwa litaifunika dunia. Anamwagiza ndugu mkubwa mjeuri ajenge mashua ya chuma, na yule ndugu mdogo mpole ajenge mashua ya mbao. Kisha anamwambia yule mdogo amwingize dada yake ndani ya mashua hiyo ya mbao, na pia mnyama wa kiume na wa kike wa kila jamii na mbegu mbili za kila mmea.

Furiko linapoanza, mashua ya chuma inazama, lakini ile ya mbao inaelea. Kisha joka kubwa lililo na umbo la upinde wa mvua linaikausha dunia. Mwishowe, yule ndugu mdogo anamwoa dada yake na wazao wao wanaijaza tena dunia. Ona kwamba kuna mambo yanayofanana kati ya hekaya hiyo na simulizi lililoripotiwa kwa usahihi kwenye Biblia Takatifu katika sura ya 6 hadi ya 10 ya kitabu cha Mwanzo.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Wanawake wa makabila ya milimani wakiwa wamejipamba

[Hisani]

Hilltribe Museum, Chiang Mai

[Picha katika ukurasa wa 17]

Jawlay akiwa na familia yake

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Both pictures: Hilltribe Museum, Chiang Mai