Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Barua ya Papa Benedikto wa 16 inasema hivi: “Kuna uhitaji mkubwa sana . . . wa kubadili Shirika la Umoja wa Mataifa na vilevile taasisi za uchumi na fedha za kimataifa, ili lile wazo la kuwa na muungano wa mataifa, liweze kutimia kikweli.”—L’OSSERVATORE ROMANO; italiki ni zao.

“Mtu mmoja kati ya watu watatu nchini Ukrainia huvuta pakiti moja hivi ya sigara kila siku.”—EXPRESS, UKRAINIA.

Asilimia 44 ya wavulana Wamarekani waliofanyiwa uchunguzi walisema kwamba “wamewahi kuona picha ya mwanafunzi mwenzao wa kike akiwa uchi, kupitia Intaneti au kupitia simu ya mkononi.”—TIME, MAREKANI.

“Hatua Yenye Kusikitisha”

Vita, ukame, msukosuko wa kisiasa, kupanda kwa bei ya chakula, na umaskini vimefanya wanadamu wafikie “hatua yenye kusikitisha,” linasema Shirika la Habari la Associated Press. Idadi ya watu wenye njaa ulimwenguni imezidi watu bilioni moja. Josette Sheeran mfanyakazi katika Shirika la Chakula Ulimwenguni la Umoja wa Mataifa alisema, “ulimwengu wenye njaa ni ulimwengu hatari. . . . Watu wanapokosa chakula, wao hufanya mambo matatu tu: Wanazua ghasia, wanahamia eneo lingine au wanakufa. Hakuna jambo lolote kati ya hayo linalofaa.” Zaidi ya hayo, idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa inaongezeka zaidi kuliko idadi ya watu ulimwenguni. Hata katika nchi zilizoendelea, idadi ya watu wasio na chakula cha kutosha imeongezeka kwa asilimia 15.4.

Faida za Kusoma Kabla ya Kulala

Mbali na kuwasaidia kupata usingizi haraka, watoto hufaidika wazazi wao wanapowasomea kabla tu ya kulala. Wachunguzi wanasema kwamba kufanya hivyo kunawasaidia watoto wakuze uwezo wao wa lugha, kunawafundisha kushika na kufungua kurasa, na pia kunaboresha kumbukumbu lao. “Lakini jambo la maana zaidi ni kwamba . . . mzazi anapomsomea mtoto kwa sauti, wao hufikiri na kuhisi kwa njia ileile,” linasema gazeti The Guardian. “Hilo hufanya kusoma kuwe jambo la kufurahisha.” Pia, Profesa Barry Zuckerman, aliyesimamia utafiti huo anasema kwamba “watoto hujifunza kupenda vitabu kwa sababu wanavisoma na mtu wanayempenda.”

Ng’ombe Walioridhika Wanatoa Maziwa Mengi

Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Newcastle, Uingereza, wanasema kwamba “ng’ombe aliye na jina hutoa maziwa mengi kuliko yule asiye na jina.” Kwa kweli, kumtendea ng’ombe kwa njia hiyo kutamfanya atoe maziwa zaidi ya lita 284 kwa mwaka kuliko kawaida. Kwa nini? “Kama vile mtu huhisi vizuri anapotendewa kwa upendo, ng’ombe pia hufurahi zaidi na kujisikia akiwa huru anapoonyeshwa upendo moja kwa moja,” anasema Dakt. Catherine Douglas mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Kilimo, Chakula na Maendeleo ya Vijijini. Pia alisema, “Uchunguzi wetu umethibitisha kile ambacho wakulima wenye kujali wamekuwa wakifanya kwa muda mrefu. Unapomtendea ng’ombe kwa upendo, kama vile kumwita kwa jina lake au kushirikiana naye kwa ukawaida tangu utotoni, mbali tu na kuboresha afya yake na mtazamo wake kuelekea wanadamu, utamfanya atoe maziwa mengi zaidi.”