Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtumbwi—Usafiri Unaofaa Zaidi Nchini Kanada

Mtumbwi—Usafiri Unaofaa Zaidi Nchini Kanada

Mtumbwi—Usafiri Unaofaa Zaidi Nchini Kanada

MVUMBUZI Mfaransa, Samuel de Champlain alivuka Bahari ya Atlantiki kwa mashua na kusafiri hadi Mto St. Lawrence ulio katika nchi ya Kanada. Punde si punde akakumbana na maporomoko madogo ya maji ya Lachine huko Montreal. Jitihada zozote za kupitisha mashua zake kwenye maporomoko hayo zingeambulia patupu, akaandika mvumbuzi huyo katika jarida lake mnamo 1603. Msitu wenye miti mingi sana ulifanya iwe vigumu kutembea kwa miguu. Kwa hiyo, Champlain na wenzake walifanya nini ili kuendelea na safari yao?

Walitumia mitumbwi kama walivyowaona wenyeji wa eneo hilo wakifanya. Champlain alisema kwamba “mtu anapotumia mitumbwi, anaweza kusafiri haraka kokote nchini na bila vizuizi na hata anaweza kuabiri kwa urahisi mito midogo na mikubwa.”

Usafiri Unaofaa Zaidi

Kwa kweli, maziwa na mito ya Kanada ilikuwa ndiyo barabara zinazofaa zaidi, na mtumbwi ulionwa kuwa usafiri bora zaidi. Mtumbwi uliwawezesha Wenyeji wa Asili wa Amerika kusafiri, kuwinda, na kusafirisha bidhaa. Bila shaka, mitumbwi ilitengenezwa kwa njia mbalimbali ikitegemea matumizi yake na vifaa vilivyotumiwa. Kwa mfano, watu wanaoishi pwani ya magharibi ya Kanada walitengeneza mitumbwi kwa kuchimba shimo kwenye gogo kubwa la mti mwekundu wa mkangazi. Shimo hilo lilijazwa maji na mawe moto. Hilo lilifanya mti huo kuwa laini na hivyo ungeweza kuchongwa kwa urahisi katika umbo linalofaa. Baadhi ya mitumbwi hiyo ingeweza kubeba mizigo yenye uzito wa tani mbili hivi, na ilisafiri kwa kasi na kwa njia salama baharini, ambapo ilitumiwa kuwinda wanyama wakubwa wa baharini, kutia ndani nyangumi.

Huenda mtumbwi unaojulikana zaidi kati ya mitumbwi ya Amerika Kaskazini ni ule uliotengenezwa kutokana na ganda la nje la mbetula. Kwa sababu ya utomvu fulani ulio ndani ya mbetula, mti huo hudumu kwa muda mrefu na haufyonzi maji. Pia mti huo ni mgumu na unaweza kupindika kwa urahisi. David Gidmark, mtengenezaji wa mitumbwi anasema hivi: “Mtumbwi uliotengenezwa kutokana na ganda la mbetula unaweza kupita kwenye maporomoko yenye nguvu ambayo yanaweza kuharibu mtumbwi uliojengwa kwa mbao na turubai.”

Baadhi ya vitu vinavyotumiwa kutengeneza mtumbwi wa mbetula ni mbao za mbetula na mierezi, mizizi ya misonobari, na utomvu wa mti. Kwa kuwa vitu hivi vyote vinapatikana msituni, mitumbwi ingeweza kurekebishwa kwa urahisi. Isitoshe, mitumbwi hiyo ilikuwa myepesi, kwa hiyo ingeweza kubebwa kwa urahisi kwenye maporomoko hatari na vizuizi vingine. Pia, haikuchafua mazingira kwa kuwa mtumbwi ulipotupwa, ulioza tu kama mti uliokatwa.

Mitumbwi ilijengwa kwa njia yenye kustaajabisha. Mtu mmoja aliyeishi katika karne ya 19 anasema kwamba wenyeji “hawatumii misumari wala skurubu bali kila kitu hushonwa na kufungwa pamoja. Mikunjo, nyuzi na vifundo vimeshonwa kwa ustadi sana hivi kwamba havihitaji kufanyiwa marekebisho yoyote.”

Kabla ya gari-moshi kuanza kutumiwa, mitumbwi ndiyo iliyokuwa njia ya usafiri ya haraka na yenye kutegemeka katika sehemu nyingi za Kanada. Hata baada ya watu kuanza kutumia gari-moshi, mitumbwi haikuacha kutumiwa mara moja, kwa kuwa mara nyingi watu wangetumia njia zote mbili za usafiri.

Mitumbwi ilikuwa muhimu sana katika maisha ya Wenyeji wa Asili wa Amerika Kaskazini hivi kwamba iliathiri utamaduni na imani yao. Kwa mfano, hekaya fulani zinasema kwamba wakati wa gharika kubwa inayotajwa katika Biblia watu waliokolewa kwa kutumia mtumbwi na si safina.

Kuendesha Mitumbwi Leo

Bado mitumbwi inapendwa huko Kanada lakini kwa ajili ya tafrija tu. Inasikitisha kwamba miti ya kutengeneza mitumbwi ya mbetula haipatikani kwa urahisi sasa. Hata hivyo, vifaa vingine kama vile alumini, turubai, mbao, na mseto wa nyuzi na glasi hupatikana kwa urahisi.

Bill Mason, mwendeshaji mashuhuri wa mtumbwi, alisema hivi kuhusu uendeshaji mtumbwi: “Kuendesha mtumbwi katika mito ya zamani ni njia nzuri ya kuyafahamu mazingira na pia kumfahamu Muumba aliyeumba vitu hivyo zamani za kale.” Wengi watakubaliana kabisa na maneno hayo!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

KAYAKI

Watu wa kabila la Inuit huishi katika sehemu ya Kanada isiyo na misitu. Hata hivyo, hilo halikuwazuia kujenga vyombo vya kusafiria majini. Walitumia ngozi ya sili na kuro, na pia mifupa na mbao zilizobebwa na maji hadi kwenye fuo za Aktiki. Mafuta ya wanyama ilitumiwa kuzuia vyombo hivyo kupenya maji. Chombo walichotengeneza kiliitwa kayaki.

Tofauti inayoonekana wazi kati ya kayaki na mtumbwi wa kawaida ni kwamba kayaki ina kifuniko kinachowakinga watu kutokana na jua na mvua na pia kinachozuia maji mengi yasiingie ndani kayaki inapobingirika. Kayaki za kisasa hutengenezwa kutokana na nyuzi za glasi na vifaa vingine.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

Library of Congress