Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ridhika na Rangi ya Ngozi Yako

Ridhika na Rangi ya Ngozi Yako

Ridhika na Rangi ya Ngozi Yako

● Watu fulani wanaoishi Afrika, Asia Kusini, Karibea, na Mashariki ya Kati huhusianisha ngozi nyeupe na mafanikio au huliona kuwa jambo la pekee. Hilo limewafanya wanaume na wanawake fulani katika maeneo hayo waanze kutumia mafuta fulani ili kubadili rangi ya ngozi zao na hata wakati fulani kuhatarisha uhai wao.

Krimu fulani za kubadili rangi zina kemikali aina ya hydroquinone, ambayo huzuia kutokezwa kwa melanini, na hilo linapunguza uwezo wa ngozi wa kujikinga kutokana na miale ya jua (UV). Hydroquinone hupenya ngozi na kusababisha madhara ambayo hayawezi kutibiwa. Matokeo ni kwamba ngozi huanza kuzeeka kabla ya wakati wake. Kemikali hiyo pia inaweza kusababisha kansa. Krimu nyingine huwa na zebaki, ambayo pia ni sumu.

Isitoshe, mtu anapoendelea kutumia krimu hizo, ngozi yake inaweza kuanza kupatwa na upele unaoharibu ngozi, madoadoa, na pia kufanya ngozi kuwa hafifu kiasi cha kutoweza kushonwa anapopata jeraha. Pia baadhi ya kemikali hizo zinapoingia katika damu, zinaweza kuathiri ini, figo, ubongo, au hata kufanya viungo viache kufanya kazi.

Jambo la kushangaza ni kwamba wakati watu fulani weusi wanapotaka kubadili ngozi yao kuwa nyeupe, watu wengi weupe hujaribu kubadili rangi yao. Ni kweli kwamba mtu anapopigwa na jua kwa kiasi anaweza kupata manufaa ya afya. Kwa mfano, jua linaweza kumsaidia mtu atokeze vitamini D. Lakini kupigwa na jua kwa muda mrefu, hasa jua linapokuwa kali kunaweza kuwa hatari. Rangi ya ngozi inapobadilika na kuanza kuwa ya kahawia, inamaanisha kuwa ngozi yako imeathiriwa na hivyo imeanza kujikinga kutokana na miale zaidi ya jua. Lakini ulinzi huo ni wa muda tu. Kwa mfano, ngozi inapobadilika na kuwa rangi ya kahawia inaweza kuzuia miale hiyo kwa asilimia 4 tu. Ingawa kutumia mafuta ya kuzuia miale ya jua isipenye kwenye ngozi kunaweza kukusaidia, hayalindi ngozi isiharibike au kupatwa na kansa fulani kutia ndani kansa inayoathiri chembe za ndani ya ngozi.

Kwa sababu hiyo, Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza “kwamba kila mtu aridhike na rangi ya asili ya ngozi yake,” ambayo “ni hatua muhimu ya kujilinda na madhara yanayoletwa na jua.” Hata hivyo, watu walio na hekima hutilia maanani kile ambacho Biblia huita “mtu wa siri wa moyoni,” ambaye, tofauti na ngozi inayozeeka, huboreka kadiri muda unavyopita!—1 Petro 3:3, 4; Methali 16:31.