Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kulinda Familia Yako Dhidi ya Homa

Kulinda Familia Yako Dhidi ya Homa

Kulinda Familia Yako Dhidi ya Homa

Yesu alipotoa unabii kuhusu mwisho wa mfumo huu wa mambo, alitabiri kwamba “katika mahali pamoja baada ya pengine kutakuwa na tauni.” (Luka 21:11) Homa ni moja kati ya tauni hizo.

HOMA husababishwa na virusi. Virusi hivyo ni vitu vidogo sana ambavyo huingia ndani ya chembe na kuteka kila sehemu ya chembe hizo ili zizaane. Virusi hivyo vya homa ambavyo hushambulia mfumo wa kupumua, vinapitishwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia umajimaji wa mwili unaotokezwa mtu mwenye homa anapopiga chafya, kukohoa, au hata kuzungumza. Tauni hutokea watu wengi sana wanapoambukizwa katika eneo kubwa.

Mbali na wanadamu, wanyama na ndege pia huathiriwa na virusi. Virusi vya homa hugawanywa katika vikundi vitatu, yaani, A, B, na C. Aina ya A ndiyo mara nyingi husababisha homa. Kiini kinachotokezwa na aina hiyo ya virusi kinatambuliwa kutokana na protini mbili zinazopatikana juu ya virusi hivi: hemagglutinin (H) na neuraminidase (N).

Tatizo kuu kuhusu virusi vya homa ni kwamba vinaweza kuzaana haraka huku vikibadilika mara nyingi na pia kiini kimoja kinaweza kuchanganyikana na kingine na kutokeza kiini kipya. Ikiwa kiini kinachotokea ni cha kipekee sana, huenda kingamwili ya mwanadamu ikashindwa kukidhibiti.

Mara nyingi watu hupatwa na homa katika miezi ya baridi. Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kuwa kunapokuwa na baridi, sehemu ya nje ya virusi hutokeza ute unaolinda virusi vikiwa hewani, lakini unayeyuka vinapokuwa ndani ya mfumo wa mwanadamu wa kupumua wenye joto na hivyo kutokeza maambukizo. Baridi haisababishi maambukizo bali inaweza kutokeza hali zinazosaidia virusi hivyo vienee.

Njia za Kujikinga

Serikali nyingi zimetambua umuhimu wa kujitayarisha kwa ajili ya milipuko ya homa. Lakini wewe unaweza kufanya nini? Acheni tuchunguze hatua tatu za msingi za kujikinga:

Imarisha mwili wako: Hakikisha kuwa familia yako inapata usingizi wa kutosha na kula vyakula vitakavyosaidia mwili kuimarisha kinga yake. Hakikisha kwamba unakula matunda, mboga, nafaka, na protini zisizo na mafuta mengi ambazo zitakupa asidi amino zinazohitajika ili kuimarisha mfumo wako wa kinga.

Usiruhusu viini nyumbani: Kwa kadiri unavyoweza, hakikisha kwamba meza ni safi kabisa kila siku. Osha vyombo vya kupikia na vya kula baada ya kuvitumia na uoshe matandiko kwa ukawaida. Tumia sabuni ya kuua viini kupangusa vitu ambavyo watu hugusa kama vile: mlango, simu, kifaa cha televisheni cha kubonyeza kutoka mbali. Ikiwezekana, hakikisha kuna hewa safi ya kutosha.

Dumisha mazoea mazuri ya usafi: Osha mikono yako vizuri kwa sabuni na maji. (Ikiwa inafaa, beba chupa ndogo yenye sabuni ya kuua viini.) Ikiwezekana, usitumie taulo moja kukausha mikono au uso pamoja na mtu mwingine yeyote kutia ndani hata watu wa familia.

Usiguse macho, mapua, au mdomo bila kunawa mikono. Ikiwezekana, tumia shashi kufunika mdomo na mapua unapokohoa au kupiga chafya na uitupe mara moja. Epuka kutumia vifaa pamoja na wengine vinavyoweza kueneza viini, kama vile simu. Watoto wanahitaji kuzoezwa kabisa kuhusu mambo hayo. Mazoea hayo yanafaa kila wakati lakini yanafaa zaidi wakati watu wengi wana homa.

Wajali Watu Wengine

Unaweza kuambukiza wengine siku moja kabla ya dalili za homa kuonekana na siku tano baada ya kuugua. Dalili hizo zinafanana na zile za mafua lakini zinamwathiri mtu zaidi. Zinatia ndani kuongezeka sana kwa joto mwilini, maumivu ya kichwa, kuchoka sana, kohozi kavu, na maumivu ya misuli. Kutokwa na kamasi na matatizo ya tumbo—kama vile kichefuchefu, kutapika, na kuendesha—huwaathiri watoto zaidi kuliko watu wazima. Ikiwezekana, ukiwa na dalili hizo kaa nyumbani ili usiwaambukize wengine.

Pumzika vya kutosha na unywe vinywaji vingi. Dawa za kuua viini zinaweza kusaidia iwapo zitatumiwa mara tu unapoanza kuona dalili. Aspirini (asidi ya acetylsalicylic) haipaswi kupewa watoto ambao wana homa. Unapopatwa na dalili za nimonia kama vile, matatizo ya kupumua, maumivu ya kifua, au maumivu makali ya kichwa yanayoendelea, mwone daktari mara moja.

Mtu anaweza kuogopa sana anapopatwa na homa. Lakini unaweza kukabiliana nayo ikiwa uko tayari. Zaidi ya hilo, unaweza kutazamia wakati ambapo, kama vile Biblia inaahidi, “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”—Isaya 33:24.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

HOMA KALI SANA

Homa ambayo iligunduliwa huko Mexico mnamo 2009 ni aina ya H1N1 inayofanana na homa ya Hispania ya mwaka wa 1918, ambayo iliua mamilioni ya watu. Hata hivyo, homa hiyo ilikuwa pia na vitu fulani vinavyopatikana katika virusi vinavyoathiri nguruwe na ndege.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 28, 29]

NJIA 6 ZA KUJILINDA NA KUWALINDA WENGINE

1. Funika kinywa unapokohoa

2. Nawa mikono

3. Hakikisha nyumba ina hewa safi ya kutosha

4. Dumisha usafi

5. Ukiwa mgonjwa, usitoke nyumbani

6. Epuka kuwagusa wengine

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 29]

KUNAPOKUWA NA MLIPUKO WA HOMA

Kwanza, fuata maagizo ya wahudumu wa afya. Usiwe na wasiwasi au kushtuka kupita kiasi. Hakikisha kwamba unatilia maanani mazoea mazuri yaliyotajwa katika habari hii. Ikiwezekana, epuka maeneo yenye watu wengi. Ikiwa wewe ni mgonjwa, huenda ikafaa kujifunika uso kwa njia inayofaa. Nawa mikono yako kwa ukawaida. Hakikisha una chakula kisichoweza kuharibika upesi unachoweza kutumia kwa majuma mawili kutia ndani dawa na vitu vingine vya kudumisha usafi iwapo hutaweza kwenda dukani kwa sababu ya hali hiyo.

Unapokuwa kazini, mahali pa ibada, au mahali pengine popote palipo na watu wengi, fuata mapendekezo yaliyotolewa. Pia hakikisha kwamba kuna hewa safi ya kutosha mahali ulipo.

[Picha katika ukurasa wa 27]

Virusi vya homa ya H1N1 vilivyoongezwa ukubwa

[Hisani]

CDC/Cynthia Goldsmith