Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Utepe wa Chuma” Unaounganisha Bahari Mbili

“Utepe wa Chuma” Unaounganisha Bahari Mbili

“Utepe wa Chuma” Unaounganisha Bahari Mbili

MIAKA 150 hivi iliyopita, sehemu kubwa ya Kanada, nchi ya pili kwa ukubwa duniani, haikuwa imewahi kutembelewa. Mwanahistoria Pierre Berton anaeleza hivi: “Asilimia 75 ya wakazi waliishi mbali na watu wengine kwenye mashamba,” na hali mbaya ya barabara “ilifanya usafiri uwe jambo gumu sana.” Pia, usafiri wa majini ulitatizwa sana kwani maziwa na mito iliganda na kuwa barafu kwa miezi mitano hivi kwa mwaka.

Kwa sababu ya magumu hayo yote, mnamo 1871, waziri mkuu Sir John A. Macdonald, alipendekeza kwamba reli ijengwe ambayo ingeunganisha Pwani ya Bahari ya Atlantiki na Pwani ya Bahari ya Pasifiki. Ingawa reli ya aina hiyo ilikuwa imejengwa kule Marekani mwaka wa 1869, nchi ya Kanada ilikabili magumu ya kipekee, kama vile upungufu wa pesa, reli hiyo ingepitia eneo kubwa zaidi kuliko ile ya Marekani, na pia idadi ya wakazi wa Kanada ilikuwa asilimia 10 hivi ikilinganishwa na ile ya Marekani. Kiongozi mmoja wa kisiasa wa Kanada, alisema kuwa “wazo hilo ni mojawapo ya mambo ya kipumbavu zaidi kuwaziwa.” Mwingine pia alimdhihaki waziri mkuu na kusema kuwa sasa angependekeza reli ijengwe kuelekea kwenye mwezi.

Pendekezo Ghali Mno

Licha ya hayo, serikali ya Kanada iliahidi kukamilisha ujenzi huo wa reli baada ya miaka kumi. Sandford Fleming, aliyekuwa injinia wa reli Mskoti, alikadiria kuwa ujenzi huo ungegharimu dola milioni 100 hivi, pesa nyingi sana wakati huo. Ingawa ingekuwa rahisi sana kupitisha sehemu fulani ya reli kwenye eneo la Marekani, Macdonald alisisitiza kwamba reli ijengwe kwenye eneo la Kanada pekee bila kupitia nchi nyingine, ili kulinda masilahi ya Kanada iwapo vita vingezuka.

Wawekezaji wengi hawakutaka kushiriki mpango huo, kwa sababu waliuona kuwa ghali sana na pia usiotegemeka. Hata hivyo, kufikia mwaka wa 1875, shirika la reli la Canadian Pacific Railway (CPR) lilianza ujenzi. Lakini miaka kumi baadaye, ujenzi huo ulikuwa karibu kukatishwa. Shirika hilo lilikuwa limeshindwa kulipa deni lake la dola 400,000 za Kanada ambalo lilipaswa kulipa kufikia saa 9, Julai 10. Lakini alasiri hiyohiyo mwendo wa saa 8, Bunge la Kanada lilikubali kutoa mkopo zaidi, na ujenzi ukaendelea.

Magumu ya Ujenzi

Ujenzi wa reli ulipokuwa ukiendelea huko Ontario kaskazini, wafanyakazi walifika mahali palipokuwa na mwamba mkubwa uliokuwa futi moja chini ya ardhi. Hivyo walilazimika kusafirisha mchanga kutoka mbali sana. Huko Kanada ya kati, wakati wa msimu wa baridi kali, viwango vya joto vilishuka kufikia nyuzi 47 Selsiasi chini ya sufuri, na hivyo kusababisha matatizo mengi ujenzi ulipokuwa ukiendelea. Zaidi ya hayo, ilikadiriwa kwamba kiwango cha theluji iliyomwagika kila mwaka ilifikia mamia ya sentimita juu ya ardhi. Eneo la Milima ya Rocky iliyo upande wa magharibi ilisemekana kuwa “mahali ambapo kifo hutokea ghafula.” Walihitaji kujenga madaraja na barabara za chini ya ardhi. Kufanya kazi saa kumi kwa siku ilikuwa kawaida licha ya mvua, matope, au theluji.

Hatimaye, Novemba 7, 1885 (7/11/1885), bila mbwembwe nyingi, msumari wa mwisho ulipigiliwa kwenye eneo la Eagle Pass huko British Columbia, iliyoko magharibi. Kituo hicho kiliitwa Craigellachie, jina linalofanana na kijiji fulani huko Scotland ambalo lilijulikana kwa upinzani wake mkali. Baada ya kuombwa atoe hotuba fupi, meneja mkuu wa CPR alisema hivi kifupi: “Kile tu ninachoweza kusema ni kwamba kazi hii imefanywa vizuri sana.”

Jinsi Watu Walivyoathiriwa

Maelfu ya Wachina waliokuwa wameletwa nchini Kanada ili kushiriki kwenye ujenzi huo, walihakikishiwa kupata ajira ya kudumu kwenye kampuni hiyo ya reli. Mara nyingi kazi ilikuwa yenye kuhatarisha, hasa kwenye Milima ya Rocky. Wengi wa wafanyakazi hao hawakufaulu kupata pesa za kutosha kulipia nauli ya kurudi nyumbani hadi miaka mingi baada ya kazi hiyo kwisha.

Kwa sababu ya reli hiyo, viwanda na biashara zilianzishwa upande wa magharibi wa nchi hiyo, jambo ambalo liliathiri sana tamaduni za hapo awali. Miji na majiji yalianzishwa, na wenyeji wakahamishwa kwenye hifadhi. Njia za biashara za hapo awali, biashara ndogondogo, kama vile mikahawa ya barabarani, ilifungwa. Kwa upande mwingine, inasemekana kwamba ujenzi wa reli hiyo, “ulisaidia jamii iepuke vumbi na matope” na pia “ikawaepusha na athari za majira ya baridi kali.” Zaidi ya hilo, ilichukua siku chache tu kwa vyakula vilivyosafirishwa kutoka nchi za Mashariki, kupitia Pwani ya Bahari ya Pasifiki, kufika kwenye majiji yaliyo upande wa mashariki.

Ingawa treni bado zinatumiwa kusafirisha mizigo nchini Kanada, kuongezeka kwa utumizi wa magari na ndege, kumefanya watu wengi waache kusafiri kwa treni. Hata hivyo, bado watu wengi leo huepuka pilkapilka za maisha ya leo kwa kufurahia mandhari zenye kupendeza wakiwa ndani ya treni yenye kustarehesha kutoka Toronto hadi Vancouver. Kwa hiyo, badala ya kufanya maisha yasonge kwa haraka kama ilivyokuwa hapo mwanzoni, usafiri wa treni umewawezesha abiria wapumzike na kutafakari kuhusu historia yake yenye kupendeza wanaposafiri kutoka bahari moja hadi nyingine wakitumia “utepe wa chuma” wa Kanada.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

KUSHIRIKI TUMAINI LETU KWENYE “UTEPE WA CHUMA”

Bado treni ndiyo njia kuu ya usafiri kwa jamii nyingi za Kanada, hivyo Mashahidi wa Yehova huitumia ili kufikia maeneo ya mbali wakiwa na ujumbe wa Biblia kuhusu Ufalme wa Mungu. (Isaya 9:6, 7; Mathayo 6:9, 10) “Ni rahisi kuzungumza kuhusu Biblia ukisafiri kwenye treni,” Mashahidi wanaeleza, “kwa sababu watu wanataka kujua tunaelekea wapi na tuna kusudi gani.”

Shahidi mmoja anaeleza hivi kuhusu safari ya treni kuelekea hifadhi ya Ojibwa karibu na Ziwa Nipigon, kaskazini mwa Ontario: “Ingawa tulifurahia kuona mandhari na wanyama-mwitu, tulifurahia zaidi kukutana na watu wa huko. Kwa sababu wao hutembelewa na watu wachache tu, walitukaribisha kwa vishindo na vigelegele tulipowasili. Wenyeji fulani walituazima mitumbwi yao, na pia walituruhusu kutumia madarasa yao bila malipo yoyote. Baada ya kuhubiri siku nzima, wenyeji hao walikusanyika pamoja na kutazama video kuhusu kazi yetu ya kuhubiri ulimwenguni kote.”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Sir John A. Macdonald

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kazi ya kujenga reli ilikuwa ngumu sana

[Picha katika ukurasa wa 17]

Madaraja na barabara nyingi za chini ya ardhi zilijengwa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kupigiliwa kwa msumari wa mwisho kulikamilisha ujenzi wa reli iliyounganisha Kanada

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kusafiri leo kwa kutumia “utepe wa chuma”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Top: Canadian Pacific Railway (A17566); middle: Library and Archives Canada/C-006513

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Top, left to right: Canadian Pacific Railway (NS13561-2); Canadian Pacific Railway (NS7865); Library and Archives Canada/PA-066576; bottom: Canadian Pacific Railway (NS1960)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Top: Canadian National Railway Company; right: Courtesy VIA Rail Canada Inc.