Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jifunze Kuhusu Wabatak

Jifunze Kuhusu Wabatak

Jifunze Kuhusu Wabatak

Mvumbuzi Mwitaliano Marco Polo, wa karne ya 13 alipotembelea kisiwa cha Sumatra, huko Indonesia, alieleza kuhusu kabila fulani la “watu wa milimani” ambao, alisema, “wanaishi . . . kama wanyama . . . na wanakula nyama ya wanadamu.” Inadhaniwa kwamba watu aliokuwa akizungumza kuwahusu walikuwa Wabatak. Hata hivyo, mimi na mke wangu tuna maoni tofauti sana kuhusu watu hao. Jifunze kuhusu Wabatak ambao tumewajua na kuwapenda.

“HORAS!” Hivyo ndivyo rafiki zetu wapya Wabatak walivyotusalimu kwa uchangamfu tulipowasili Sumatra Kaskazini, huko Indonesia, kwa ajili ya mgawo wetu mpya wa umishonari karibu na Ziwa Toba. Ziwa hilo ni moja kati ya maeneo ya kiasili yenye kuvutia sana huko Sumatra na ndilo ziwa kubwa zaidi ulimwenguni lililotokezwa na mlipuko wa volkano, na ni kitovu cha Wabatak.—Ona  sanduku lililo hapa chini.

Wabatak ndio kikundi kikubwa zaidi cha wenyeji wa asili wa Indonesia. Kikundi hicho ambacho kina watu milioni nane hivi huenda kimefanyizwa na makabila sita yanayojitegemea lakini yanashirikiana kwa ukaribu. Makabila hayo ni: Toba, Simalungun, Karo, Dairi, Angkola, na Mandailing. Kila kabila limefanyizwa na ukoo mbalimbali wenye familia kubwa. Wabatak wanapokutana, swali la kwanza wao huuliza ni, “Wewe ni wa ukoo gani?” Hivyo mara moja wanajua wana uhusiano wa karibu kadiri gani.

Sheria za Ndoa

Ndoa za kimila za Wabatak haziunganishi tu watu wawili bali pia koo mbili. Ndoa kati ya binamu kutoka upande wa mama huonwa kuwa zinafaa. Lakini ni mwiko kabisa kumwoa binamu kutoka upande wa baba au mtu mliye na ukoo mmoja. Kwa kawaida, ndoa za kimila hufuata mpangilio huu: Wanaume kutoka ukoo A huoa wanawake kutoka ukoo B, wanaume kutoka ukoo B huoa wanawake kutoka ukoo C, na wanaume kutoka ukoo C huoa wanawake kutoka ukoo A. Mpangilio huo huimarisha vifungo vya kiukoo na walioana huwa na watu wengi wa ukoo.

Hata ikiwa wenzi Wabatak wataoana kisheria na kupata watoto, ndoa hiyo haitambuliwi na ukoo wao hadi wafanye harusi ya kimila. Sherehe hizo zenye madoido mengi huwahusisha mamia ya watu wa ukoo na zinaweza kuchukua saa kadhaa.

Kwa mfano, katika harusi ya kabila la Karo, mahari huhesabiwa kwa uangalifu na kugawanywa kati ya vikundi hususa katika kila ukoo. Lazima hilo lifanywe ndipo sherehe ya harusi iendelee. Watu wa ukoo hutoa hotuba ndefu kuhusu maisha ya ndoa. Bwana na bibi-arusi husikiliza kwa heshima. Kisha kunakuwa na karamu na kucheza dansi.

Eneo Lenye Rutuba Sana

Zamani familia nyingi za Wabatak ziliishi pamoja katika nyumba ndefu zilizokuwa na paa zinazofanana na pembe za nyati. Baadhi ya nyumba hizo zenye mapambo zilizojengwa kwa mbao, mianzi, na miwa, zilijengwa juu ya nguzo za mbao na nyingine zilikuwa kubwa sana hivi kwamba familia 12 zingeishi ndani yake. Hazikupigiliwa misumari yoyote. Bado watu wanaishi ndani nyumba kadhaa zilizojengwa miaka 300 iliyopita. Chini ya sakafu iliyoinuliwa, walifuga ng’ombe, kuku, mbwa, nguruwe, na nyati.

Uchumi wa eneo hilo hutegemea hasa ukulima, uvuvi, ufugaji, na vilevile utalii. Kwa kweli, eneo hilo kubwa linalozunguka Ziwa Toba lina rutuba sana. Matuta ya mpunga yenye rangi ya kijani kibichi yanaonekana juu milimani. Kahawa, matunda, na vikolezo, pamoja na mboga za majani hukua katika udongo huo mweusi wa volkano wenye rutuba sana. Wakiwa kwenye mitumbwi yao iliyotengenezwa kwa mbao, wavuvi huvua samaki wengi katika maji safi na yaliyotulia ya ziwa hilo.

Jioni inapofika, watoto wenye furaha huogelea ziwani, wanaume hukutana kwenye mikahawa, na muziki husikika. Kwa kweli, Wabatak wanajulikana kuwa watu wanaoimba kwa nguvu na kwa hisia. Pia wao hupenda kucheza dansi—wanaume wakiwa mbali na wanawake—wakizungusha viganja na mikono yao taratibu.

Historia Yenye Matatizo

Tangu wakati wa Marco Polo hadi kufikia karne ya 19, ilisemekana kwamba Wabatak walikula nyama ya wanadamu, na hasa walikuwa na zoea la kuwala wahalifu na askari-jeshi maadui. Hata hivyo, “huenda Wabatak wenyewe ndio waliotoa habari zenye kutisha kuhusu zoea lao la kula watu ili kuwazuia wageni wasishambulie nchi yao,” anasema Leonard Y. Andaya, profesa wa historia. Kwa vyovyote vile, “katika karne ya 19, serikali ya kikoloni ya Uholanzi ilipiga marufuku ulaji wa watu katika maeneo yaliyokuwa chini ya utawala wake,” kinasema kitabu The Batak—Peoples of the Island of Sumatra.

Wabatak waliabudu maumbile na miungu kadhaa na pia walijihusisha na ushirikina. Pia walitoa dhabihu za matambiko, waliwasiliana na pepo, walifanya uaguzi na uchawi. Mizungu na mbinu mbalimbali za uponyaji za kutumia uaguzi ziliandikwa kwenye ganda la mti lenye urefu wa mita 15, kisha ganda hilo lilikunjwa kama pepeo na kuwa kama kitabu. Pia walifuma nguo takatifu zenye mapambo za kufukuza pepo na kutabiri wakati ujao.

Rekodi zinaonyesha kwamba R. Burton na N. Ward ambao walikuwa Wabaptisti, ndio waliokuwa wamishonari wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika eneo la Wabatak mwaka wa 1824. Miaka kumi baadaye, jeshi la Uholanzi lilipokuwa likijaribu kuteka maeneo fulani ya Indonesia, wamishonari wengine wawili kutoka Marekani, H. Lyman na S. Munson, waliingia katika eneo la Wabatak lakini wakauawa. Wamishonari wawili Wakatoliki ambao walipuuza onyo kwamba wasiingie katika maeneo hatari, huenda pia waliuawa.

Hata hivyo, mmishonari Mjerumani Ludwig Nommensen, ambaye alianza kufanya kazi na Wabatak mwaka wa 1862 hakuuawa na kazi yake ya umishonari ilifanikiwa sana. Bado anaheshimiwa sana na wenyeji wengi. Leo, Wabatak wengi wanadai kuwa Wakristo, na wengine hasa ni Waislamu au waabudu maumbile. Hata hivyo, wengi bado wanafuata baadhi ya desturi zao za kitamaduni.

Habari Njema ya Kweli Yafika

Mnamo 1936, Mashahidi wa Yehova waliwasili katika eneo la Wabatak, wakiwa na habari njema ya Ufalme wa Mungu, ambayo Yesu alisema itahubiriwa “katika dunia yote inayokaliwa.” (Mathayo 24:14) Wabatak wengi walikubali ujumbe huo wa Biblia na kuacha ushirikina. Kwa sababu hiyo, eneo hilo sasa lina makutaniko 30 hivi ya Mashahidi wa Yehova.—Ona  sanduku lililo katika ukurasa huu.

Mimi na mke wangu tunapowaambia watu wa eneo hilo habari njema, mara nyingi sisi hukutana na watalii ambao hustaajabia mandhari maridadi ya Ziwa Toba na hali nzuri ya hewa. Tunakubaliana kabisa nao. Lakini kwa maoni yetu, uzuri hasa wa eneo hilo ni watu wake—Wabatak wachangamfu na wenye urafiki.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

 ZIWA BARIDI LILILOTOKEZWA KWA MOTO

Ziwa Toba lina urefu wa kilomita 87 na upana wa kilomita 27, nalo ndilo ziwa kubwa zaidi ulimwenguni lililotokezwa na mlipuko wa volkano. Lina maji mengi sana baridi ambayo yanaweza kufunika nchi yote ya Uingereza kwa kina cha mita moja hivi. Likiwa limezungukwa na vilele vya milima ya volkano ambayo ni sehemu ya safu ya Milima ya Barisan, ziwa hilo maridadi hupendwa sana na wapiga-picha.

Ziwa hilo lilitokezwa na mlipuko mmoja au zaidi ya volkano, ambayo wanasayansi wanasema kwamba huenda ikawa ndiyo iliyokuwa milipuko yenye nguvu zaidi kuwahi kutokea katika historia. Baada ya muda, shimo kubwa sana lililotokea lilijaa maji na kutokeza Ziwa Toba. Milipuko kadhaa chini ya ziwa hilo ilitokeza Kisiwa maridadi cha Samosir, ambacho kimeenea kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita 647 za mraba, ukubwa unaokaribia ule wa Jamhuri ya Singapore.

[Sanduku katika ukurasa wa 18]

PARADISO YENYE HALI NZURI YA HEWA

Ingawa Ziwa Toba liko kilomita 300 hivi kutoka kwenye ikweta, inashangaza kwamba eneo hilo lina baridi. Sababu ni kwamba ziwa hilo liko mita 900 juu ya usawa wa bahari. Mitende na misonobari hukua kwenye paradiso hiyo yenye joto la kadiri.

Ziwa hilo ndilo huwatenganisha wanyama fulani. Kwa mfano, orangutangu, sokwe wadogo wanaoitwa white-handed gibbon, na tumbili wanaiotwa Thomas’ leaf huishi upande wa kaskazini wa ziwa hilo, huku tapir, tarsier, na tumbili fulani walio na milia hupatikana upande wa kusini.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]

 MCHAWI ANABADILIKA NA KUWA MKRISTO WA KWELI

Nursiah alikuwa ḍukun, au mchawi wa Wabatak. Alitumia ufundi wa uchawi kuponya magonjwa, kufukuza roho waovu, na kuwasiliana na “wafu.” * Biashara yake ilinawiri sana na licha ya matendo yake ya kichawi, alikuwa mshiriki aliyeheshimiwa wa kanisa la Kiprotestanti.

Nursiah alipokutana na Mashahidi wa Yehova, alishangaa kujifunza kwamba jina la Mungu ni Yehova. (Zaburi 83:18) Baadaye, alisoma katika Biblia kwamba katika karne ya kwanza, wengi ambao waligeuka na kuwa waamini waliacha ufundi wa uchawi na kuteketeza vitabu vyao vya uchawi ili wamtumikie Mungu kwa njia inayokubalika. (Matendo 19:18, 19) Nursiah aliamua kufanya hivyo licha ya upinzani mkali, akiwa na uhakika kamili katika maneno ya Yesu: “Kweli itawaweka ninyi huru.”—Yohana 8:32.

Leo, Nursiah pamoja na mwana wake Besli, ni Mashahidi waliobatizwa, na mume wake, Nengku, anahudhuria mikutano ya Kikristo kwa ukawaida. Nursiah anasema: “Maisha yangu yameboreshwa kwa kumtumikia Yehova. Nilipokuwa ḍukun, nilitamani sana kujua kweli. Sasa nimeridhika kabisa.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 31 Ona habari “Maoni ya Biblia: Roho Waovu Ni Nani?,” kwenye ukurasa wa 20.

[Picha]

Nursiah, mume wake, na mwana wao

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sumatra

Ziwa Toba

[Hisani]

Based on NASA/Visible Earth imagery

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Ziwa Toba unapolitazama kutoka Mlima Pusuk Buhit

[Picha katika ukurasa wa 18]

Poromoko la maji la Sipisopiso, lililo katika ncha ya kaskazini ya Ziwa Toba, lenye urefu wa mita 110