Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Shirika la Kimataifa la Uchunguzi wa Kansa limebadili maoni kuhusu utumizi wa vifaa vinavyotumia miale ya urujuanimno kubadili rangi ya ngozi. Badala ya kusema kuwa “huenda vinasababisha kansa kwa wanadamu” shirika hilo sasa linasema kwa hakika kwamba vifaa hivyo “vinasababisha kansa kwa wanadamu.”—THE LANCET ONCOLOGY, UINGEREZA.

Nchini Argentina, wanawake 9 kati ya 10 ambao ni wajawazito walipata mimba bila kutaka.—CLARÍN, ARGENTINA.

“Ni jambo la kawaida kwa wanasayansi kugundua spishi mpya. Inakadiriwa kwamba wanabiolojia wanatambua spishi 50 kila siku. Karibu mimea na wanyama 17,000 walitambuliwa kuwa spishi za pekee katika mwaka wa 2006 tu, hiyo ni asilimia 1 ya spishi milioni 1.8 hivi ambazo zimepewa majina.”—TIME, MAREKANI.

Je, Kuwa na Bunduki Ni Ulinzi?

Je, mashambulizi yanapotokea, mtu anaweza kupata ulinzi akiwa na bunduki? Uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Kitiba cha Pennsylvania, Marekani, ulionyesha kwamba kwa wastani, bunduki haiwezi kumlinda mtu. Mbali na visa vinavyohusisha polisi, mtu kujipiga risasi, na kufyatuliwa risasi kimakosa, watafiti waligundua kwamba kuna uwezekano “mara 4.5 [kwa mtu aliye na bunduki] kupigwa risasi kuliko mtu asiye na bunduki.” Uchunguzi huo ulionyesha kwamba watu fulani walio na bunduki hufanikiwa kujilinda kwa kutumia silaha zao, lakini kuna uwezekano mdogo wa kufanikiwa. Ripoti hiyo ilisema kuwa wazo la kwamba kuwa na bunduki “ni njia ya kujilinda kunapokuwa na hatari linapaswa kuzungumziwa na kufikiriwa tena kwa uangalifu.”

Watawa Wanajipaka Rangi Midomoni

Ripoti fulani ya habari kutoka Bangkok inasema kwamba watawa wapya wa kiume huko Thailand wamekuwa “wakichafua jina la dini ya Budha,” kwa kupaka midomo rangi, kuvalia kanzu zenye kuwabana sana, “wakitembea kwa madaha huku wakizungusha viuno vyao mno wakiwa wamebeba vibeti.” Mwenendo wa watawa wapya wa kiume ambao pia ni mashoga umewafanya viongozi wa dini hiyo kuamua kuwafunza watawa hao mwenendo unaofaa. Mhubiri mmoja mashuhuri wa Budha alieleza kwamba ushoga haujapigwa marufuku kati ya watawa, “kwani kufanya hivyo kutamaanisha kwamba karibu watawa wote watavuliwa utawa.”

Treni za Wanawake Pekee

Kwa miaka mingi huko India wanawake ambao wamesafiri kwa treni za umma zilizojaa kupita kiasi walikuwa wakitendewa vibaya kwani walitukanwa, wakashikwashikwa, wakachunwa, wakatazamwa kimahaba, na kwa ujumla walidhulimiwa na abiria wanaume. Kwa sababu ya malalamishi hayo, serikali imeamua katika visa fulani kuwaondoa kabisa wanaume katika treni hizo, linaripoti gazeti The Telegraph la Calcutta. Kwa sababu hiyo, katika majiji manne makubwa zaidi ya India, yaani, New Delhi, Mumbai, Chennai, na Calcutta, kuna treni kwa ajili ya wanawake peke yao. Inasemekana kwamba wanawake wamefurahi sana.