Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mchochota wa Ini Aina ya B—Ugonjwa Unaoua Kimyakimya

Mchochota wa Ini Aina ya B—Ugonjwa Unaoua Kimyakimya

Mchochota wa Ini Aina ya B—Ugonjwa Unaoua Kimyakimya

“Nilikuwa na umri wa miaka 27, nilikuwa nimetoka tu kuoa, na nilijihisi na kuonekana kuwa mwenye afya. Nilikuwa na kazi yenye mkazo sana na majukumu mengi katika kutaniko letu la Mashahidi wa Yehova. Sikujua kwamba mchochota wa ini aina ya B ulikuwa umeanza kuharibu ini langu.”—Dukk Yun.

INI huchuja sumu kutoka kwenye damu na kufanya kazi nyingine muhimu 500. Kwa sababu hiyo, mchochota wa ini, yaani, uvimbe katika ini unaweza kuharibu afya ya mtu. Mchochota wa ini unaweza kusababishwa na kunywa kileo kupita kiasi au sumu inapoingia mwilini. Hata hivyo, mara nyingi ugonjwa huo husababishwa na virusi. Wanasayansi wamegundua virusi vitano vinavyosababisha ugonjwa huo na wanasema kwamba huenda kuna vingine vitatu.—Ona  sanduku lililo hapa chini.

Moja tu kati ya virusi hivyo vitano—virusi vya mchochota wa ini aina ya B (HBV)—huua watu 600,000 hivi kila mwaka, idadi ya watu inayolingana na wale wanaokufa kutokana na malaria. Zaidi ya watu bilioni mbili, yaani, asilimia 33 hivi ya watu wote ulimwenguni, wameambukizwa virusi vya HBV, na wengi wao hupona baada ya miezi michache. Watu milioni 350 hivi huendelea kuwa na virusi hivyo mwilini. Maisha yao yote, iwe wana dalili za ugonjwa huo au la, watu hao wanaweza kuwaambukiza wengine. *

Mtu aliye na virusi vya HBV mwilini akianza matibabu mapema, anaweza kuzuia ini lake lisiharibike sana. Lakini watu wengi hawajui kwamba wameambukizwa kwa kuwa ni uchunguzi fulani hususa wa damu unaoweza kuonyesha virusi hivyo. Hata uchunguzi wa kawaida wa kuangalia utendaji wa ini unaweza kukosa kuonyesha virusi hivyo. Kwa hiyo, mchochota wa ini aina ya B unaweza kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote. Huenda dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa. Zinapoonekana, huenda tayari ini limenyauka au lina kansa, na magonjwa hayo huua asilimia 25 ya watu walio na virusi vya HBV.

“Niliambukizwa Virusi Hivyo Namna Gani?”

Dukk Yun anasema hivi: “Dalili zilianza kuonekana nilipokuwa na umri wa miaka 30. Nilianza kuharisha, kwa hiyo, nilienda kumwona daktari hospitalini ambaye alitibu dalili tu. Kisha nikaenda kwa daktari wa miti-shamba kutoka Asia ambaye alinipa dawa ya tumbo. Madaktari wote wawili hawakuchunguza ikiwa nilikuwa na mchochota wa ini. Kwa kuwa niliendelea kuharisha, nilirudi hospitalini kwa daktari aliyenitibu mara ya kwanza. * Aligonga polepole upande wa kulia wa tumbo langu, nami nikahisi maumivu. Uchunguzi wa damu ulithibitisha kwamba nilikuwa na virusi vya mchochota wa ini aina ya B. Nilishtuka sana! Sijawahi kutiwa damu mishipani wala kujihusisha katika mwenendo mpotovu kingono.”

Baada ya Dukk Yun kujua kwamba alikuwa na virusi hivyo, mke wake, wazazi wake, na ndugu na dada zake walipimwa na ikaonekana kwamba damu yao ilikuwa na kingamwili za kupingana na virusi hivyo. Lakini mifumo yao ya kinga tayari ilikuwa imeondoa virusi hivyo mwilini. Je, Dukk Yun aliambukizwa virusi hivyo na mtu fulani katika familia yake? Je, wote walikuwa wameambukizwa kutoka chanzo kimoja? Hakuna aliyejua. Kwa kweli, asilimia 35 hivi ya watu hawajui jinsi walivyoambukizwa. Hata hivyo, kinachojulikana ni kwamba virusi vya mchochota wa ini aina ya B havirithiwi na haviambukizwi kwa kumgusa mtu aliye na virusi hivyo au kula chakula pamoja naye. Badala yake, mtu huambukizwa virusi hivyo wakati damu au umajimaji mwingine wa mwili kama vile mate, shahawa, au umajimaji unaotoka katika sehemu ya uke ya mtu aliyeambukizwa unapoingia kwenye mfumo wa damu kupitia kidonda kwenye ngozi au tando-telezi za mwili.

Watu wengi wanaendelea kuambukizwa kwa kutiwa damu yenye virusi hivyo, hasa katika nchi ambako hakuna vifaa bora vya kuchunguza virusi hivyo katika damu. Virusi vya HBV vina uwezo mkubwa zaidi wa kuambukiza kwa kulinganishwa na virusi vya UKIMWI. Hata kiasi kidogo sana cha damu yenye virusi hivyo kama ile inayobaki kwenye wembe, inaweza kupitisha virusi hivyo, na tone la damu iliyokauka kwa juma moja au hata zaidi inaweza kumwambukiza mtu virusi hivyo. *

Watu Wanapaswa Kufundishwa

“Wasimamizi wa kampuni niliyokuwa nikifanya kazi walipojulishwa kwamba nina virusi vya mchochota wa ini aina ya B, waliniweka kwenye ofisi ndogo mbali na wafanyakazi wenzangu,” anasema Dukk Yun. Hilo ni jambo la kawaida kwa kuwa watu wengi hawaelewi jinsi ambavyo virusi hivyo vinaambukizwa. Hata wale walio na habari zaidi kuhusu ugonjwa huo hawawezi kutofautisha katika ya mchochota wa ini aina ya B na mchochota wa ini aina ya A, ambao huambukizwa kwa urahisi sana lakini si rahisi usababishe kifo. Pia, kwa kuwa mchochota wa ini aina ya B unaweza kuambukizwa kupitia kufanya ngono, nyakati nyingine hata watu wenye maadili mazuri ambao wana virusi hivyo hutiliwa shaka.

Madhara makubwa yanaweza kutokea watu wanapokosa kuelewa ugonjwa huo vizuri au wanapowatilia shaka wenye virusi hivyo. Kwa mfano, katika maeneo mengi, watu wanawatenga watu walio na virusi vya HBV, wawe vijana au wazee. Majirani hawawaruhusu watoto wao kucheza nao, wanafukuzwa shuleni, na waajiri wanawanyima kazi. Kwa sababu ya kuogopa kubaguliwa, watu hawaendi kupimwa au hawawaelezi wengine kwamba wana ugonjwa huo. Badala ya kusema ukweli wengine hata huhatarisha afya yao na ya familia zao. Kwa hiyo, ugonjwa huo unaweza kupitishwa kwa vizazi vingi.

Kupumzika Ni Muhimu

“Ingawa daktari wangu alikuwa ameniagiza nipumzike kabisa, nilirudi kazini baada ya miezi miwili,” anasema Dukk Yun. “Uchunguzi mbalimbali wa damu na eksirei za hali ya juu zilionyesha kwamba ini langu lilikuwa sawa, kwa hiyo nilidhani niko sawa.” Miaka mitatu baadaye, kampuni aliyokuwa akifanyia kazi ilimhamisha Dukk Yun hadi kwenye jiji kubwa na maisha yake yakawa na mkazo zaidi. Kwa kuwa alihitaji kulipia gharama za kawaida na kuitunza familia yake, aliendelea kufanya kazi.

Katika muda wa miezi michache, virusi hivyo viliongezeka sana katika damu ya Dukk Yun, naye akaanza kujihisi mchovu. Anasema hivi: “Ilinibidi niache kazi, na sasa ninajuta kwamba nilifanya kazi sana. Laiti ningalipunguza kazi yangu mapema, nisingalikuwa mgonjwa sana na kudhuru ini langu hata zaidi.” Dukk Yun alijifunza jambo muhimu. Kuanzia wakati huo, alipunguza muda aliotumia kazini na pia akaacha kutumia pesa nyingi. Isitoshe, familia yake yote ilimuunga mkono, hata mke wake alitafuta kazi ndogo ili kusaidia kulipia gharama.

Kuishi Ukiwa na Mchochota wa Ini Aina ya B

Ingawa Dukk Yun alipata nafuu, ini lake halingeweza kupitisha damu na hilo lilifanya shinikizo la damu lipande. Baada ya miaka 11, mshipa fulani kwenye umio lake ulipasuka na kumwaga damu kwenye koo lake, jambo ambalo lilimfanya alazwe hospitalini kwa juma moja. Miaka minne baadaye alianza kuvurugika kiakili. Kulikuwa na amonia nyingi ndani ya ubongo wake kwa sababu ini lake halingeweza kuichuja yote. Hata hivyo, tatizo hilo lilitibiwa kwa dawa na hivyo akapata nafuu baada ya siku chache.

Sasa Dukk Yun ana umri wa miaka 54. Hali yake ikizorota, kuna matibabu machache sana ya kudhibiti ugonjwa huo. Dawa za kuua virusi haziwezi kuondoa kabisa virusi hivyo mwilini na huenda zikaleta madhara mengine. Matibabu yanayobaki tu ni kupandikizwa ini, lakini wale wanaongojea kupandikizwa ni wengi kuliko wale walio tayari kutoa ini lao. Dukk Yun anasema, “Ninaweza kufa wakati wowote, lakini hakuna faida kufikiria sana hali hiyo. Bado kuna mambo ninayoweza kufanya maishani, nina mahali pa kulala, na familia nzuri. Kwa kweli, hali yangu imeniletea baraka ambazo sikutarajia. Sasa ninatumia wakati mwingi pamoja na familia yangu na pia nina wakati mwingi wa kujifunza Biblia. Hilo hufanya nisiogope kifo cha ghafula na kunisaidia kutazamia wakati ujao ambapo hakutakuwa na magonjwa.” *

Kwa sababu Dukk Yun ana mtazamo unaofaa, familia yake inaishi maisha yenye furaha na yeye pamoja na mke wake, na watoto wao watatu ni wahubiri Wakristo wa wakati wote.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Virusi hivyo hudumu mwilini ikiwa mfumo wa kinga wa mwili haujaviondoa katika muda wa miezi sita.

^ fu. 7 Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa.

^ fu. 9 Damu kutoka kwa mtu mwenye virusi hivyo inapaswa kupanguswa haraka na vizuri mtu akiwa amevaa glavu kwa kutumia kipimo 1 cha dawa ya kuondoa madoa kilichochanganywa na vipimo 10 vya maji.

^ fu. 18 Kuhusu tumaini la Biblia la wakati ambapo hakutakuwa na magonjwa, soma Ufunuo 21:3, 4 na pia kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa?

[Blabu katika ukurasa wa 13]

Kutibiwa mapema kunaweza kupunguza madhara

[Blabu katika ukurasa wa 14]

Kwa sababu ya kuogopa kubaguliwa, wengi hawaendi kupimwa au hawawaelezi wengine kwamba wana ugonjwa huo

[Sanduku katika ukurasa wa 12, 13]

 NI AINA GANI YA MCHOCHOTA WA INI?

Kuna virusi vitano vinavyojulikana kusababisha mchochota wa ini, na vile vitatu vinavyojulikana sana hupewa alama ya A, B, na C. Bado kuna vingine vinavyodhaniwa kuwa vinasababisha ugonjwa huo. Aina zote za mchochota wa ini huwa na dalili kama za homa na huenda zikatia ndani homa ya nyongo manjano. Watu wengi, hasa watoto hawaonyeshi dalili zozote. Dalili za mchochota wa ini aina ya B na C zinapoonekana, huenda tayari ini huwa limeharibika sana.

MCHOCHOTA WA INI AINA YA A (HAV)

Virusi vya ugonjwa huu hupatikana katika kinyesi cha mtu aliyeambukizwa. Virusi hivyo vinaweza kuendelea kuishi katika maji ya chumvi, maji baridi, au vipande vya barafu. Mtu anaweza kuambukizwa HAV kwa

Kula nyama mbichi ya viumbe wa baharini ambao wamekunywa maji yenye virusi hivyo au waliovuliwa katika maji yaliyochafuliwa na kinyesi cha mwanadamu

Kushirikiana kwa ukaribu na mtu aliyeambukizwa au kula, kunywa katika chombo kilekile, au kutumia vyombo vya kulia alivyotumia

Kukosa kunawa mikono vizuri baada ya kwenda chooni au kumbadilisha nepi mtoto aliyeambukizwa, au kutayarisha chakula bila kunawa mikono

HAV husababisha ugonjwa mkali lakini si wa kudumu. Karibu katika visa vyote, mwili huondoa virusi hivyo mwilini baada ya majuma au miezi michache. Hakuna matibabu hususa isipokuwa kupumzika na kula vyakula vyenye lishe. Mtu anapaswa kuepuka pombe, na pia dawa ambazo haziwezi kuchujwa kwa urahisi na ini kama vile dawa ya acetaminophen, hadi daktari atakaposema kuwa ini limepona kabisa. Huenda mtu aliyeugua HAV asiambukizwe virusi hivyo tena lakini anaweza kuambukizwa aina nyingine ya mchochota wa ini. Chanjo inaweza kuzuia mtu asiambukizwe HAV.

MCHOCHOTA WA INI AINA YA B (HBV)

Virusi vya HBV hupatikana katika damu, shahawa, na umajimaji unaotoka kwenye sehemu za uke za watu walioambukizwa. Virusi hivyo huambukizwa wakati umajimaji huo unapoingia mwilini mwa mtu asiye na kinga. Virusi hivyo vinaweza kupitishwa

Mama anapojifungua (mama mwenye virusi hivyo anaweza kuvipitisha kwa mtoto wake)

Vifaa vya kitiba, matibabu ya meno, au vya kuchanja mwili visiposafishwa vizuri

Mtu anapotumia vitu ambavyo vimetumiwa na mtu mwingine kama vile sindano, wembe, vitu vya kukata kucha, miswaki, au kitu chochote kile kinachoweza kupitisha kiasi kidogo cha damu kupitia kidonda kwenye ngozi

Kupitia kufanya ngono

Wataalamu wa kitiba wanasema kwamba virusi vya HBV haviambukizwi kupitia wadudu, au kwa kukohoa, kushikana mikono, kukumbatiana, kupigana busu kwenye mashavu, kunyonyesha, au kula chakula au vinywaji katika chombo kimoja, vijiti vya kulia, au vyombo vingine vya kulia. Watu wazima wengi wenye virusi hivyo hupona na huwa na kinga ya ugonjwa huu. Ni rahisi sana kwa virusi hivyo kudumu katika damu ya watoto wadogo. Usipotibiwa, mchochota wa ini aina ya B unaweza kusababisha ini liache kufanya kazi na hatimaye kutokeza kifo. Kuna chanjo ya kuzuia ugonjwa huo.

MCHOCHOTA WA INI AINA YA C (HCV)

HCV huambukizwa kwa njia ileile kama HBV, lakini mara nyingi unaambukizwa kupitia kujidunga dawa za kulevya mishipani kwa kutumia sindano zilizoambukizwa. Hakuna chanjo ya mchochota wa ini aina ya C. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 46 Shirika la Afya Ulimwenguni linatoa habari zaidi kuhusu mchochota wa ini katika lugha mbalimbali katika Tovuti yao, www.who.int.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

KUZUIA KUENEA KWA HBV

Ingawa HBV huathiri watu ulimwenguni pote, asilimia 78 hivi ya wale ambao virusi hivyo vimedumu mwilini huishi Asia na katika visiwa vya Pasifiki. Katika mengi ya maeneo hayo, mtu 1 kati ya watu 10 ana virusi hivyo. Wengi wao huambukizwa virusi hivyo kutoka kwa mama zao wanapozaliwa au utotoni kupitia damu ya watoto wenye virusi hivyo. Chanjo kwa ajili ya watoto waliotoka tu kuzaliwa na watu walio katika hatari ya kuambukizwa imesaidia kuzuia kuenea kwa virusi hivyo. * Katika maeneo ambayo chanjo hiyo imetumiwa, maambukizo yamepungua sana.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 51 Huenda chanjo ya mchochota wa ini ikatengenezwa kutokana na visehemu vya damu. Ikiwa ungependa habari zaidi, soma “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika toleo la Juni 15, 2000 (15/6/2000) na toleo la Oktoba 1, 1994 (1/10/1994) la Mnara wa Mlinzi. Habari zaidi pia inaweza kupatikana kwenye ukurasa wa 215 wa kitabu “Jitunzeni Katika Upendo wa Mungu,” Kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Dukk Yun, mke wake, na watoto wao watatu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

© Sebastian Kaulitzki/Alamy