Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mbegu Ndogo Yatokeza Mwaloni Mkubwa

Mbegu Ndogo Yatokeza Mwaloni Mkubwa

Mbegu Ndogo Yatokeza Mwaloni Mkubwa

Mbegu ndogo sana inaanguka chini kutoka kwenye mti. Kindi anayekimbia-kimbia anazika mbegu hiyo, kisha inachipuka baada ya muda. Mbegu hiyo inakua na kutokeza mwaloni mkubwa sana, mti mkubwa zaidi katika misitu ya Uingereza.

Mwaloni ambao umetajwa mara nyingi hata katika hadithi, unaweza kuishi kwa zaidi ya miaka elfu moja. Baadhi ya miti hiyo hufikia kimo cha mita 40! Mialoni ambayo imekuwepo kwa miaka mingi inajulikana kwa mashina yao makubwa na matawi yao yaliyosambaa. Ingawa kuna aina mbili za kiasili za mwaloni nchini Uingereza, kuna aina 450 hivi ulimwenguni. Aina zote hizo hutambuliwa kwa mbegu yake ndogo.

Kwa kulinganishwa na miti mingine nchini Uingereza, mwaloni ndio huandaa makao kwa viumbe wengi zaidi. Wanatia ndani wadudu wa aina nyingi sana. Viwavi wengi hupenda kula majani yake laini yanayotokea wakati wa kiangazi. Lakini mti huo hujikinga. Majani yanayokomaa hutokeza kemikali isiyo na ladha nzuri.

Kila sehemu ya mti huwa na viumbe. Aina nyingi za wadudu wanaoishi kwenye mti huo, huwavutia ndege mbalimbali na pia buibui. Mbawakawa hutoboa maganda ya mti huo. Bundi na vikundi vya popo huishi ndani ya mashimo kwenye mashina yake. Wanyama wadogo kama vile panya, panyabuku, melesi, sungura, na mbweha huishi katikati ya mizizi yake.

Mwaloni una njia yake ya pekee ya kuondoa majani na mbegu zake zilizoanguka. Kila mwaka, mwaloni uliokomaa hupukuta majani 250,000 hivi. Kuvu na bakteria hushirikiana kufanya majani yaliyoanguka yaoze na kufanya madini yarudi udongoni. Kwa miaka fulani, mwaloni unaweza kutokeza mbegu 50,000. Nyingi ya mbegu hizo hukusanywa au kuliwa na ndege na wanyama pia. Utitiri na mbawakawa hula sehemu za mti huo zilizooza, na kuvu hula maganda yake.

Mbao za mwaloni ni ngumu sana na hudumu kwa muda mrefu. Kwa muda mrefu, zimetumiwa kujenga nyumba na vifaa vingine vya mbao. Zinafaa sana kutengenezea mapipa ya kuhifadhi divai na pombe ili ikomae. Na mashua zenye nguvu zilizojengwa kwa mbao za mwaloni zilisaidia Jeshi la Wanamaji la Uingereza kushinda vita dhidi ya maadui wake kwa miaka mingi.

Bado mbao za mwaloni zina thamani sana. Na mti huo ambao ni sehemu muhimu katika mandhari ya Uingereza, unapendwa sana kwa sababu una nguvu, unategemeka, na una uwezo wa kudumu kwa muda mrefu. Ndiyo, mbegu ndogo sana inatokeza mwaloni mkubwa sana—maajabu ya uumbaji!

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mwaloni unaweza kuishi zaidi ya miaka elfu moja na kufikia kimo cha mita 40 na upana wa mita 12 na sentimita 30

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Tree: © John Martin/Alamy; acorn: © David Chapman/Alamy