“Mfalme wa Mwituni” wa Amerika
“Mfalme wa Mwituni” wa Amerika
YEYE ni nani? Ni jaguar, chui mkubwa wa Amerika. Anapatikana wapi? Katika misitu, vinamasi, jangwani, na maeneo mengine kama hayo ya Amerika ya Kati na Kusini. Tofauti na wanyama wengi wa jamii ya paka, chui huyu anaweza kuishi kwenye nchi kavu, juu ya miti, na pia ndani ya maji.
Jiwazie ukiwa umesimama kando ya jaguar wa kiume aliyekomaa. Huenda akawa na urefu wa mita mbili hivi, bila kutia ndani mkia, na uzito wa kilogramu 120 au zaidi. Kwa kuwa ni mnyama anayependa kujitenga, yeye hukutana na jaguar wengine kwa ajili tu ya kuzaliana. Jaguar wa kiume huwa na uwezo wa kuzalisha wanapofikia umri wa miaka mitatu au minne, nao wa kike wanaweza kuzaa wanapokuwa na umri wa miaka miwili. Kwa kawaida wao huzaa watoto wawili baada ya kubeba mimba kwa miezi mitatu au minne. Imesemekana kwamba jaguar fulani wamewahi kuishi kwa zaidi ya miaka 20 katika hifadhi za wanyama.
Mwanabiolojia mmoja alisema hivi kuhusu mnyama huyo asiyeonekana kwa urahisi: “Ni vigumu sana kuwaona jaguar! Ninaweza kuwa nimesimama kando ya mmoja wao, . . . lakini bado nikose kumwona.” Ngozi ya chui huyo ya kahawia iliyo na madoa madogo meusi yaliyozungukwa na mengine makubwa, humsaidia kujificha na kutokomea msituni bila kuonekana.
Anawinda Peke Yake Akiwa Kimya
Jaguar ni mwindaji stadi ambaye hula aina 85 hivi za wanyama kutia ndani, tapir, mbawala, na tumbili. Kwa kuwa anaweza kuishi majini, jaguar pia huvua samaki na kasa kwa urahisi. Wakati mmoja watu fulani walimwona jaguar akimwua farasi aliyekomaa, akamburuta umbali wa mita 80 hivi kwenye nchi kavu kisha akavuka naye hadi upande mwingine wa mto.
Mara nyingi chui huyo mwerevu husubiri mawindo yake akiwa kimya juu ya mti. Aina fulani ya nguruwe-mwitu wanapopita chini ya mti huo bila kujua lolote, anawarukia mara moja na kumwua mmoja kwa kumwuma kwa nguvu kisha anaruka tena juu ya mti. Akiwa hapo, anasubiri nguruwe-mwitu hao wapite kisha anateremka na kuchukua windo lake.
Hata hivyo, kati ya wanyama wote wa jamii ya paka, si rahisi kwa jaguar kumshambulia mtu na hawali wanadamu. Kwa kweli, wanadamu ndio wanaoweza kumdhuru.
Kwa Nini Ni Wachache Sana?
Wakati mmoja jaguar walipatikana katika maeneo ya kusini mwa Marekani hadi mwisho wa Amerika Kusini. Leo, chui hao wanapatikana tu katika nusu ya makao ambayo waliishi miaka 100 iliyopita. Kufikia katikati ya miaka ya 1970, wawindaji waliwaua maelfu ya jaguar kila mwaka kwa ajili ya ngozi yao. Katika mwaka wa 1968 pekee, zaidi ya ngozi 13,500 zilisafirishwa
kutoka katika maeneo ya Amerika. Mnamo 2002, ilikadiriwa kwamba ni jaguar wasiozidi 50,000 ambao wanasalia. Sasa huenda ni 15,000 hivi ambao wanapatikana msituni.Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Wanyama-Pori unasema kwamba asilimia 40 hivi ya makao ya kiasili ya jaguar yameharibiwa kwa sababu ya ukataji wa miti. Nchini Mexico pekee, makao yanayotoshana na uwanja wa mpira yanatoweka kila dakika. Hilo humfanya jaguar aanze kuwinda mifugo ili aendelee kuishi.
Jitihada za Kumlinda
Nchi 200 hivi zinaunga mkono sheria za Mkataba wa Kupinga Biashara ya Kimataifa ya Viumbe na Mimea Inayokabili Hatari ya Kutoweka zinazosema kwamba ni kosa kuwawinda jaguar kwa ajili ya faida za kibiashara. Mbuga za taifa zimeanzishwa ili kulinda makao yao ya asili. Mnamo 1986, Hifadhi ya Wanyama ya Cockscomb huko Belize ilikuwa ndiyo hifadhi ya kwanza ya jaguar ulimwenguni. Kwa kuongezea, Mexico imetenga zaidi ya ekari 370,000 za msitu ndani ya Hifadhi ya Calakmul kwenye Rasi ya Yucatán ili kuwalinda jaguar.
Bado tunasubiri tuone ikiwa jitihada hizo za wanadamu za kumhifadhi ‘mfalme huyo wa mwituni’ zitafanikiwa. Lakini bado tunaweza kufarijiwa kujua kwamba hivi karibuni Muumba wetu mwenye upendo ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia’ na kwamba baada ya muda kutakuwa na amani kati ya wanadamu na wanyama kama vile Mungu alivyokusudia.—Ufunuo 11:18; Isaya 11:6-9.
[Ramani katika ukurasa wa 24, 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Eneo la Jaguar
□ Walipopatikana zamani
▪ Wanapopatikana leo
AMERIKA KASKAZINI
AMERIKA YA KATI
AMERIKA KUSINI