Upweke Katika Ulimwengu Uliojaa Mawasiliano
Upweke Katika Ulimwengu Uliojaa Mawasiliano
SIMU za mkononi, ujumbe mfupi, barua-pepe, vituo vya mawasiliano, vituo vya maongezi—hakujawahi kuwa na pindi ambapo kuna njia nyingi za kuwasiliana kama leo. Hata hivyo, katika ulimwengu huu wenye njia nyingi za mawasiliano, watu wengi, vijana kwa wazee, ni wapweke sana. Kwa nini?
Katika kitabu chao Loneliness—Human Nature and the Need for Social Connection, watafiti John T. Cacioppo na William Patrick wanazungumzia kwa undani kuhusu upweke. Wanazungumzia uchunguzi mmoja uliosema kwamba “kutumia sana Intaneti badala ya kuzungumza na mtu moja kwa moja, kunaweza kufanya watu wajitenge na jamii na pia kuongeza kushuka moyo.”
Hekaheka za maisha ya kisasa zinafanya iwe vigumu kwa watu kuwasiliana kwa njia inayofaa. Kwa kawaida, huwezi kuona uso wenye tabasamu na upendo unapowasiliana na mtu kupitia simu au kwa kutuma ujumbe kupitia kompyuta.
Zaidi tu ya kutokea kazini, mambo yaliyotajwa hapa juu hutokea pia katika familia. Katika nyumba nyingi, watu wa familia huja na kuondoka bila kula pamoja au kuzungumza pamoja. Vijana wana kompyuta zao wenyewe nao hujitenga na watu wengine wa familia. Licha ya kwamba wana vifaa vingi vya mawasiliano, vijana wengi hujihisi wakiwa wapweke.
Siku hizi hata ndoa zinaweza kuhatarishwa kwa sababu ya wenzi kujihisi wakiwa wapweke. Wenzi wa ndoa wasipowasiliana, wanaweza kuwa katika nyumba moja lakini kila mtu anaishi maisha yake. Kuhisi upweke huku ukiwa unaishi na mwenzi wa ndoa ni upweke unaofadhaisha sana.
Wazazi wasio na mwenzi hasa wanaweza kupatwa na hisia za upweke. Mbali na vitu vingine vingi, kuwepo kwa vifaa vingi sana vya mawasiliano kunaweza kukatiza mawasiliano kati ya mzazi na watoto na hivyo kufanya hisia za upweke ziongezeke. Pia waseja wengi wanatamani kuwa na mwenzi, lakini mahitaji yao ya kihisia hayatoshelezwi.
Upweke umekuwa tatizo kubwa katika jamii ambalo linaweza kusababisha uraibu wa kileo, kula kupita kiasi, kutumia dawa za kulevya, kufanya ngono ovyoovyo, na hata kujiua. Kwa hiyo, ni muhimu kutambua visababishi vya upweke. Kuchukua hatua hiyo ya kwanza kutamsaidia mtu kukabiliana inavyofaa na tatizo hilo.