Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuabiri Bahari ya Atlantiki Hadi ya Pasifiki

Kuabiri Bahari ya Atlantiki Hadi ya Pasifiki

Kuabiri Bahari ya Atlantiki Hadi ya Pasifiki

MABAHARIA wa kale walitamani sana kuvumbua njia ya kaskazini ambayo ingeunganisha Bahari ya Atlantiki pamoja na ya Pasifiki, lakini walikabili changamoto kubwa: njia ya bahari ya Aktiki ilikuwa imefungwa na barafu.

Hata hivyo, jambo fulani liliwachochea sana kuvumbua njia hiyo fupi. Kufikia karne ya 16, njia zilizotumika kuelekea kwenye maeneo ya Asia Mashariki kwa ajili ya biashara kupitia kusini ya Afrika na Amerika Kusini, zilikuwa zikidhibitiwa na Wareno na Wahispania. Wafanyabiashara wengine walihitaji kutafuta njia inayopitia kaskazini ikiwa walitaka kufanya biashara na watu wa Asia Mashariki. Watu wengi walijaribu kufanya hivyo, kutia ndani wafuatao.

Waingereza: Mnamo 1553, Sir Hugh Willoughby na Richard Chancellor waliongoza kikundi cha kwanza cha Waingereza. Dhoruba ilipopiga meli zao na kuwafanya watengane, Willoughby alilazimika kutua kwenye pwani isiyo na mimea ya Rasi ya Kola upande wa kaskazini ya mbali ya Urusi hadi majira ya baridi kali yalipokwisha. Kwa kuwa hawakuwa wamejitayarisha vizuri kwa ajili ya hali hizo mbaya, yeye pamoja na wote waliosafiri naye walikufa. Kwa upande ule mwingine, Chancellor alifika kwenye bandari ya Arkhangel’sk. Kutoka hapo alisafiri hadi Moscow baada ya kukaribishwa na Maliki Ivan wa Nne Vasilyevich, Mkatili. Chancellor alishindwa kupata njia ya kwenda Asia, lakini alikuwa amefungua njia ya kufanya biashara kati ya Waingereza na Warusi.

Waholanzi: Mnamo 1594, Willem Barents alisafiri kwanza hadi Novaya Zemlya. Hata hivyo, mnamo 1596, alipokuwa kwenye safari yake ya tatu, meli yake ilinaswa katika barafu na ikaharibika kabisa alipokuwa akizunguka ncha ya kaskazini ya visiwa hivyo vya Urusi. Baada ya kuvumilia majira ya baridi kali sana wakiwa ndani ya nyumba waliyojenga kwa mbao za meli zilizovunjika na wakila nyama ya dububarafu, mabaharia wa Barents walirudi katika mashua mbili ndogo. Barents alikufa katika safari hiyo.

Warusi: Wavumbuzi Warusi walifunga safari za kuichunguza Siberia na eneo la Mashariki ya Mbali ya Urusi. Katika miaka 60 tu, kuanzia 1581 hadi 1641, walisonga kutoka kwenye Milima ya Ural hadi kwenye Bahari ya Pasifiki. Wakati huo, watu wa jamii ya Cossack waliabiri Bahari ya Aktiki kupitia mito ya Siberia. Waliteka eneo la Siberia kwa ajili ya Urusi na wakaanzisha usafiri wa meli kwenye pwani ya kaskazini mashariki ya Siberia. Mnamo 1648, meli za Urusi zilipita kwenye njia iliyokuja kuitwa Mlango-Bahari wa Bering, ulioitwa hivyo kutokana na jina la baharia Mdenishi Vitus Bering.

Safari Nyingine

Kuanzia mwaka wa 1733 hadi 1743, wanaume elfu moja hivi wakiwa chini ya uongozi wa Bering walisafiri katika vikundi saba ili kuchunguza pwani ya Urusi ya Bahari ya Aktiki na ya Pasifiki. Barafu ilinasa meli zao tena na tena na mabaharia wengi walikufa. Hata hivyo, safari hiyo ilisaidia kuchora ramani ya karibu pwani yote ya Aktiki. Habari iliyokusanywa, kutia ndani chati, sauti za sona, na habari kuhusu barafu, ziliwasaidia sana mabaharia wa Bahari ya Aktiki.

Muda wote huo, safari kwenye Bahari ya Aktiki zilifanywa kwa kutumia meli za mbao. Lakini safari ya Bering ilionyesha wazi kwamba hazikufaa kutumiwa kuvuka hiyo Njia ya Bahari ya Kaskazini. * Mnamo 1778, mvumbuzi Mwingereza James Cook alifikia mkataa huohuo alipoelekea upande wa magharibi kupitia Mlango-Bahari wa Bering, na kupata barafu imemfungia njia. Karne nyingine ilipita kabla ya Nils Adolf Erik Nordenskiöld wa Finland kufaulu kupitia njia hiyo akitumia meli inayoendeshwa kwa mvuke.

Ustadi wa Warusi

Baada ya Mapinduzi ya Urusi mnamo 1917, hakuna meli zilizoruhusiwa kupitia kwenye Bahari ya Aktiki ya Urusi isipokuwa meli za Urusi. Kuanzia miaka ya 1930 na kuendelea, Muungano wa Sovieti ulitokeza ile iliyoitwa Njia ya Bahari ya Kaskazini na kujenga bandari zilizotumiwa na viwanda vipya. Kwa sababu hiyo, Urusi ikawa stadi katika kuabiri Bahari ya Aktiki.

Wakati wa Vita Baridi, Njia ya Bahari ya Kaskazini haikutumiwa na meli za kigeni. Hata hivyo, kwa sababu ya mabadiliko ya kisiasa na ya kiuchumi, sasa wenye mamlaka nchini Urusi wanawatia moyo watu wote wapitie kwenye njia hiyo. Mfano ufuatao unaonyesha faida ya kutumia njia hiyo.

Katika kiangazi cha 2009, meli mbili za mizigo za Ujerumani zilipitia kwenye Mlango-Bahari wa Bering na kusafiri kuelekea magharibi kando ya pwani isiyokuwa na barafu ya Asia na Ulaya hadi Uholanzi. Ilikuwa mara ya kwanza kwa meli za kampuni ambayo si ya Urusi kusafiri kutoka upande mmoja wa Njia ya Kaskazini-Mashariki hadi upande ule mwingine. Safari hiyo iliokoa kilomita 5,560 na siku kumi ambazo zingetumika kusafiri kwa meli kupitia njia ile ya kawaida. Kampuni hiyo ilikadiria kwamba kila meli iliokoa euro 300,000 (wakati huo zilikuwa dola 450,000, za Marekani) kwa kutumia njia hiyo fupi ya Bahari ya Aktiki.

Leo, barafu kwenye bahari ya Aktiki inayeyuka upesi sana. Kwa sababu hiyo, kila majira ya kiangazi sehemu kubwa ya barafu inapotea baharini. * Ingawa huenda hilo likawa tisho kwa mazingira, iwapo barafu hiyo itaendelea kuyeyuka, meli zitaacha kutumia maeneo ya kando karibu na pwani ya Urusi na kusafiri moja kwa moja kutoka Bahari ya Atlantiki hadi ya Pasifiki, zikipitia juu kabisa ya dunia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 “Njia ya Bahari ya Kaskazini” ndilo jina la Kirusi la Njia ya Kaskazini-Mashariki.

^ fu. 14 Kwa sababu ya hilo na mambo mengine, urefu wa msimu wa kuabiri umeongezwa mara tatu hivi kuliko ulivyokuwa awali kwa ajili ya meli zinazotoka upande wa mashariki wa Aktiki na kuongezwa zaidi ya mara mbili kwa ajili ya meli zinazotoka upande wa magharibi wa Aktiki.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

NJIA ZILIZOTUMIWA NA

Sir Hugh Willoughby na Richard Chancellor

Willem Barents

Vitus Bering

Nils Adolf Erik Nordenskiöld

Mipaka ya barafu

[Ramani]

BAHARI YA AKTIKI

Ncha ya Kaskazini

Mpaka wa kudumu wa barafu

Mpaka wa kiangazi wa barafu

Mpaka wa majira ya baridi kali wa barafu

MZINGO WA AKTIKI

SWEDEN

GREENLAND

KANADA

ALASKA

Bahari wa Bering

URUSI

SIBERIA

MILIMA YA URAL

Mlango-Novaya Zemlya

Rasi ya Kola

Arkhangel’sk

MOSCOW

[Picha katika ukurasa wa 16]

Barafu ya Bahari ya Aktiki inayeyuka upesi

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Library and Archives Canada/Samuel Gurney Cresswell collection/C-016105