Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wachunguzi nchini Kanada walitaka kuchunguza jinsi ponografia inavyowaathiri wanaume. “Tulianza uchunguzi wetu kwa kuwatafuta wanaume walio na umri wa miaka 20 na kitu ambao hawajawahi kutazama ponografia,” anaeleza mshiriki mmoja wa kikundi hicho, lakini “hatukuweza kupata hata mmoja.”—CHUO KIKUU CHA MONTREAL, KANADA.

Jengo refu zaidi ulimwenguni linaloitwa Burj Khalifa, lilizinduliwa huko Dubai mnamo Januari (Mwezi wa 1). Jengo hilo lina kimo cha mita 828, lina zaidi ya orofa 160, na linaweza kuonekana umbali wa kilomita 95.—GULF NEWS, MUUNGANO WA FALME ZA KIARABU.

“Dini ya Kiyahudi inazidi kujipatanisha na nyakati za kisasa. Hivi majuzi sala mpya kwa ajili ya watu wanaofanyiwa upasuaji wa kubadilishwa jinsia iliongezwa katika sala za dini hiyo.”—THE NEW YORK TIMES MAGAZINE, MAREKANI.

Watoto Ambao Hawawezi Kuwasiliana

Leo wazazi wanatumia muda mfupi zaidi kuzungumza na watoto wao wakati wa milo au kuwasomea wanapoenda kulala kuliko wazazi wa nyakati zilizopita walivyofanya. “Watoto wanaoingia kwenye shule ya msingi wanazungumza kama watoto wenye umri wa miezi 18 tu na idadi ya wale ambao hawawezi hata kuunda sentensi rahisi sana inazidi kuongezeka,” linasema gazeti The Times la London. Nchini Uingereza, “asilimia 18 ya watoto walio na umri wa miaka 5 (zaidi ya 100,000) wanashindwa kuzungumza kama watoto wanavyotazamiwa kufanya wanapokuwa na umri huo.” Kwa sababu hiyo, watoto wengi ambao hawawezi kuelewa maagizo rahisi au kujieleza wanapohitaji kitu “ni kama wageni darasani,” wanashindwa kuelewa kinachoendelea.

Je, Makanisa Nchini Ireland Yatakosa Makasisi?

“Kanisa Katoliki lililokuwa na makasisi wengi linatokomea,” linasema gazeti The Irish Times. Miaka 50 iliyopita, Ireland ilikuwa ndiyo nchi iliyotokeza makasisi wengi zaidi. Lakini sasa, idadi inayoongezeka ya makasisi waliozeeka nchini Ireland inaonyesha kwamba hivi karibuni, makasisi hao watakapotimia miaka 75 na hivyo kustaafu, parokia fulani hazitakuwa na makasisi. Inasemekana kwamba tatizo lilitokana na uamuzi wa kupiga marufuku mbinu zisizo za kiasili za kuzuia uzazi uliochapishwa katika barua ya papa Humanae Vitae ya mwaka wa 1968. Gazeti Times linasema kwamba barua hiyo iliwafanya “watu waanze kushuku mafundisho ya Kanisa,” kisha “ikawafanya waache kuwa na imani katika uongozi wa kanisa.”

Upande wa Kaskazini wa Dira Unasonga

Upande wa kaskazini wa dira ulipotambuliwa mnamo 1831, ulikuwa kaskazini mwa Kanada, “kilomita 2,750 kutoka kwenye Ncha ya Kaskazini,” linasema gazeti la Kifaransa Le Figaro. Kufikia mwaka wa 1989, upande huo wa kaskazini wa dira ulikuwa ukisonga karibu na Ncha ya Kaskazini kwa mwendo wa kilomita 5 hadi 15 kila mwaka. Kulingana na Taasisi ya Paris ya Fizikia ya Ulimwengu, kwa sasa upande wa kaskazini wa dira unasonga “kilomita 55 hivi kila mwaka” na mnamo 2007 ulionekana kuwa kilomita 550 kutoka kwenye Ncha ya Kaskazini. Kupatana na mwendo na mwelekeo wa sasa, kufikia mwaka wa 2020, mianga ya kaskazini, au aurora borealis, “itaonekana wazi zaidi juu ya Siberia kuliko Kanada,” linasema gazeti hilo.