Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Mayday! Mayday! Mayday!” Mwito Ambao Huokoa Uhai

“Mayday! Mayday! Mayday!” Mwito Ambao Huokoa Uhai

“Mayday! Mayday! Mayday!” Mwito Ambao Huokoa Uhai

Meli ya uvuvi ilikumbwa na moto na moshi mwingi! Kila mtu aliyekuwa ndani yake alikuwa katika hatari kubwa. Mlinzi mmoja wa Pwani alisema, “Ikiwa kapteni wa meli hiyo inayoitwa ‘Nautical Legacy’ hangetoa mwito wa ‘Mayday,’ mashua hiyo haingewahi kupatikana.” Walinzi wa Pwani wa Kanada waliitikia upesi na hivyo wakafaulu kuokoa mabaharia wote wa meli hiyo. *

“MAYDAY! Mayday! Mayday!” Maneno hayo yanaposikika kwenye redio yanatangaza hali ya dharura yenye kutishia uhai na ni mwito wa kuomba msaada haraka. Lakini je, mwito huo hujibiwa? Katika mwaka wa 2008, Walinzi wa Pwani wa Marekani waliitikia mwito huo zaidi ya mara 24,000. Waliwaokoa watu 4,910—wastani wa watu 13 kwa siku—na wakasaidia zaidi ya watu 31,000 waliokuwa hatarini.

Lakini kwa nini neno “Mayday” linatumika? Na kabla ya mawasiliano ya redio kuanza kutumiwa, mabaharia waliokuwa waliokabili hatari walitumia njia gani kuomba msaada?

Njia Zilizotumiwa Zamani Kuomba Msaada

Katika mwaka wa 1588, meli ijulikanayo kama Santa Maria de la Rosa ya Manowari za Hispania ililipua mizinga yake kama ishara ya kwamba ilikuwa taabani wakati nahodha wake aliposhindwa kuimudu chini ya dhoruba kali. Meli hiyo ilizama na hakuna aliyeokoka. Katika pindi nyingine, mabaharia walipeperusha bendera zilizotoa ishara kwamba walikuwa hatarini. Hata leo, meli inapopeperusha bendera nyeupe yenye msalaba mwekundu uliokingamana, ni ishara inayojulikana ulimwenguni pote ya kuomba msaada.

Katika miaka ya 1760, mabaharia walianza kujifunza kutumia njia ya kuwasiliana kwa kutumia mfumo wa ishara zinazoonekana unaoitwa semaphore. Mtoaji ishara hushika bendera mbili na kutoa ishara kwa kuiga mikono ya saa. Kila ishara ya “wakati” inawakilisha herufi au nambari fulani.

Hata hivyo, utumizi wa bendera, mizinga, na ishara zilisaidia iwapo tu watu wangeweza kuziona au kuzisikia sauti zilizotolewa kama mwito wa kuomba msaada. Mara nyingi, mabaharia waliokuwa hatarini hawakuwa na matumaini makubwa ya kuokolewa. Hali hiyo ingeboreshwa jinsi gani?

Njia Nzuri Zaidi za Kuomba Msaada

Katika miaka ya 1840 kulikuwa na maendeleo makubwa katika teknolojia ya mawasiliano. Samuel Morse alivumbua njia ya kuwasiliana ambayo watu wangetumia telegrafu kutuma ujumbe kupitia waya iliyounganishwa kwenye kifaa cha kurushia habari. Kifaa hicho kilipobonyezwa, mtu aliye upande ule mwingine angeweza kusikia mlio fulani uliotokezwa na umeme. Morse alihakikisha kwamba kila herufi na nambari inawakilishwa na sauti, nukta, au kistari kifupi au kirefu.

Ili kuwasiliana kwa kutumia mfumo wa alama za siri wa Morse baharini, mabaharia walitumia miale ya nuru badala ya sauti zilizotumwa kwa telegrafu. Ikiwa mtu angeangaza mwale kwa muda mfupi, mwale huo ungewakilisha nukta, na ikiwa angemulika kwa muda mrefu zaidi mwale huo ungewakilisha kistari. Baada ya muda, watu walianza kutuma mwito mfupi wa kuomba msaada kwa kutumia nukta tatu, vistari vitatu, kisha nukta tatu zaidi, kumaanisha herufi SOS. *

Kwa kupendeza, bado watu waliendelea kubuni njia za kuomba msaada. Mnamo 1901, Guglielmo Marconi alituma ujumbe wa kwanza kwa kutumia mawimbi ya redio akiwa kwenye Bahari ya Atlantiki. Sasa ujumbe wa SOS ungetumwa kupitia mawimbi ya redio badala ya miale ya mwanga. Lakini bado, watu hawangeweza kutuma mwito wa kuomba msaada kupitia maneno. Maneno “Mayday! Mayday! Mayday!” hayakuwa yameanza kutumiwa.

Hatimaye maneno yaliyotamkwa yalisikika kupitia mawimbi ya redio katika mwaka wa 1906, wakati Reginald Fessenden, alipopeperusha programu ya mazungumzo na muziki kwenye redio. Mabaharia waliokuwa na vifaa vya redio walisikia programu hiyo ya Fessenden wakiwa umbali wa kilomita 80. Katika mwaka wa 1915, watu wengi zaidi walifurahi kusikia matangazo ya moja kwa moja kutoka Arlington, Virginia, Marekani, hadi Mnara wa Eiffel huko Paris, Ufaransa—zaidi ya kilomita 14,000! Na hebu wazia furaha ambayo mabaharia wa meli inayoitwa S.S. America walipata mnamo 1922 walipozungumza wakiwa baharini umbali wa zaidi ya kilomita 600 kupitia redio na watu katika mji wa Deal Beach, New Jersey, Marekani.

Kuwa na Mwito Mmoja wa Kuomba Msaada

Katika miaka ya 1920 na 1930 watu wengi walianza kutumia redio kuwasiliana. Kwa kuwa mabaharia wanazungumza lugha tofauti, ni mwito gani ambao nahodha wa meli angeweza kutuma ili kuomba msaada ambao kila mtu angeweza kuelewa? Katika mwaka wa 1927, Kongamano la Kimataifa la Telegrafu ya Mawimbi ya Redio lilisuluhisha tatizo hilo kwa kuamua kwamba neno “Mayday” ndilo litakalokuwa mwito wa kimataifa wa kuomba msaada. *

Tunashukuru sana kwamba njia za mawasiliano zimeboreshwa. Kwa mfano, rada na Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Setilaiti (GPS) umeanza kutumiwa badala ya mizinga na ishara za bendera. Pia, redio zimekuwa vifaa vikuu vya mawasiliano, na mashirika ya huduma za uokoaji huchunguza mawimbi ya redio kwa ukawaida. Kama vile kisa cha meli ya Nautical Legacy kinavyoonyesha, hali ya dharura inapotokea wakati au mahali popote pale, mwito “Mayday! Mayday! Mayday!” huenda ukasikika. Tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya zamani, ukipatwa na hatari baharini, badala ya kuwa na matumaini madogo ya kuokolewa, unaweza kuwa na uhakika kwamba utapata msaada.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Iliripotiwa katika kitabu True Stories of Rescue and Survival—Canada’s Unknown Heroes

^ fu. 11 Herufi SOS zilichaguliwa kwa sababu zingetumwa kwa urahisi na kueleweka. Hazikuwa na maana hususa.

^ fu. 15 Neno “Mayday” linapaswa kurudiwa mara tatu ili kukazia kuwa ni mwito wa kuomba msaada na ili mtu asipate maana tofauti.

[Picha katika ukurasa wa 27]

“Nautical Legacy” ikiteketea baharini

[Hisani]

Courtesy Fisheries and Oceans Canada, reproduced with the permission of © Her Majesty the Queen in Right of Canada, 2010 ▸

[Picha katika ukurasa wa 28]

Ili kuwasiliana kwa kutumia mfumo wa alama za siri wa Morse baharini, mabaharia walitumia miale ya nuru badala ya sauti zilizotumwa kwa telegrafu

[Hisani]

© Science and Society/SuperStock