Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Panyabuku wa Milima ya Alps

Panyabuku wa Milima ya Alps

Panyabuku wa Milima ya Alps

Nilisikia mbinja kali sana. Ilikuwa kama ile ya mvulana akimwita rafiki yake, lakini ilikuwa ya sauti ya juu zaidi. Mbinja hiyo ilisikika katika mlima wote hivi kwamba hungeweza kujua ilitokea wapi. Kisha nikamwona mnyama mdogo mwenye manyoya mengi akikimbia kuingia katika shimo. Nilipotazama upesi kitabu kidogo nilichokuwa nacho, kilinihakikishia kwamba nilikuwa nimemwona na kumsikia panyabuku wa Milima ya Alps.

SIKU kadhaa zilizofuata, nilijifunza mambo mengi kuwahusu wanyama hao wadogo wenye manyoya. Nilijifunza wao hupenda kulala juu ya miamba gani wanapoota jua, mahali mashimo yao yalipo, na jinsi wanavyoweza kustahimili maeneo ya juu yenye baridi kali ambayo hayana miti.

Ushirikiano na Ulinzi wa Familia

Maisha ya panyabuku kwenye Milima ya Alps si rahisi. Kuna baridi kali sana na huenda eneo lote likafunikwa kwa theluji kwa miezi kadhaa. Pia, kuna hatari ya kuvamiwa na wanyama wa ardhini na wa angani. Kwa hiyo, panyabuku wanahitaji kushirikiana, kupanga mambo, na kuwa macho ili waendelee kuishi.

Panyabuku huishi pamoja kama familia katika vikundi vinavyotia ndani baba, mama, na watoto wao. Kila familia ina mashimo kadhaa ya chini ya ardhi, shimo moja likiwa ndilo makao ya familia na mengine ni mahali pa kujificha wakati wa hatari. Nyakati nyingine panyabuku huchimba mashimo yao katika mianya iliyo chini ya miamba mikubwa. Makao hayo yanayofanana na ngome hutumika kama minara ya kuwasaidia panyabuku kuona hatari kutoka mbali na pia kama maeneo ya kupumzika na kuota jua.

Panyabuku huhakikisha kwamba usafi unadumishwa. Wao hutumia shimo moja kama choo ili kuhakikisha kwamba shimo wanalotumia kama makao linadumishwa likiwa safi. Mwisho wa shimo kuu, panyabuku huchimba shimo lingine kubwa zaidi na kutandaza nyasi chini. Shimo hilo hutumika wakati panyabuku wa kike anapozaa. Pia familia nzima hulala karibu-karibu katika shimo hilo wakati wa majira marefu ya baridi kali.

Daraka muhimu zaidi katika familia ni lile la ulinzi. Panyabuku aliyekomaa ndiye huwa mlinzi huku wengine wakitafuta chakula karibu. Nyakati nyingine, panyabuku husimama kwa miguu yake ya nyuma ili aone vizuri zaidi ikiwa kuna hatari katika maeneo yanayozunguka. Tai, mbweha, na wanadamu ndio wanaowahatarisha zaidi panyabuku wa Milima ya Alps. Wanapokaribia au ndege yeyote mkubwa anapoonekana, mlinzi hutoa kilio kinachoonyesha kwamba kuna hatari. Kwa kupendeza, kilio kinachoonyesha kwamba tai wanakaribia ni tofauti na vilio vingine, kwa kuwa wao ndio wawindaji wakuu wa panyabuku. Kilio hicho kinaposikika, panyabuku wote hutoweka. Mara moja, huwezi kumwona panyabuku hata mmoja juu ya ardhi!

Kutii kunaweza kuokoa maisha, hasa ya panyabuku wachanga, kwani wao ndio chakula ambacho tai-dhahabu wanapenda zaidi. Ikiwa hatari iko karibu sana, mlinzi huingia katika shimo lililo karibu pamoja na panyabuku wengine. Kisha, baada ya dakika chache anachomoza kichwa chake kuona ikiwa hatari imekwisha.

Maisha Wakati wa Joto na wa Baridi

Katika maeneo ya juu ambako panyabuku hao huishi kuna nyasi nyingi sana za kula, na kuna joto wakati wa kiangazi. Kunapokuwa na baridi ya kadiri, panyabuku hujipasha joto wakiwa juu ya mwamba. Lakini majira ya joto huwaletea matatizo kwa kuwa hawawezi kuvua koti lao lenye manyoya mengi. Kwa sababu hiyo panyabuku ni watendaji zaidi asubuhi na jioni.

Panyabuku wa Milima ya Alps hawana tatizo la kulala; wao hulala kwa miezi sita hivi. Panyabuku mwingine anayeitwa hoary anaweza kulala kwa miezi tisa hivi. Wakati huo wanapolala, moyo wa panyabuku wa Milima ya Alps hupiga mara moja au mbili tu kwa dakika, na joto la mwili wake hushuka kufikia nyuzi 5 Selsiasi. Kwa kweli, anahitaji kujitayarisha vizuri sana ili aweze kukaa muda wote huo bila kula. Wakati wa miezi mingine, panyabuku hula sana ili wapate mafuta mwilini ambayo yatawasaidia wanapolala wakati wa majira marefu ya baridi kali.

Panyabuku wachanga hupenda kucheza na mara nyingi wao hukimbizana huku na huko. Niliwatazama panyabuku watatu wachanga wakibingirika chini kwenye mlima huku wakicheza kana kwamba wanapigana. Panyabuku wa umri wote husalimiana kwa kugusana pua; pia panyabuku wote katika familia huoshana, na wakati wa baridi wao hulala pamoja ili wapate joto.

Panyabuku hujitayarisha kwa ajili ya wakati ujao, nao huwa chonjo nyakati zote. (Ayubu 12:7) Familia za wanadamu zinaweza kujifunza kutokana na wanyama hao wadogo.

[Blabu katika ukurasa wa 11]

Panyabuku hufanya Milima ya Alps ivutie zaidi, na ushirikiano katika familia yao ni uthibitisho wa hekima ya Muumba.—Zaburi 50:10

[Blabu katika ukurasa wa 12]

Panyabuku aliyekomaa ndiye huwa mlinzi huku wengine wakitafuta chakula karibu