Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kati ya tani milioni 95.2 za wanyama wa baharini ambao huvuliwa kila mwaka, milioni 38.5 hivi hawahitajiki. “Iwapo asilimia 40 ya wanyama tunaovua kutoka baharini wanatupwa, basi idadi ya samaki baharini itazidi kupungua,” akasema Karoline Schacht, mtaalamu wa Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni.—BERLINER MORGENPOST, UJERUMANI.
“Huenda ikaonekana ni kama ng’ombe, kondoo na mbuzi wanaathiriwa na tamaa ya binadamu ya kula nyama, lakini . . . mifugo ulimwenguni pote wanapoteuka, wanatoa asilimia 18 ya gesi zinazoongeza joto duniani [hasa methani]—kiasi kikubwa zaidi ya kinachotolewa na vyombo vyote vya kusafiri.”—NEW SCIENTIST, UINGEREZA.
Gundi ya Zamani za Kale
Wanasayansi waliokuwa wakifanya kazi huko KwaZulu-Natal, Afrika Kusini waligundua gundi iliyotumika maelfu ya miaka iliyopita. “Gundi hiyo . . . ni nzuri kama gundi yoyote ile inayopatikana dukani leo,” likaripoti The Star, gazeti la Johannesburg. Inasemekana kwamba wawindaji wa kale walitumia gundi hiyo kuunganisha ncha za mishale au mikuki kwenye mipini yake. Wanasayansi walijitahidi sana kutengeneza gundi kama hiyo ya zamani wakitumia ngegu nyekundu, mafuta ya wanyama, gundi inayopatikana kwenye mgunga, pamoja na mchanga. Walijaribu sana kuikausha kwa kuiweka karibu na moto lakini hawakufanikiwa. Hilo lilifanya wawaheshimu watu walioitengeneza mwanzoni.
Kulala kwa Saa Chache Kunaleta Mafua
Ripoti moja kutoka Chuo Kikuu cha Carnegie Mellon huko Pittsburgh, Pennsylvania, Marekani, ilisema kwamba “kuna uwezekano mara tatu kwa watu ambao hulala kwa muda unaopungua saa saba kila siku kupatwa na mafua kuliko watu ambao hulala saa nane au zaidi.” Pia kuna uwezekano “mara tano na nusu kwa wale ambao kwa asilimia 8 ya muda ambao huwa kitandani” bila kupata usingizi kushikwa na mafua kuliko ilivyo kwa wale ambao huwa na usingizi mtulivu. Sheldon Cohen aliyeongoza utafiti huo alisema hivi: “Ingawa tunajua vyema kwamba usingizi unaweza kuathiri mfumo wa kinga wa binadamu, huu ni uthibitisho wa kwanza unaoonyesha kwamba hata usingizi unapokatishwa kwa kiasi kidogo sana, unaweza kuathiri jinsi mwili hutenda unaposhambuliwa na virusi vya mafua. Hii inaonyesha sababu nyingine muhimu kwa nini watu lazima wapange ratiba zao vizuri ili waweze kupata usingizi wa kutosha kila siku.”
Mashamba Zaidi kwa Ajili ya Kilimo
Gazeti New Scientist lilisema kwamba “kuna nafasi ya kutosha katika dunia inayoweza kutokeza chakula kinachohitajika kwa ajili ya idadi ya watu inayozidi kuongezeka. Na tofauti na matarajio ya wengi, mengi ya mashamba hayo yanapatikana barani Afrika.” Gazeti hilo lilinukuu ripoti ya kilimo iliyochapishwa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. Kulingana na ripoti hiyo, ardhi iliyotengwa sasa hivi ulimwenguni pote kwa ajili ya kilimo, huenda ikaongezeka zaidi ya mara mbili. Ripoti hiyo ilisema kwamba “zaidi ya nusu ya mashamba hayo yanapatikana barani Afrika na Amerika ya Latini.”