Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chungu wa Jangwani Wanaotokeza Asali Tamu

Chungu wa Jangwani Wanaotokeza Asali Tamu

Chungu wa Jangwani Wanaotokeza Asali Tamu

YUMINIYA, rafiki yetu ambaye ni Mwenyeji wa Asili wa Australia, anataka kutuonyesha mahali ambapo yeye hupata chakula kitamu jangwani. Anatupeleka kwenye eneo kavu lenye vichaka kaskazini ya Alice Springs, katikati ya Australia, kisha anakagua kwa uangalifu ardhi yenye mchanga. Chini ya miti ya mulga, ambayo ni aina fulani ya migunga, anaona wadudu wadogo watakaotuongoza kwenye chakula hicho. Wadudu hao ni chungu wanaotokeza asali.

Anachimba mahali hapo kwa bidii na kufuata njia ya chungu inayoelekea chini ya mchanga. Punde anachimba shimo lenye kina cha zaidi ya mita moja na upana unaoweza kumtosha mtu kuketi chini. “Unaweza kuchimba ili kutafuta chungu wa asali wakati wowote, lakini ni afadhali kufanya hivyo wakati wa majira ya baridi kali kwa kuwa kunakuwa na joto jingi wakati wa kiangazi,” anasema akiwa ndani ya shimo hilo. Tunamtazama anapokagua kwa makini njia kadhaa za chungu. “Unahitaji kujua utafuata njia gani,” anaeleza.

Punde si punde, Yuminiya anapata nyumba ya chungu. Ndani yake kuna chungu 20 hivi wenye tumbo zilizovimba, kubwa kama zabibu, zilizojaa umajimaji ulio na rangi ya chungwa. Wadudu hao wadogo huning’inia kutoka kwenye dari la mchanga, wasiweze kusonga kwa sababu ya tumbo zao zilizovimba. Katika muda wa dakika chache, Yuminiya anakusanya chungu zaidi ya mia moja kutoka vyumba mbalimbali. Anasema: “Asali ya chungu hawa ni mojawapo ya chakula kitamu tunachotoa msituni.”

Miili Iliyojaa Asali

Kati ya jamii zaidi ya 10,000 za chungu wanaojulikana, chungu wanaotokeza asali ni wa pekee sana. Tofauti na nyuki ambao huhifadhi asali yao katika masega ya asali, chungu hao huhifadhi nekta ndani ya miili ya chungu wafanyakazi. Chungu wengine hula asali hiyo kunapokuwa na upungufu wa chakula nje.

Ili aweke au kutoa asali, chungu hutumia vipapasio vyake kugusa vipapasio vya chungu anayebeba asali. Chungu huyo hufungua mdomo wake na hivyo asali iliyo tumboni inaweza kufikiwa. Tumbo lake lina valvu ya pekee ambayo hudhibiti jinsi asali inavyoingia na kutoka. Katika muda wa maisha yake ya miezi kadhaa, chungu huyo anaweza kukamuliwa na kujazwa asali mara kadhaa.

Kwa kawaida, chungu wanaobeba asali hawafanyi kazi yoyote chini ya ardhi, ambapo wanalindwa kutokana na ukame, joto, na hatari. Wakiwa chini ya ardhi, wao pia hujilinda dhidi ya bakteria na kuvu kwa kupaka miili yao umajimaji fulani kutoka kwenye tezi ya pekee ambao huua viini.

“Asali” yao hutoka wapi? Kwanza, utomvu na nekta hutoka kwenye miti ya migunga. Kisha umajimaji huo huliwa na wadudu wadogo wanaoitwa aphid. Halafu chungu wafanyakazi wanakamua umajimaji huo mtamu kutoka kwa wadudu hao, au wanakusanya nekta moja kwa moja kutoka kwenye miti. Mwishowe, chungu wafanyakazi huwalisha umajimaji huo chungu wanaobeba asali. Kwa kuwa chungu wanaobeba asali hawafanyi kazi yoyote, wao huhitaji kiasi kidogo sana cha umajimaji huo wenye lishe, kwa hiyo kiasi kinachobaki huhifadhiwa tu ndani ya tumbo lao.

Namna gani wadudu hao wanaoitwa aphid? Je, wao hupata hasara? La, hasha. Kwa kawaida, chungu huwaachia nekta ya kutosha. Pia, chungu huwalinda aphid kutokana na vimelea na hatari. Kwa njia hiyo, chungu na wadudu hao hufaidika kutokana na ushirikiano huo.

Biblia inasema: “Mwendee chungu, . . . zitazame njia zake upate kuwa na hekima. Ijapokuwa hana kiongozi, ofisa wala mtawala, yeye hutayarisha chakula chake wakati wa kiangazi; amekusanya akiba ya chakula chake wakati wa mavuno.” (Methali 6:6-8) Maneno hayo ni kweli kama nini, kwa kuwa chungu hushirikiana kwa ukaribu sana, wana utaratibu wa hali ya juu, na ni wenye bidii! Na inastaajabisha sana kwamba wakazi hao wa jangwani hutokeza asali yenye ladha tamu sana chini ya hali ngumu!

[Picha katika ukurasa wa 11]

Tumbo la chungu aliyebeba asali lililojaa nekta tamu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]

Pages 10, 11, top: M Gillam/photographersdirect.com; page 11: © Wayne Lynch/age fotostock