Kombe la Konokono Anayeitwa Scaly-Foot
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Kombe la Konokono Anayeitwa Scaly-Foot
● Konokono anayeitwa scaly-foot ndiye mnyama mwenye kombe gumu zaidi. Anaishi kwenye sakafu ya Bahari ya Hindi, na anaweza kustahimili shinikizo la maji akiwa mita 2,400 hivi chini ya bahari. Isitoshe, konokono huyo haathiriwi na maji yenye chumvi nyingi au kiwango cha joto kinachobadilika-badilika—ambacho kinatia ndani maji moto yanayotoka kwenye chemchemi za maji moto. Pia kombe lake linamlinda anaposhambuliwa.
Fikiria hili: Kombe la konokono huyo lina matabaka matatu. Tabaka la kwanza limefanyizwa kwa chuma iliyo na salfaidi; la pili linafanana na protini ambayo kwa kawaida inapatikana juu ya makombe ya konokono wengine; na la tatu limefanyizwa kwa madini fulani ya kalisi inayoitwa aragonite. Matabaka hayo matatu humfanya konokono huyo asishambuliwe na kaa ambao hujaribu kuvunja kombe lake kwa kutumia miguu yao yenye nguvu. Nyakati nyingine, kaa anaweza kumbana konokono huyo kwa siku kadhaa, lakini kombe lake halivunjiki.
Wakitumia kifaa fulani kilicho na ncha ya almasi, watafiti waligundua kwamba “sehemu ya nje ya kombe imeundwa kwa njia ambayo inafanyiza nyufa zinazofyonza nishati,” linaripoti gazeti Discover. “Nyufa hizo huenea kwa kuzunguka chembe za chuma iliyo na salfaidi. Nyufa hizo ndogo zinazofanyizwa hufyonza nishati na pia zinahakikisha kwamba nyufa kubwa zaidi hazijitokezi.” Wakati huohuo, tabaka la katikati hufyonza nishati inayotokezwa anaposhambuliwa.
Watafiti wanatumaini kwamba wataweza kuiga muundo wa kombe la konokono huyo anayeitwa scaly-foot ili kutokeza kofia ngumu zaidi za kulinda kichwa na fulana zisizopenya risasi, na vilevile kutokeza viunzi vya meli na ndege. “Mabomba ya mafuta ya Aktiki ambayo mara nyingi yanagongwa na miamba ya barafu yanaweza kufaidika,” linasema gazeti Discover.
Una maoni gani? Je, kombe la konokono anayeitwa scaly-foot lilijitokeza lenyewe? Au lilibuniwa?
[Mchoro katika ukurasa wa 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kifaa chenye ncha ya almasi
Tabaka la nje
Tabaka la katikati
Tabaka la ndani
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Courtesy Anders Warén