Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi ya Kuzuia Aksidenti za Barabarani

Jinsi ya Kuzuia Aksidenti za Barabarani

Jinsi ya Kuzuia Aksidenti za Barabarani

MAGURUDUMU yanapiga kelele, vyuma vinakwaruzana, vioo vinavunjika, watu wanapiga mayowe . . . Huenda mtu yeyote ambaye amewahi kuhusika katika aksidenti ya barabarani akafahamu vizuri sauti hizo. Shirika fulani nchini Marekani (The Population Reference Bureau) linaripoti kwamba ulimwenguni pote “watu milioni 1.2 hivi hufa katika aksidenti za barabarani kila mwaka, na wengine milioni 50 hujeruhiwa.”

Hata hivyo, kukazia fikira usalama na kutumia akili kunaweza kumsaidia mtu aepuke aksidenti nyingi. Jinsi gani?

Viwango vya Mwendo, Mikanda ya Usalama, na Simu

Huenda katika barabara fulani viwango vya mwendo vilivyowekwa kisheria vikaonekana kuwa vya chini sana. Lakini mara nyingi kupitisha kiwango kilichowekwa hakutokezi badiliko kubwa sana kuhusu wakati utakaochukua kufika uendako. Kwa mfano, ikiwa unasafiri umbali wa kilomita 80, kuongeza mwendo kutoka kilomita 100 kwa saa hadi kilomita 120 kwa saa, kutakupunguzia dakika nane hivi. Je, kuna faida yoyote kuhatarisha uhai wako ili uokoe muda mfupi hivyo?

Mikanda ya usalama imeundwa ili iokoe uhai. Shirika moja la serikali nchini Marekani lilisema kwamba mikanda ya usalama iliokoa uhai wa watu zaidi ya 72,000 kati ya mwaka wa 2005 na 2009 nchini humo pekee. Je, mifuko ya usalama yenye hewa ni bora kuliko mikanda ya usalama? Hapana. Mifuko ya hewa husaidia zaidi inapotumiwa pamoja na mikanda ya usalama. Usipojifunga mkanda wa usalama, mfuko wa hewa peke yake hauwezi kukusaidia na hata unaweza kukuumiza. Kwa hiyo, uwe na mazoea ya kujifunga mkanda wa usalama, na uwaombe wale unaosafiri nao wafanye vivyo hivyo. Tahadhari nyingine: Usithubutu kusoma au kuandika ujumbe mfupi unapoendesha gari.

Hali ya Barabara na Udumishaji wa Gari

Barabara zenye maji, mchanga au kokoto, hufanya iwe vigumu kwa magurudumu kushika barabara vizuri. Unapopunguza mwendo, itakuwa rahisi kufunga breki bila kuteleza. Ikiwa wewe huendesha gari kwa ukawaida kwenye barabara zilizofunikwa kwa theluji au barafu, unaweza kununua magurudumu ya pekee yanayotumiwa kwenye theluji. Magurudumu hayo huwa na tredi kubwa zaidi ambazo huyasaidia kushika barabara vizuri zaidi.

Makutano ya barabara ni hatari kwa madereva wote. Mtaalamu mmoja anapendekeza mambo yafuatayo: Wakati taa ya barabarani ya kijani inapowaka, subiri kwanza kabla ya kuingia barabarani. Unaposubiri kidogo, unaweza kuepuka kugongwa na gari ambalo halikusimama taa nyekundu ilipowaka.

Ili uepuke aksidenti, ni muhimu kudumisha gari lako likiwa katika hali nzuri. Hebu wazia ikiwa gari lako lingekosa kufunga breki unapoliendesha. Ili kuepuka hitilafu, watu fulani hupanga kwamba mara kwa mara magari yao yafanyiwe udumishaji na mekanika aliye na uzoefu. Kwa upande mwingine, watu fulani hujifanyia kazi fulani za udumishaji. Njia yoyote ile utakayotumia, hakikisha kuwa gari lako linakaguliwa na kurekebishwa inavyofaa.

Kunywa Kileo na Kuendesha Gari

Hata madereva ambao kwa kawaida ni waangalifu sana, wanaweza kuhatarisha uhai wao wanapoendesha gari baada ya kunywa kileo. Katika mwaka wa 2008, nchini Marekani, zaidi ya watu 37,000 walipoteza uhai wao katika aksidenti za barabarani. Asilimia 33 hivi ya idadi hiyo walikufa kwa sababu ya madereva ambao waliendesha magari baada ya kunywa kileo. Hata kiasi kidogo sana cha kileo kinaweza kuathiri uwezo wako wa kuendesha gari. Wengine huamua kutokunywa kileo hata kidogo ikiwa wataendesha gari.

Kutii sheria za barabarani, kujifunga mikanda ya usalama, kudumisha gari lako likiwa katika hali nzuri, na kuepuka kuendesha gari baada ya kunywa kileo kunaweza kulinda uhai wako na wa wengine pia. Madokezo haya yanaweza kukusaidia uepuke aksidenti unapoendesha gari iwapo tu utayatumia.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 11]

USIENDESHE GARI UKIWA NA USINGIZI

“Lazima ukumbuke kwamba kuendesha gari ukiwa na usingizi ni sawa tu na kuendesha gari ukiwa umelewa.” Maneno hayo yaliyosemwa na ofisa mmoja wa Shirika la Kitaifa Kuhusu Usingizi la Marekani, yanaonyesha hatari za kuendesha gari ukiwa na usingizi. Ishara zifuatazo zinaonyesha kwamba ni hatari kwako kuendesha gari: *

Ni vigumu kwako kuwa chonjo, na una macho mazito

Ni vigumu kuweka kichwa chako kikiwa wima

Unapiga miayo mfululizo

Ni vigumu kukumbuka kilomita chache zilizopita ukiendesha gari

Unakosa kutambua barabara unayopaswa kuingilia au ishara za barabarani

Unayumbisha-yumbisha gari, unakaribia sana gari lililo mbele yako, au unapandisha gari kando ya barabara sehemu ambayo hupaswi kukanyaga

Ukiona dalili hizo, mruhusu dereva mwingine aendeshe gari au simamisha gari mahali salama na ulale kidogo. Afadhali kuchelewa kuliko kuhatarisha uhai wako na ule wa watu wengine!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 16 Orodha hii imetolewa na Shirika la Kitaifa Kuhusu Usingizi.