Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Unamna-Namna wa Viumbe Katika Msitu wa Amazoni (Aprili 2010) Habari hiyo ilisema kwamba watu wa kabila la Awajun (Aguaruna) huabudu miungu mitano tofauti. Mimi ni mwenyeji wa kabila la Awajun na sikubaliani nanyi. Nafikiri mlikosea, kwa sababu wengi kati ya watu wa kabila la Awajun ni Wakristo na hatuabudu miungu mitano kama gazeti lenu lilivyosema. Kwa kuwa watu wa kabila la Awajun husoma gazeti lenu kwa ukawaida, tafadhali rekebisheni kosa hilo.

T.P.T., Peru

“Amkeni!” lajibu: Mwandishi wetu alikusanya habari kutoka vyanzo mbalimbali kutia ndani mahoji pamoja na watu walioishi katika vijiji vya Aguaruna hapo zamani na vyanzo vingine vilivyochapishwa. Chanzo kimoja kati ya hivyo ni Atlas Regional del Perú, Chapa ya 2004, ambayo ina majina na maelezo ya miungu hiyo mitano ya Aguaruna. Hata hivyo, kama ulivyoandika, wakazi fulani wa jamii ya Aguaruna wameacha imani hizo na kuwa Wakristo. Tunaomba msamaha ikiwa habari hiyo ilieleweka vibaya.

Jinsi ya Kukabiliana na Kigugumizi (Mei 2010) Asanteni kwa habari hiyo. Mimi pia nina kigugumizi, na mara nyingi tatizo hilo hunifanya nijihisi mpweke. Lakini baada ya kusoma habari hiyo, nilitambua kwamba siko peke yangu. Sasa nimeazimia kukabiliana na tatizo hilo, na kama Rafael, ‘neno fulani likinifanya nishikwe na kigugumizi, mimi hucheka.’

Y. S., Japani

Vijana Huuliza . . . Nifanye Nini ili Nijiamini Zaidi? (Mei 2010) Nina umri wa miaka 12 na ninaishi na mama yangu, ambaye ni mgonjwa sana na hana mwenzi. Niliposoma swali, “Je, unahisi kuwa unapendwa?” nilijibu kwa unyoofu, “Hapana.” Jambo hilo lilinifadhaisha sana. Kwa hiyo, nilizungumza na Wakristo fulani wakomavu na pia mama yangu. Habari hiyo ilinisaidia kuelewa kwamba sipaswi kujihukumu vikali sana. Watu wengi wananipenda. Asanteni kwa kunisaidia kuona jinsi ambavyo Yehova anatujali sisi vijana.

C. H., Ufaransa

Habari hiyo ilinisaidia niweze kukabiliana na mambo fulani yaliyonipata zamani na hisia za kwamba sifai ambazo bado zinanisumbua. Sitasahau kamwe njia tatu zilizotajwa katika habari hiyo za kunisaidia nijiamini zaidi na hasa ule mfano kuhusu noti iliyoraruka kidogo! Asanteni kwa habari hiyo nzuri!

S. W., Korea Kusini