Programu kwa Ajili ya Wagonjwa Mahututi—Lengo Ni Nini?
Programu kwa Ajili ya Wagonjwa Mahututi—Lengo Ni Nini?
“Mama yangu mwenye umri wa miaka 94, aliyekuwa na ugonjwa wa “Alzheimer” na tatizo la moyo, hangeweza kutoka kitandani. Hangeweza kula wala kuamka. Hospitalini nilielezwa kwamba alikuwa amepoteza fahamu kabisa. Nilitaka kumtunzia nyumbani lakini nilihitaji msaada.”—Jeanne.
MGONJWA MAHUTUTI hukabili hali ngumu sana na ndivyo pia na watu wa familia yake. Watu wa ukoo hukabili uamuzi mgumu. Je, uhai wa mgonjwa uendelezwe kwa njia yoyote ile, hata wakati ambapo anaendelea kuugua sana bila sababu? Au je, wamsaidie tu awe na starehe kwa kiasi kinachowezekana kisha afe baada ya muda fulani kutokana na ugonjwa wake?
Watu wengi huchagua kumsaidia mgonjwa astarehe akisubiri kifo. Utunzaji huo unahusisha kushughulikia mahitaji ya kihisia, kiroho, na ya kijamii ya mgonjwa mahututi. Kusudi ni kumfanya mtu aliye mgonjwa mahututi asiteseke sana. Karibu nusu ya nchi ulimwenguni pote zinatoa huduma hizo. Kwa mfano, kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu walio na ugonjwa wa UKIMWI na kansa barani Afrika, nchi nyingi za Afrika zimeamua kutoa utunzaji wa aina hiyo au zinajiandaa kutoa huduma hizo.
Lengo la Programu Hizo
Wagonjwa fulani huhisi kwamba kukubali kumwingiza katika programu kama hiyo ni sawa na kuamua kwamba hawataki kuendelea kuishi. Watu fulani wa familia wanaweza kuhisi kwamba kumwingiza mpendwa wao katika programu ya aina hiyo ni sawa na kumsubiri afe bila kumwonyesha hisia zozote. Hata hivyo, kukubali utunzaji huo si sawa na kuamua kwamba mtu hataki kuendelea kuishi. Badala yake, unaweza kumsaidia mgonjwa afurahie maisha yenye kusudi akiwa pamoja na wapendwa wake kwa muda mrefu kadiri awezavyo, huku akidhibiti maumivu. Pia, unaweza kuwapa watu wa familia ya mgonjwa nafasi ya kumfariji na kumtegemeza mpendwa wao kwa muda mrefu kadiri wanavyoweza.
Ingawa utunzaji huo hauwezi kumponya mgonjwa mahututi, unaweza kusaidia kushughulikia matatizo fulani yanayotokea kama vile ugonjwa wa pumu au maambukizo kwenye kibofu. Iwapo hali zitabadilika—kwa mfano, iwapo tiba itapatikana au ikiwa dalili za ugonjwa zitapotea kwa muda—mgonjwa anaweza kurudia matibabu ya kawaida.
Faida za Kutunziwa Nyumbani
Katika nchi fulani, huduma za utunzaji wa wagonjwa mahututi hutolewa tu katika vituo vya afya. Hata hivyo, katika maeneo fulani, watu wa familia wanaweza kuwatunza wagonjwa wao nyumbani. Mgonjwa anapotunziwa nyumbani anaweza kushiriki katika mambo ya familia.
Utunzaji huo wa nyumbani unapatana na mahitaji ya kitamaduni ya nchi nyingi, kama vile, Uganda, ambako kidesturi watu wa familia wanapaswa kuwatunza wagonjwa na wazee.Chini ya mpango huo wa kuwatunzia wagonjwa mahututi nyumbani, mara nyingi watu wanaowatunza hupewa msaada, labda kutoka kwa daktari, wauguzi, na wafanyakazi wengine wa kitiba. Wataalamu hao wanaweza kuwaelemisha watunzaji kuhusu njia wanazoweza kutumia ili kuwasaidia wagonjwa wastarehe na kuwaeleza mambo wanayoweza kutazamia mgonjwa anapokufa. Pia wao hutoa msaada huo kupatana na mapendezi ya mgonjwa na familia yake. Kwa mfano, iwapo familia haitaki, wafanyakazi hao wataepuka kufanya uchunguzi fulani usiohitajika au hawatamlisha mgonjwa kupitia mirija iwapo mgonjwa hawezi kumeng’enya chakula.
Dolores na Jean humtunza nyumbani baba yao mwenye umri wa miaka 96. Kwa sababu ya hali yake inayozidi kuzorota, wao huthamini sana msaada wanaopata. “Mfanyakazi fulani huja siku tano kwa juma kutusaidia kumwosha Baba,” anasema Dolores. “Mfanyakazi huyo hubadili matandiko ya kitanda cha Baba na iwapo tunataka anamnyoa nywele, anakata kucha, na kumsaidia awe nadhifu kwa njia nyingine kama hizo. Mwuguzi huja mara moja kila juma ila kumchunguza Baba na kumletea dawa zake anazotumia kila siku. Na daktari huja baada ya majuma matatu. Tunapowahitaji tunaweza kuwaita wakati wowote, kwa kuwa wanapatikana saa 24 kwa siku.”
Kuweza kuwapata wataalamu wakati wowote ni sehemu muhimu sana ya utunzaji wa wagonjwa mahututi kwa kuwa wanaweza kuamua dawa za kutumia na kuhakikisha kwamba mgonjwa hana maumivu na wakati huohuo yuko chonjo vya kutosha. Wanaweza kumpa mgonjwa oksijeni ili kumsaidia kupumua. Wataalamu hao wanaposaidia kwa njia hiyo, watunzaji pamoja na mgonjwa wanakuwa na uhakika, na hivyo wanaacha kuwa na woga kwamba mgonjwa atapatwa na maumivu makali au dalili nyingine zenye kuhuzunisha anapokaribia kufa.
Utunzaji Wenye Huruma
Watu wanaowatunza wagonjwa mahututi wanatambua uhitaji wa kuhakikisha kwamba wagonjwa wanatendewa kwa heshima wakati wote.
Martha, aliyefanya kazi ya kuwatunza wagonjwa mahututi kwa zaidi ya miaka 20, anasema hivi: “Niliwajua wagonjwa, mapendezi yao na mambo wasiyopenda, na nilijaribu kuwasaidia kwa kiasi nilichoweza wafurahie wakati wao uliobaki kwa kadiri waliyoweza. Mara nyingi nilijihisi nikiwa nina uhusiano wa karibu nao, na wengine wao niliwapenda sana. Ni kweli kwamba wagonjwa fulani waliokuwa na ugonjwa wa Alzheimer au tatizo lingine la kusahau mambo wangekuwa wagumu nilipokuwa nikiwatunza. Wangejaribu kunipiga, kuniuma, au hata kunipiga teke. Lakini kila wakati nilijaribu kukumbuka kwamba si mtu mwenyewe aliyetaka kufanya mambo hayo bali ni ugonjwa uliomfanya atende hivyo.”Martha anasema hivi kuhusu uradhi aliopata kwa kuwategemeza watunzaji wa wagonjwa: “Msaada wangu uliwasaidia wasichoke kuwatunza wapendwa wao. Kujua tu kwamba wataalamu walikuwa wakisaidiana nao kuliwafariji sana.”
Iwapo utunzaji wa aina hiyo unapatikana karibu na mahali unapoishi unaweza kufaa zaidi kuliko hospitali au makao ya kuwatunzia wazee. Jeanne, aliyenukuliwa mwanzoni, anafurahi kwamba aliamua kumtunza mama yake kwa njia hiyo. Anasema: “Mama aliendelea kuishi nyumbani akiwa amezungukwa na watu wa familia ambao walimtegemeza kimwili, kihisia, na kiroho, na wakati huohuo, alipewa utunzaji na dawa alizohitaji ili astarehe. Wataalamu waliotusaidia kumtunza walifanya hivyo kwa ustadi na huruma. Tulithamini sana mashauri na ujuzi wao. Nina uhakika kwamba Mama hangetaka kutunzwa kwa njia nyingine isipokuwa hiyo.”
[Blabu katika ukurasa wa 17]
Kuweza kuwapata wataalamu wakati wowote ni sehemu muhimu sana ya utunzaji wa wagonjwa mahututi
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]
“Tuliweza Kuwa Pamoja Naye”
Isabel, mwanamke huko Mexico ambaye mama yake alikabiliana na kansa ya matiti kwa miaka 16 hadi ilipoenea sana na haikuweza kutibiwa, anaeleza hivi: “Mimi na familia yangu tulikuwa na wasiwasi mwingi kwamba Mama angeteseka. Tulisali kwamba asipatwe na maumivu makali ambayo huwapata wagonjwa wengi wa kansa kabla ya kufa. Daktari fulani nchini Mexico anayeshughulikia hasa kupunguza maumivu alijibu sala zetu. Alitutembelea mara moja kwa juma, akatupa dawa zinazofaa za kukabiliana na maumivu, na akatupa maagizo hususa lakini rahisi ya jinsi ya kuzitumia na kumtunza Mama. Tulifarijika kujua kwamba tungeweza kumpigia simu daktari huyo wakati wowote, usiku au mchana, naye angekuja. Tulifurahi kama nini kumwona mama yetu akiwa bila maumivu na akiwa mtulivu siku zake za mwisho, hata akifurahia chakula kidogo alichoweza kula. Tulikuwa pamoja naye, papahapa nyumbani, hadi alipokufa katika usingizi.”
[Sanduku katika ukurasa wa 17]
Mgonjwa Anapokaribia Kufa
Hakikisheni kwamba shuka ni safi, kavu, na hazijakunjamana. Ili mgonjwa asipate vidonda, mgeuze mara kwa mara na ubadili nguo zake za ndani au nepi za watu wazima iwapo hawezi kuzuia choo chake. Iwapo inahitajika anaweza kusaidiwa kwenda choo kwa kutumia mirija au dawa fulani inayoingizwa kwenye sehemu za nyuma. Iwapo mgonjwa anakaribia kufa, kukosa kula au kutokunywa maji hakuwezi kumfanya ateseke. Zuia midomo yake isikauke kwa kutia vipande vya barafu au pamba iliyotiwa maji na mafuta ya midomo. Kumshika mgonjwa mkono kunafariji na kumbuka kwamba anaweza kusikia hadi atakapokufa.