Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ibn Battuta Anafunua Ulimwengu wa Wakati Wake

Ibn Battuta Anafunua Ulimwengu wa Wakati Wake

Ibn Battuta Anafunua Ulimwengu wa Wakati Wake

KATIKA mwaka wa 1325, kijana mmoja alisafiri kutoka Tangier, nchini Morocco, katika safari ya kwanza kati ya nyingi ambazo zingemfikisha kwenye sehemu za mbali za ulimwengu uliojulikana wakati huo, kutia ndani, China, India, Indonesia, Mali, Siria, Tanzania, Uajemi, Urusi, Uturuki, na nchi zote za Waarabu. Mtu huyo aliitwa Abu Abdallah ibn Battuta, na alisafiri umbali wa kilomita 120,700 hivi—umbali ambao hakuna mtu aliyewahi kufikia kabla ya kuvumbuliwa kwa injini inayoendeshwa kwa mvuke.

Imesemekana kwamba Ibn Battuta ndiye Mwislamu aliyesafiri zaidi katika enzi hizo za kale. Maandishi yake, aliyoyaandika aliporudi nyumbani baada ya kusafiri kwa miaka 30, yanatusaidia kujifunza mambo mbalimbali kuhusu maisha na utamaduni katika karne ya 14, hasa katika ulimwengu wa Waislamu wa Enzi za Kati.

Kwenda Hija Kule Mecca

Ibn Battuta aliondoka kule Tangier akatembelee maeneo matakatifu na ili akahiji kule Mecca, jambo ambalo ni takwa kwa kila Mwislamu mtu mzima ambaye ana uwezo wa kifedha na afya ya kumwezesha kusafiri. Mecca iko umbali wa kilomita 4,800 hivi mashariki ya Tangier. Kama tu wahiji wengi walivyofanya, Ibn Battuta alisafiri pamoja na msafara ili awe salama na aweze kufika alikokuwa akienda.

Kwa kuwa baba yake alikuwa kadhi, au hakimu, Ibn Battuta alipata mafunzo ya ukadhi, elimu bora zaidi ambayo angeweza kupata huko Tangier. Wasafiri wenzake walipogundua hilo, walimweka awe mwamuzi juu yao ili atatue migogoro yoyote ambayo ingetukia wakiwa safarini.

Kuelekea Aleksandria, Cairo, na Sehemu ya Juu ya Mto Nile

Msafara wao ulipita kwenye pwani ya Afrika Kaskazini hadi Misri. Huko, Ibn Battuta aliona mnara maarufu wa taa wa Aleksandria—moja kati ya maajabu ya ulimwengu wa kale—ambao wakati huo sehemu yake ilikuwa imeanza kuwa magofu. Alifafanua Cairo kuwa jiji lenye “majengo mengi sana, umaridadi na fahari isiyo na kifani, mahali pa kukutania pa anayekuja na anayekwenda, mahali pa kupumzikia pa mnyonge na shujaa, umati ambao husonga kama mawimbi ya bahari.” Alivutiwa sana na mashua, bustani, mitaa yenye maduka mengi, majengo ya ibada, na utamaduni wa jiji hilo kuu. Kama ilivyokuwa desturi yake, alipokuwa Misri alitafuta na akapata utegemezo kutoka kwa viongozi wa kidini, wasomi, na watu wengine mashuhuri.

Kutoka Cairo alielekea upande wa juu wa Mto Nile hadi kusini mwa Misri, na njiani alikaribishwa kwenye nyumba za watu wa kidini, makao ya watawa, na madrasa yaliyotegemezwa kwa michango ya wafadhili—jambo lililokuwa la kawaida katika majiji ya Kiislamu. Kusudi lake lilikuwa kuvuka jangwa hadi kwenye Bahari Nyekundu, avuke kwa mashua hadi mashariki mwa Arabia, kisha asafiri hadi Medina, eneo ambamo msikiti wa nabii Muhammad ulikuwa, halafu aelekee Mecca. Lakini vita vilimzuia, kwa hiyo akarudi Cairo.

Anatumia Njia Ndefu

Akiwa bado ameazimia kufika Medina na Mecca, Ibn Battuta alielekea kaskazini hadi Gaza, kisha akaelekea Hebroni, halafu akaenda mahali ambapo inafikiriwa Abrahamu, Isaka, na Yakobo walizikwa. Alipokuwa akielekea Yerusalemu na kwenye Kuba la Mwamba, alitua huko Bethlehemu, ambako aliona jinsi watu waliodai kuwa Wakristo walivyofanya matendo mbalimbali ya ibada mahali ambapo Yesu alizaliwa.

Kisha Ibn Battuta akaelekea kaskazini hadi Damasko, ambako alijifunza pamoja na wasomi Waislamu na akapata shahada zilizomwidhinisha kuwa mwalimu. Alisema kwamba Msikiti wa Umayyad wa jiji hilo ndio uliokuwa “mkubwa zaidi” ulimwenguni. Maduka ya eneo hilo yaliuza vito, vitambaa, vifaa vya kuandika, vitabu, na vitu vya glasi, na maduka ya mawakili yalikuwa na “mashahidi watano au sita na mtu mmoja aliyeidhinishwa na kadhi kushughulikia sherehe za arusi.” Akiwa huko Damasko, Ibn Battuta alifunga ndoa. Hata hivyo, mke wake alikuwa mmoja kati ya wake zake wengi na masuria ambao wanatajwa kwa ufupi tu katika hadithi yake.

Huko Damasko, Ibn Battuta aliungana na wahiji wengine waliokuwa wakielekea Mecca. Njiani, kikundi chake kilipiga kambi kwenye chemchemi ambako watu waliobeba maji walitumia ngozi za nyati kutengeneza matangi makubwa. Wasafiri walitumia matangi hayo kunywesha ngamia wao na kujaza viriba vyao kabla ya kuvuka jangwa hilo. Mwishowe alifika Mecca. Hiyo ndiyo iliyokuwa mara yake ya kwanza kati ya saba kwenda huko kuhiji. Wahiji wengi walirudi nyumbani baada ya kumaliza kuhiji. Lakini Ibn Battuta hakurudi. Alielekea Baghdad “ili tu akatalii,” anasema mwandishi mmoja.

Anaanza Kusafiri Sana

Huko Baghdad, ambao wakati huo ulikuwa ndio mji mkuu wa Uislamu, Ibn Battuta alivutiwa sana na mabafu ya umma. “Kila jengo huwa na mabafu kadhaa ya kibinafsi,” akasema, “kila moja ikiwa na beseni kwenye kona lenye mabomba mawili ya maji moto na baridi.” Kupitia jenerali fulani mwenye urafiki, kijana huyo aliweza kukutana na sultani, Abu Sa’id. Ibn Battuta aliondoka kwenye mkutano huo akiwa na zawadi za pekee—farasi, kanzu ya sherehe, na barua ya kumtambulisha iliyomwomba gavana wa Baghdad ampe ngamia na maandalizi ya safari.

Kisha Ibn Battuta alisafiri kuelekea kwenye bandari za Afrika Mashariki za Mogadishu, Mombasa, na Zanzibar kabla ya kuelekea Arabia na kisha kwenye Ghuba ya Uajemi. Baadaye alieleza kuhusu watu, desturi, na bidhaa alizoona akiwa njiani, yaani, ukarimu aliopokea kutoka kwa wafanyabiashara huko Somalia, utafunaji wa mbegu za tambuu na ukuzaji wa nazi huko Yemen, na upigaji-mbizi ili kutafuta lulu katika Ghuba ya Uajemi. Kisha akatumia njia ndefu kwenda India—akisafiri kupitia Misri, Siria, na Anatolia (Uturuki); akavuka Bahari Nyeusi; akazunguka upande wa kaskazini kwenye Bahari ya Kaspiani; kisha akaelekea chini kupitia Kazakhstan, Uzibekistani, Afghanistan, na Pakistan.

Kutoka India Hadi China

Huko India, Ibn Battuta alifanya kazi akiwa kadhi wa sultani wa Delhi kwa miaka minane. Kwa kuwa alijua kwamba Ibn Battuta anapenda kusafiri, sultani huyo alimtuma akiwa balozi kwa maliki wa China, Togon-temür, aliyekuwa Mmongolia. Alipofika, alipaswa kutoa zawadi iliyotia ndani “farasi 100 ambao chembe zao za urithi hazijachanganywa, watumwa 100 weupe, wasichana 100 Wahindu wa kucheza dansi na kuimba, vitambaa 1,200 vya aina mbalimbali, vinara vya taa na mabeseni ya dhahabu na shaba, majoho ya hariri, kofia, mapodo, mapanga, glavu zilizopambwa kwa lulu, na matowashi kumi na watano.”

Katika bandari ya Calicut iliyo kusini mwa India, Ibn Battuta aliona meli kubwa za wafanyabiashara zilizoitwa junks ambazo zilikuwa zikielekea China. Meli hizo zilikuwa na matanga 12, yote yalikuwa yamefumwa kwa mianzi, na zilikuwa na wafanyakazi 1,000 hivi—mabaharia 600 na wanaume 400 wa vita. Familia za mabaharia hao ziliishi kwenye meli hizo na “walikuza mboga na tangawizi katika matangi ya mbao,” akasema Ibn Battuta.

Ibn Battuta hakuweza kutimiza mgawo wake wa kwenda China akiwa balozi kwa sababu meli hiyo ilivunjika. Badala yake, alifanya kazi na mtawala Mwislamu huko Maldives na akawa wa kwanza kuwaeleza watu wote ulimwenguni kuhusu desturi za eneo hilo. Mwishowe, alifaulu kufika China. Hata hivyo, ingawa alivutiwa na vitu vingi, aliona mambo ambayo kulingana na imani yake yalikuwa yenye kuchukiza. Mambo machache aliyoandika kuhusu China yanawafanya watu fulani watilie shaka ikiwa alitembelea maeneo mengi ya nchi hiyo kama anavyodai. Huenda alifika tu katika bandari zilizo kusini mwa China.

Misiba Anaporudi Nyumbani

Ibn Battuta aliporudi Damasko baada ya miaka 20, alipata kwamba mwana wake alikuwa amekufa miaka 8 baada ya yeye kuondoka na baba yake aliyeishi Tangier alikuwa amekufa miaka 3 kabla ya kifo cha mwanaye. Ulikuwa ni mwaka wa 1348, na ile Tauni ya Karne ya 14 (Black Death) ilikuwa ikienea katika Mashariki ya Kati. Kwa kweli, Ibn Battuta aliripoti kwamba huko Cairo watu 21,000 walikuwa wakifa kila siku!

Mwaka mmoja baadaye, msafiri huyo mwenye umri wa miaka 45 aliwasili Morocco, lakini akapata kwamba mama yake alikuwa amekufa miezi kadhaa mapema kutokana na ugonjwa huo. Alipoondoka alikuwa na umri wa miaka 21. Je, kusafiri kwa miaka 24 kulikuwa kumetosheleza hamu yake? La, kwa sababu baada ya muda mfupi aliondoka na kuelekea Hispania. Miaka mitatu baadaye, alifunga safari yake ya mwisho, iliyomfikisha Mto Niger na Tombouctou (Timbuktu), jiji katika nchi ya Afrika ambayo sasa inajulikana kama Mali.

Anaagizwa Aandike Kumbukumbu Zake

Baada ya kugundua kuhusu safari za Ibn Battuta, sultani wa Fez, huko Morocco alimwagiza aandike simulizi kwa ajili ya makao ya sultani na akampa mwandishi, Ibn Juzayy. Maandishi hayo hayakuenezwa sana katika Kiarabu, na kazi ya kuyatafsiri katika lugha za nchi za Magharibi haikufanywa hadi wasomi kutoka Ulaya walipoyagundua katika karne ya 19.

Ibn Juzayy anafafanua simulizi hilo kuwa ufupisho wa maneno ya msafiri huyo, lakini inaonekana kwamba mwandishi huyo alibadili kimakusudi sehemu fulani za simulizi hilo. Hata hivyo, maandishi hayo yanatusaidia kuona mambo kuhusiana na maisha, biashara, desturi, dini, na siasa za nchi ambazo Ibn Battuta alitembelea hasa zile zilizokuwa katika ulimwengu wa Waislamu wa Enzi za Kati.

[Picha katika ukurasa wa 14]

Picha ya karne ya 13 iliyochorwa na al-Wasiti, ikionyesha wahiji Waislamu wa Enzi za Kati

[Hisani]

Scala/White Images/Art Resource, NY

[Picha katika ukurasa wa 16]

Atlasi ya Catalan ya 1375, inayoonyesha sehemu fulani ya maeneo ambayo Ibn Battuta alitembelea

[Hisani]

Snark/Art Resource, NY