Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nini Hufanya Kibao cha Muziki Kiuzwe Sana?

Ni Nini Hufanya Kibao cha Muziki Kiuzwe Sana?

Ni Nini Hufanya Kibao cha Muziki Kiuzwe Sana?

BIASHARA ya muziki inabadilika-badilika upesi na ina ushindani mkubwa. Mapendezi ya wasikilizaji hubadilika, miziki iliyopendwa inapitwa na wakati, na mbinu za kurekodi na kusambaza muziki zinatokea. Wadhamini “hutafuta muziki motomoto kila wakati,” anasema Kelli S. Burns mtaalamu wa mawasiliano. Lakini si rahisi kufanya “muziki fulani” uuzwe kwa wingi. “Vijana wengi hutamani sana kuwa wasanii maarufu, . . . lakini si kazi rahisi kupata mkataba na kampuni ya kurekodi,” kinasema kitabu kimoja cha mwongozo.—Ona sanduku “Mabadiliko Katika Biashara ya Muziki,” kwenye ukurasa wa 6.

Kutunga Maneno ya Muziki

Wasanii (1) hujaribu sana kutunga maneno yanayogusa hisia za watu—maneno ambayo hufanya watu watafakari kuhusu matumaini yao, matarajio, na hisia za ndani zaidi. Watu huimba hasa kuhusu nini? Ikiwa umejibu, mahaba, hilo ndilo jibu sahihi. Wasanii pia hujaribu kubuni mstari fulani wenye maneno yanayovutia sana ambayo yatanasa akili ya msikilizaji na kubaki akilini kwa muda mrefu.

Kisha, msanii hurekodi wimbo wake kwa mara ya kwanza, ili usikizwe na kampuni ya kurekodi. Ikiwa baada ya kusikiliza wimbo ule wasimamizi wa kampuni ya kurekodi wanaona kwamba wimbo huo utakuwa maarufu, huenda basi wakampa msanii huyo mkataba wa kurekodi (2). Lakini ikiwa hawana uhakika na msanii huyo (labda kwa sababu yeye si maarufu sana), wanaweza kununua wimbo huo na kumpa msanii mwingine maarufu zaidi.

Ndani ya Studio

Ili kusimamia kazi ya kurekodi (3), kwa kawaida kampuni za kurekodi humtafuta producer, au mtayarishaji, aliye na uzoefu. Yeye huamua mtindo ambao msanii atatumia na kuidhinisha rekodi ya mwisho ya wimbo huo. Yeye ndiye hutafuta na kusimamia studio ya kurekodia itakayotumiwa, anatafuta pia wapangaji wa muziki, wanakili wa muziki, wanamuziki, waimbaji wa ziada, mainjinia wa kurekodi, na vifaa vitakavyorekodi muziki wa hali ya juu ambao utawavutia wasikilizaji.

Nyimbo nyingi hurekodiwa hatua kwa hatua, mara nyingi kuanzia kwa kurekodi midundo ya ngoma, gitaa mbalimbali, na piano. Kisha, sauti za waimbaji wanaoongoza muziki hurekodiwa pamoja na zile zinazoambatana na ala za muziki, na madoido mengine ya pekee ya sauti huchanganywa ili kutokeza nakala ya awali ya wimbo uliorekodiwa kielektroniki (4).

Uuzaji

Ili muziki uwe maarufu na kuuzwa zaidi, mara nyingi makampuni ya kurekodi hutokeza video za muziki (5). Video hizo zenye urefu wa dakika tatu hadi tano huenda zikatokeza msisimuko kama ule wa tamasha ya muziki na pia kusaidia wasikilizaji kumwona na kumsikia msanii huyo. Pia video hizo zinaweza kuiletea kampuni ya kurekodi pesa nyingi sana.

Wasanii wa muziki huuza albamu nyingi zaidi katika maeneo wanakofanyia tamasha za muziki (6). Hivyo wao hutangaza kuhusu albamu zao mpya popote waendapo na wanapopanga kufanya tamasha za muziki. Pia wasanii wengi hufungua Tovuti (7) na kupachika baadhi ya nyimbo, picha, video, blogu za kibinafsi, habari kuhusu tamasha za muziki zijazo, kutia ndani viunganishi vinavyowaelekeza mashabiki kwenye vituo ambavyo wanaweza kutoa maoni yao, na pia wanawaelekeza kwenye vituo ambavyo muziki wao huuzwa.

Ni nani anayeamua ikiwa muziki utakuwa maarufu sana? Ni wewe—msikilizaji. Hivyo basi, ni nini hukuchochea uchague muziki fulani? Unapochagua muziki, je, wewe huvutiwa na mdundo tu au msanii, au wewe una viwango vinavyokuongoza? Haya ni maswali muhimu, kwa sababu muziki una nguvu na unaweza kutuathiri sana. Mambo haya yanatukumbusha shauri muhimu kutoka kwa Muumba wetu: “Linda moyo wako kuliko vitu vingine vyote vinavyopaswa kulindwa, kwa maana ndiko zinakotoka chemchemi za uzima.”—Methali 4:23.

Unaweza kutii shauri hilo lenye hekima jinsi gani unapochagua muziki? Na ikiwa wewe ni mzazi, unaweza kutimiza jinsi gani jukumu lako la kuwalinda watoto wako dhidi ya hatari za kiroho, kiakili, na kihisia?

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Mabadiliko Katika Biashara ya Muziki

Intaneti, vyombo vya kurekodi muziki vya bei ya chini, pamoja na programu za kompyuta zimechangia sana mabadiliko katika biashara ya muziki. Siku hizi, wanamuziki wanaweza kurekodi muziki wa hali ya juu kwa ustadi sana wakiwa nyumbani na kuusambaza kote ulimwenguni. Kulingana na ripoti moja katika gazeti The Economist, “wasanii maarufu sana walirekodi na kusambaza muziki bila kutumia kampuni yoyote ya kurekodi.”