Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Uweke Pesa Akiba Badala ya Kuzitumia?

Kwa Nini Uweke Pesa Akiba Badala ya Kuzitumia?

Kwa Nini Uweke Pesa Akiba Badala ya Kuzitumia?

“KUWEKA akiba kunachosha,” ndivyo watu wengi wanavyosema. “Lakini inafurahisha kununua nguo, vifaa vya elektroniki, na vitu kama hivyo.”

Iwe umeathiriwa na kushuka kwa uchumi wa ulimwengu au la, unaweza kufaidika kwa kufikiria njia mbalimbali ambazo unaweza kuhifadhi pesa na njia za kuzitumia kwa hekima. Chunguza mashauri kutoka katika chanzo kinachotegemeka ambacho kimewasaidia mamilioni ya watu katika karne nyingi kushughulikia matatizo yao ya kifedha.

Misemo Mitatu ya Kale Yenye Hekima

Katika moja ya mifano yake, Yesu wa Nazareti alitaja kanuni fulani muhimu inayohusiana na mambo ya kiuchumi. Katika mfano huo bwana mkubwa alimwambia mtumishi wake hivi: “Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake!” (Mathayo 25:27, Biblia Habari Njema) Maneno ambayo Yesu alisema wakati huo ni muhimu sana leo. Acheni tuone sababu.

Hivi karibuni katika nchi fulani, faida iliyopatikana baada ya miaka kumi hivi, ilizidi kiasi cha pesa ambacho mtu alikuwa ameweka katika benki. Ingawa leo benki nyingi haziwapi watu faida kubwa hivyo, na faida inayopatikana kutokana na vitu ambavyo mtu huwekeza si ya kiasi kikubwa kama ile inayotazamiwa na wawekezaji, ni jambo la hekima kuweka pesa akiba kwa ajili ya mambo ya dharura.

Biblia inakazia jambo hilo inaposema: “Hekima ni ulinzi, kama vile pesa ni ulinzi.” (Mhubiri 7:12) Lakini pesa haziwezi kukulinda ikiwa huna zozote akibani! “Kila mmoja wenu,” Biblia inasema, “aweke kando kitu fulani katika akiba kulingana na anavyofanikiwa.”—1 Wakorintho 16:2.

Jinsi Unavyoweza Kuweka Pesa Akiba

Kwanza, kabla ya kununua kitu cha bei ghali, fikiria ikiwa kwa kweli unakihitaji.

Pili, ikiwa unahitaji kitu fulani, tafuta vitu vipya ambavyo vinauzwa kwa bei iliyopunguzwa au vitu vya mtumba vilivyo katika hali nzuri. Espen na Janne, wazazi fulani wanaoishi huko Norway, walihitaji kigari cha kumbebea mwana wao, Daniel. Walinunua kigari cha mtumba kilichokuwa katika hali nzuri kwa nusu ya bei ya kawaida. Espen anasema hivi: “Daniel atakapokuwa mkubwa aache kukitumia, nina hakika kwamba tutaweza kukiuza kwa bei nzuri.” Lakini anaonya: “Unaweza kutumia wakati mwingi kutafuta kitu cha bei nafuu.” *

Tatu, usinunue vitu bila kupangia; tumia wakati wa kutosha kufikiria kuhusu bidhaa unayotaka kununua. Ukihisi kwamba bado unahitaji sana bidhaa hiyo, unaweza kuitafuta katika duka linalouza vitu kwa bei ya chini au bidhaa za mtumba. Pia, mara nyingi unaweza kuokoa pesa iwapo hutahisi unalazimika kununua bidhaa zenye majina ya watengenezaji maarufu. Isitoshe, badala ya kununua nguo za kisasa zaidi za watoto kutoka kwenye maduka yanayouza vitu kwa bei ya juu, mbona usitumie nguo zilizotumiwa hapo awali na watoto wengine?

Vivyo hivyo, mama aliyejifungua kwa mara ya kwanza anaweza kutumia nepi zinazoweza kufuliwa. Kitabu Budgeting—Personal Spending and Money Management a Key to Weathering the Storm, kilichoandikwa na Denise Chambers, kinasema hivi: “Nepi zinazotupwa baada ya kutumiwa zitagharimu dola 2,000 au zaidi katika muda wa miaka 2. Nepi za kitambaa . . . zitagharimu dola 300 hadi 500 katika kipindi hichohicho cha miaka 2.” Akaongezea hivi: “Nepi za kisasa za kitambaa ni rahisi zaidi kutumia na haziharibu mazingira!”

Nne, kumbuka kwamba kununua vitu na kupika nyumbani hakugharimu sana kama kula kwenye mkahawa. Ikiwa una watoto wanaoenda shuleni, mbona usiwafundishe kubeba chakula kilichotayarishwa nyumbani badala ya kuwapa pesa za kununua chakula cha bei ghali? Na badala ya kununua vinywaji vya bei ghali, kunywa maji. Yana afya zaidi na si bei ghali.

Muda fulani uliopita familia zilikuwa zikikuza mboga kwenye bustani zao. Je, umewahi kufikiria kukuza chakula chako? Watu wengi, kutia ndani wale wanaoishi katika nyumba za orofa au nyumba ndogo, wana eneo fulani wanaloweza kutumia kukuza vitu. Utashangaa kuona kiasi cha chakula ambacho unaweza kukuza ukiwa na sehemu ndogo tu!

Fikiria hili pia: Ikiwa unahitaji kuwa na simu ya mkononi, je, unaweza kuitumia tu kwa ajili ya hali za dharura na ulipie mapema muda fulani wa maongezi? Au ikiwa una mashini ya kukausha nguo, je, umewahi kufikiria kupunguza matumizi yake? Labda unaweza kuanika nguo fulani—au zote—nje kwenye kamba. Pia unaweza kupunguza muda unaotumia vifaa vya kuondoa hewa yenye joto, vipasha-joto, au kifaa kingine cha kielektroniki. Kabla ya kuwasha vifaa hivyo, jiulize, ‘Je, hali ya hewa ni mbaya kiasi hicho?’ Pia unaweza kuzungumza na wengine ili ufahamu jinsi wanavyodhibiti matumizi yao ya umeme.

Pia ingefaa kufungua akaunti ya kuweka pesa akiba au uwekeze pesa zako katika mpango wa bima unaolipa faida. Kwa kuongezea, Hilton, mfanyakazi wa kujitolea nchini Afrika Kusini, anaeleza hivi: “Si jambo la hekima kuweka vitu vyako vyote vyenye thamani mahali pamoja. Nyakati nyingine, benki na mashirika mengine ya kifedha hufilisika. Tumewahi kujionea jambo hilo.” Kwa hiyo, weka akiba katika benki ambayo serikali itakurudishia pesa zako iwapo benki hiyo itafilisika.

Jinsi ya Kumaliza Deni

Kwanza, jaribu kulipa zaidi ya kiasi unachodaiwa kila mwezi kwenye kadi ya mkopo au deni lingine.

Pili, jitahidi kulipa deni linalodai ulipe riba ya kiasi cha juu zaidi.

Tatu, dhibiti jinsi unavyotumia pesa. Hilo ni jambo muhimu sana.

Je, umewahi kushawishiwa na matangazo ya kibiashara? Danny, mwanamume fulani mwenye familia nchini Sweden anakiri kwamba amewahi. Alikuwa na biashara nzuri lakini alilazimika kuiuza ili alipie deni la kadi yake ya mkopo. Alijifunza kutokana na hilo na sasa anadhibiti pesa zake. Anatoa ushauri huu: “Jihadhari na pupa. Jifunze kuishi kulingana na mapato yako.”

Deni la Lazima

Ni watu wachache wanaoweza kulipa pesa taslimu kwa ajili ya nyumba wanayonunua. Kwa hiyo, wengi huchukua mkopo kwenye benki ili kununua nyumba. Kiasi wanacholipa kila mwezi ili kurudisha pesa hizo huonwa ni kana kwamba wanalipa kodi ya nyumba. Lakini baada ya kulipa mkopo huo kwa muda mrefu, wanamiliki nyumba hiyo!

Pia watu wengi huona kuwa inafaa kuchukua mkopo ili kununua gari ambalo halitumii petroli nyingi. Wanapolipa mkopo huo upesi iwezekanavyo, gari hilo huwa na faida, na hiyo ni njia nyingine ya kuokoa pesa. * Wengine wameona ni jambo la hekima kununua gari la mtumba lililo katika hali nzuri na ambalo halijatumiwa sana. Wengine huokoa pesa kwa kutumia usafiri wa umma au hata kuendesha baiskeli.

Vyovyote vile, uwe na kiasi na uone mambo kihalisi kuhusiana na vitu unavyonunua na ufanye maamuzi ukiwa makini. Unaweza kukuza tabia ya kutumia pesa bila hekima na hilo litakuletea matatizo. Kwa hiyo, jitahidi kutumia pesa kwa uangalifu na kwa busara, na huenda ukafaulu kuwa na furaha ya kudumu.

Mbali na hilo, ili ufurahie kuhifadhi pesa, unapaswa kujua jinsi ya kuzitumia kwa hekima. Habari inayofuata itazungumzia jambo hilo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Ili uwe na hakika kwamba hununui bidhaa zilizoibiwa, ni jambo la hekima kumwuliza muuzaji jina lake, anwani yake na kumwomba risiti.

^ fu. 24 Kumbuka kwamba ukipoteza kazi yako na ushindwe kulipia mkopo, huenda ukapoteza nyumba au gari lako na pesa zote ulizokuwa umelipa kufikia wakati huo. Ingawa hivyo, wengi huamua kuwa na bima ya kuzuia hilo.

[Picha katika ukurasa wa 5]

NJIA ZA KUOKOA PESA

Tafuta vitu vinavyouzwa kwa bei iliyopunguzwa

Nunua nguo kwenye maduka yanayopunguza bei au nguo za mtumba

Wafundishe watoto wako kujitayarishia chakula nyumbani

[Picha katika ukurasa wa 6]

Punguza gharama za chakula kwa kukuza bustani ndogo ya mboga nyumbani. Punguza gharama kwa kuanika nguo nje