Mbinu za Ndege za Kuvua Samaki
Mbinu za Ndege za Kuvua Samaki
WAVUVI—wawe ni wanadamu au ndege—hukabiliana na angalau matatizo matatu: (1) kutafuta samaki, (2) kuwafikia, na (3) jinsi ya kuwashika.
Kwa kawaida Wamisri wa kale walivua samaki kwa kutumia chusa. Wavuvi hao walitumia mbinu ileile ambayo ilitumiwa na ndege fulani aina ya kulasitara muda mrefu kabla ya wanadamu kuanza kuitumia.
Kulasitara wa rangi ya kijivu, ndege ambaye hupatikana kwenye delta ya Mto Nile huko Misri hutumia mdomo wake wenye ncha kali kama mkuki kuvua samaki. Anaweza hata kuwadunga samaki wawili kwa wakati mmoja, na huenda akala zaidi ya nusu-kilo ya samaki kwa siku. Kwa hiyo, inaweza kusemwa kwamba kulasitara hutumia mbinu za ujanja zaidi za kuvua kuliko wanadamu.
Kwa ujumla, kulasitara wana ustadi wa kunyemelea na kushika samaki. Kulasitara hutembea polepole ndani ya maji yasiyo na kina kirefu au wakati mwingine anasimama tuli ndani ya maji akiwa tayari kushambulia kwa mdomo wake. Samaki anaposonga karibu naye, kulasitara hutosa kichwa chake ndani ya maji na kumdunga kwa mdomo wake. Siri ya ndege huyo ya kufanikiwa ni kuwa na subira.
Kuvua kwa Kutumia Chambo
Kulingana na kitabu The Life of Birds, kulasitara aliye na mgongo wa kijani huko Japani huwaiga watu wanaolisha samaki mikate kwenye maziwa yaliyotengenezwa na wanadamu. Ndege hao werevu hutumia vipande vya mkate kuwadanganya samaki ili waje karibu nao.
Yangeyange wa visiwa vya Karibea pia hutumia mkate kuwavutia samaki. Yangeyange wanaweza kutumia miguu yao ya rangi ya manjano kuwashika samaki hata bila kutumia chambo. Wakiwa wamesimama kwa mguu mmoja kwenye maji yasiyo na kina, wanatikisa-tikisa ule mguu mwingine ndani ya maji ili kuwavutia samaki wenye udadisi.
Mbinu ya Kunyakua Samaki
Ndege huvua samaki kwa kutumia mbinu mbalimbali. Tai wala-samaki, ambao mara nyingi huitwa furukombe, ni mfano mzuri wa ndege ambao huvua samaki kwa kuwanyakua kutoka majini. Wanaruka juu ya maji, wakichunguza kwa makini waone kama kuna samaki wanaoogelea juujuu. Wanapoona samaki, furukombe hukunja mabawa yao na kuteremka kwa kasi kuelekea kwenye maji, wakijipinda kadiri inavyohitajika na kumnyakua samaki kwa kucha zao. Mbinu hiyo hutaka furukombe alenge shabaha yake vizuri na awe na uwezo mzuri sana wa kuona.
Nyakati nyingine, tai mla-samaki wa Afrika hugundua kwamba amenyakua samaki mzito kuliko anavyoweza kubeba. Samaki anaweza kuwa na uzito wa kilo 2.7! Tai hufanya nini inapokuwa hivyo? Watu wanaochunguza vitu vya asili na wanyama wanasema wameona baadhi ya tai wakitatua tatizo hilo kwa kutumia mabawa yao kama makasia hadi ufuoni!
Kuruka Kutoka Juu Sana Hadi Ndani ya Maji
Ndege aina ya ganeti na polisi pia hupiga mbizi ili kuvua samaki, lakini wao huteremka kwa kasi kutoka angani. Kikundi kidogo cha ndege hao huruka pamoja wakitafuta makundi ya samaki yanayoogelea juujuu. Rangi ya fedha ya samaki hao hufanya maji ya bahari yaonekane kutoka angani yakiwa na rangi hafifu ya kijani badala ya bluu nzito. Ganeti na polisi wakiona rangi hiyo ya kijani kutoka angani, wanaanza kuvua samaki.
Wakiona kundi la samaki, ganeti hujitumbukiza kama mishale ndani ya maji kwa mwendo unaoweza kufikia kilomita 96.56 kwa saa. Unapowatazama ndege hao wakifanya hivyo unaweza kufikiri ni wapiga-mbizi katika mashindano ya Olimpiki. Ndege wengine wanapoona hekaheka hizo wao hujiunga haraka na wenzao kusherehekea mlo huo.
Tofauti na kulasitara, polisi na ganeti hawawadungi samaki wanapoingia ndani ya maji. Kwa kuwa wanajitosa kwa kasi sana, wao hutumbukia ndani sana ya maji. Kisha wanapoogelea kuelekea juu, wanawashika samaki na kuwameza wakiwa wazima.
Membe pia wana uwezo wa kupiga-mbizi kwa ustadi, lakini wao huambaa juu ya maji. Kitabu Handbook of the Birds of the World kinaeleza kwamba badala ya kujirusha ndani ya maji kutoka juu kama mshale, kama wanavyofanya polisi na ganeti, membe “huruka kwa ustadi, madaha na wepesi.” Wao humnyakua samaki anayeogelea juujuu. Ni mara chache sana tu ambapo wao huingia ndani ya maji kwa muda mfupi ili kumfuata samaki.
Wanavua Wakiwa Kikundi
Waari hawavutii sana kwa sababu ya midomo yao mikubwa, lakini wao huruka na kushika samaki kwa ustadi. Kwa kawaida, mwari wa rangi ya kahawia huruka kutoka juu hadi ndani ya maji ili akamate samaki, lakini pia wao hunyakua samaki kutoka kwa wavuvi wanaovuta nyavu zao. Lakini waari hufanikiwa sana wanapovua wakiwa kikundi.
Kwa kawaida, waari huishi katika makundi. Wanajulikana hasa kwa sababu ya kushirikiana wanapovua. Kwa kawaida, kundi la ndege zaidi ya kumi hutua ndani ya maji na kufanyiza nusu mviringo. Wao huogelea polepole wakiwaelekeza samaki kwenye maji yasiyo na kina. Wanapofanya hivyo, wao huinua mabawa yao kisha wanatumbukiza vichwa vyao wakati uleule ndani ya maji ili kuwakamata samaki kwa midomo yao.
Lakini kama tu ilivyo na wanadamu, mara nyingi ndege hawafaulu kuwakamata samaki. Hata hivyo, wao hufanikiwa zaidi kuliko wanadamu.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Tai mla-samaki wa Afrika
[Hisani]
Photolibrary
[Picha katika ukurasa wa 12]
Kulasitara mwenye rangi ya kijivu
[Picha katika ukurasa wa 13]
Ganeti wa kaskazini
[Picha katika ukurasa wa 13]
Membe
[Picha katika ukurasa wa 13]
Waari wa Australia