Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

John Foxe—Aliishi Nyakati Zenye Msukosuko

John Foxe—Aliishi Nyakati Zenye Msukosuko

John FoxeAliishi Nyakati Zenye Msukosuko

JE, WANADAMU hujifunza kutokana na mambo yaliyotukia wakati uliopita? Fikiria kuhusu swali hilo unapochunguza maisha ya John Foxe, Mwingereza aliyeandika kitabu akitarajia kwamba wasomaji wake wangeshutumu ukatili mbaya sana uliotukia katika nyakati zake.

Masimulizi ya John Foxe, yaliyoandikwa wakati wa yale Marekebisho Makubwa ya Kidini, yalikuwa na uvutano mkubwa juu ya watu wa Uingereza kwa karne nyingi. Kitabu chake kinachoitwa Acts and Monuments of the Church, kilichukua zaidi ya miaka 25 kukamilishwa. Na watu fulani wamesema kwamba Biblia pekee ndicho kitabu kilichokuwa na uvutano mkubwa zaidi katika lugha na utamaduni wa Waingereza.

Miaka Yenye Msukosuko

John Foxe alizaliwa huko Boston, Uingereza, mnamo 1516 au 1517, karibu wakati uleule ambao inasemekana kuwa Martin Luther alitundika tasnifu zake 95, au malalamishi yake, kwenye mlango wa kanisa fulani huko Wittenberg, Ujerumani. Kwa hiyo, Foxe, ambaye alizaliwa katika familia ya Wakatoliki, alizaliwa katika kipindi ambacho viongozi wa yale Marekebisho Makubwa ya Kidini walikuwa wakipinga mamlaka na mafundisho ya Kanisa Katoliki.

Foxe alijiunga na Chuo Kikuu cha Oxford, na alijifunza Kigiriki na Kiebrania, jambo ambalo lilimwezesha kusoma Biblia katika lugha zake za awali. Kwa wazi, imani yake ya Kikatoliki iliathiriwa kwa sababu ya hilo. Hata baadhi ya rafiki zake walianza kufikiri kwamba anataka kuwa Mprotestanti—jambo ambalo liliwafanya wamshtaki kwa wakuu wa chuo hicho. Baada ya hapo, Foxe alipelelezwa sana.

Baada ya kupokea shahada yake ya pili mnamo 1543, Foxe alipaswa kutawazwa kuwa kasisi. Lakini alikataa kutawazwa kwa sababu alipinga wazo la makasisi kulazimishwa kubaki wakiwa waseja. Msimamo huo ulibadili mambo kabisa. Kwa kuwa alishukiwa kuwa mwasi—shtaka ambalo angehukumiwa kifo iwapo lingethibitishwa—alijiuzulu kutoka kwenye chuo kikuu mnamo 1545. Akiacha kazi ya hali ya juu, Foxe akawa mkufunzi wa familia fulani karibu na Stratford-upon-Avon, huko Warwickshire, ambako alifunga ndoa na mwanamke aliyeitwa Agnes Randall.

Agnes, aliyekuwa raia wa eneo la karibu la Coventry, alimweleza Foxe kuhusu mjane anayeitwa Smith (au Smythe) aliyekuwa amewafundisha watoto wake zile Amri Kumi na sala ambayo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake, ambayo mara nyingi huitwa Sala ya Bwana. Hata hivyo, badala ya kuwafundisha watoto wake katika Kilatini, aliwafundisha mambo hayo katika Kiingereza. Kwa kuwa kufanya hivyo kulisemekana kuwa ni uhalifu, aliteketezwa kwenye mti, pamoja na wanaume sita walioshtakiwa kwa uhalifu kama wake. Kwa sababu ukosefu huo mkubwa wa haki uliwakasirisha watu sana, askofu wa eneo hilo alieneza uvumi kwamba watu hao waliteketezwa kwa sababu ya ule aliouita “uhalifu mkubwa zaidi” wa kula nyama Ijumaa na siku nyingine ambazo watu walipaswa kufunga.

Wafia imani hao waliwezaje kusoma Biblia katika Kiingereza? Miaka 150 hivi mapema, licha ya upinzani wa kanisa, Biblia ilikuwa imetafsiriwa kutoka Kilatini hadi Kiingereza na John Wycliffe, ambaye pia aliwazoeza wahubiri waliosafiri walioitwa Lollards. * Walibeba sehemu za Maandiko zilizoandikwa kwa mkono, ambazo waliwasomea watu. Bunge lilijaribu kuzuia utendaji huo. Kwa hiyo, mnamo 1401, bunge lilipitisha sheria iliyowapa maaskofu mamlaka ya kuwafunga, kuwatesa, na kuwateketeza waasi kwenye mti.

Akiogopa kukamatwa, Foxe alihamia London pamoja na familia yake, ambako baadaye alijiunga na watetezi Waprotestanti. Akiwa huko alitafsiri trakti za viongozi Wajerumani wa yale Marekebisho Makubwa ya Kidini katika Kiingereza na pia akatafsiri trakti nyingine zilizokuwa zimeandikwa katika Kilatini. Pia yeye mwenyewe aliandika trakti fulani.

Zaidi ya hilo, Foxe alianza kukusanya historia ya Lollards nchini Uingereza, na akaikamilisha mnamo 1554. Maandishi hayo yalichapishwa huko Strasbourg, ambalo leo ni jiji nchini Ufaransa, katika buku dogo la Kilatini lililofanyizwa kwa karatasi 212. Hayo yakawa maandishi yake ya kwanza katika kitabu chake kilichoitwa Acts and Monuments of the Church. Miaka mitano baadaye aliongezea sehemu nyingine kwenye kitabu hicho na mwishowe kikawa na kurasa kubwa 750.

Chuki ya Kidini Yasababisha Vifo

Yale Marekebisho Makubwa ya Kidini yalifanya wanaume, wanawake, na watoto wengi wachinjwe. Mnamo 1553, nchini Uingereza, Mkatoliki fulani shupavu aliyejulikana kama Mary Mwuaji alitawazwa kuwa malkia. Kwa kuwa katika mwaka wa 1534 Bunge la Uingereza lilikuwa limevunja uhusiano wake wote na Roma, Mary Mwuaji aliazimia kurudisha Uingereza chini ya mamlaka ya papa. Katika miaka mitano ya utawala wa Mary, wanaume na wanawake 300 hivi, kutia ndani viongozi wa kanisa la Waprotestanti, waliteketezwa kwa sababu ya uasi. Wengine wengi walifia gerezani.

Foxe aliokoka kipindi hicho kwa kuwa aliihamisha familia yake hadi Basel, Uswisi, punde tu Mary alipotawazwa. Mnamo 1559, mwaka mmoja tu baada ya dada ya Mary, Elizabeth aliyekuwa Mprotestanti, kutawazwa kuwa malkia, Foxe alirudi Uingereza pamoja na wengine waliokuwa wameenda uhamishoni. Mwaka huohuo, Elizabeth alirudisha ile Mamlaka Kuu, * iliyomfanya awe Gavana Mkuu wa Kanisa. Kwa sababu hiyo, mnamo 1570 Papa Pius wa Tano akamtenga Elizabeth na kanisa. Punde baada ya hapo, hila za kimataifa dhidi ya Uingereza zikafichuliwa, kutia ndani njama za kumwua malkia huyo Mprotestanti. Kwa sababu hiyo, mamia ya Wakatoliki walihukumiwa kuwa wahaini na wakauawa kwa amri ya Elizabeth.

Makanisa hayo yanayodai kuwa ya Kikristo, yaani, ya Katoliki na Protestanti, yalikuwa yamepotoka kama nini kutokana na mafundisho ya Yesu Kristo! Aliwafundisha hivi: “Endeleeni kuwapenda adui zenu na kusali kwa ajili ya wale wanaowatesa ninyi.” (Mathayo 5:44) Kwa kuwa Wakatoliki na Waprotestanti walipuuza mwongozo huo wa wazi kabisa, waliuletea Ukristo suto kubwa sana—jambo lililokuwa limetabiriwa katika Biblia. “Ile njia ya kweli itatukanwa” kwa sababu ya watu wanaodai kuwa Wakristo, akaandika mtume Petro.—2 Petro 2:1, 2.

Foxe Anakamilisha Kitabu Chake

Huko Uingereza, Foxe alianza kushughulikia toleo lake lililokuwa na masimulizi mengi, na huenda baadhi ya wasomaji wake walikuwa wamejionea mambo aliyoandika. Toleo lake la kwanza la Kiingereza—lililokuwa na kurasa 1,800 na michoro kadhaa iliyochongwa kwenye mbao—lilitolewa mnamo 1563, na mara moja likauzwa sana.

Toleo la pili lilitolewa miaka saba baadaye. Mabuku yake mawili, yalikuwa na zaidi ya kurasa 2,300 na michoro 153. Mwaka uliofuata, Kanisa la Anglikana liliagiza kwamba nakala ya kitabu cha Foxe iwekwe kando ya Biblia katika makanisa yote makubwa ya Uingereza na katika nyumba za wakuu wa makanisa kwa ajili ya watumishi na wageni wao. Makanisa ya parokia yakafanya vivyo hivyo pia. Hata watu ambao hawakujua kusoma na kuandika walifaidika kutokana na michoro yake, nayo ilibaki akilini mwao kwa muda mrefu.

Kufikia wakati huo, Foxe alikuwa amejiunga na Wapuriti, yaani, Waprotestanti waliohisi kwamba kujitenga tu na kanisa la Roma hakukutosha. Walifundisha kwamba mambo yote yaliyohusiana na Ukatoliki yanapaswa kuondolewa—jambo ambalo kwa kushangaza liliwafanya wapingane na Kanisa la Kiprotestanti la Uingereza ambalo liliendeleza desturi na mafundisho mengi ya Kikatoliki.

Kwa kuwa maandishi yake yalifichua maovu mengi ya kidini yaliyofanywa katika nyakati hizo zenye msukosuko, John Foxe alibadili maoni ya kidini na ya kisiasa nchini Uingereza kwa karne nyingi zilizofuata.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Ona makala “The Lollards, Courageous Bible Preachers,” katika toleo la Mnara wa Mlinzi la Agosti 1, 1980 (Kiingereza).

^ fu. 14 Kitabu The Leading Facts of English History, cha D. H. Montgomery, kinasema kwamba mnamo 1534, Bunge lilipitisha ile Mamlaka Kuu, “iliyomtawaza Henry bila kupingwa kuwa kichwa pekee cha Kanisa, na yeyote aliyempinga angeshtakiwa kwa uhaini. Alipotia sahihi hati hiyo, Mfalme alipindua utamaduni wa miaka elfu moja, na Uingereza ikajisimamia ikiwa na Kanisa la Taifa lisilomtegemea Papa.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 28]

KITABU CHA WAFIA IMANI CHA FOXE

Kanisa Katoliki lilipoendelea kupigana na yale Marekebisho Makubwa ya Kidini, watu fulani barani Ulaya kama vile Jean Crespin walikuwa wakiandika kuhusu mateso na mauaji ya wafia imani nchini mwao. * Kwa sababu hiyo, kitabu cha Foxe Acts and Monuments of the Church kikaja kuitwa Kitabu cha Wafia Imani cha Foxe (Foxe’s “Book of Martyrs”). Baadaye, matoleo yaliyorekebishwa na kufupishwa yalipotolewa, kichwa hicho kilichobuniwa kikachukua mahali pa kile ambacho Foxe alichagua.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 26 Ona makala “Kitabu cha Wafia Imani cha Jean Crespin” katika toleo la Machi 2011 la gazeti hili.

[Hisani ya Picha]

© Classic Vision/age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 27]

John Wycliffe aliwatuma wahubiri waliosafiri walioitwa “Lollards”

[Hisani ya Picha]

From the book The Church of England: A History for the People, 1905, Vol. II

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

From Foxe’s Book of Martyrs