Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Vibonyezo kwenye mashine za kuweka na kutoa pesa [ATM] katikati mwa miji mikubwa nchini Uingereza vilipochunguzwa, vilionyesha kuwa vina bakteria nyingi hatari sawa tu na vikalio katika vyoo vya umma.—THE TELEGRAPH, UINGEREZA.

“Wakati mwingine, wanasayansi wanashtuliwa na matetemeko ya nchi [kama yale yaliyotokea New Zealand mwaka huu na Haiti mwaka jana] kwa sababu yanatokea kwenye nyufa ambazo hazijagunduliwa. . . . Hilo huzusha swali linalotia wasiwasi: Ni matetemeko mangapi makubwa yanayoweza kutokea katika maeneo ambayo yana nyufa zisizoonekana kuwa hatari au ambazo hazijulikani?”—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.

“Raia wanne matajiri zaidi duniani . . . ni matajiri kuliko nchi 57 zilizo maskini zaidi duniani.”—FOREIGN POLICY, Januari/​Februari 2011, MAREKANI.

Wamiliki wa asilimia 90 ya biashara zote nchini Poland wameripoti kwamba wameibiwa au kudanganywa na wafanyakazi wao katika miaka miwili iliyopita.—GAZETA PRACA, POLAND.

Kanisa moja la Kikatoliki nchini Brazili sasa linawatoza faini ya dola 300 za Marekani bibi-arusi ambao huchelewa kufika kwenye arusi zao. Wenzi wa ndoa lazima waandike cheki kabla ya sherehe, na itarudishwa tu iwapo watafika kwa wakati.—G1, BRAZILI.

Viungo vya Papa Haviwezi Kutumiwa Kupandikiza

Joseph Ratzinger alipokuwa kadinali wa Kanisa Katoliki, alikuwa ametoa idhini ili atakapokufa viungo vya mwili wake vipandikizwe watu wengine, linasema gazeti la Kiitaliano La Repubblica. Hata hivyo, tangu achaguliwe kuwa papa, viungo vya mwili wa Benedict wa 16 haviwezi kutolewa vipandikizwe mtu mwingine. Kwa nini? “Mwili wa papa ni mali ya kanisa lote,” anaeleza askofu mkuu Zygmunt Zimowski, mmoja wa wakuu wa Vatikani. “Kwa hiyo, inaeleweka kwamba papa anapokufa mwili wake unapaswa kuhifadhiwa ukiwa kamili, kwa kuwa huenda baadaye ukatumiwa kwa njia fulani katika ibada.”

Pesa Badala ya Uhai?

Je, watu wanaweza kukubali kuuza mwaka mmoja wa uhai wao kwa bei ya euro milioni moja? Nchini Ujerumani, mwanamume 1 kati ya 4 na mwanamke 1 kati ya 6 angefanya hivyo, inasema ripoti ya taasisi moja maarufu inayoitwa Emnid iliyokusanya maoni kwa niaba ya jarida Reader’s Digest Deutschland. Watu wenye umri wa chini waliohojiwa, ndio waliokubali kwa wingi zaidi kwamba wangefanya hivyo—asilimia 29 ya walio na umri wa kati ya miaka 14 hadi 29, na asilimia 25 ya walio na umri kati ya miaka 30 hadi 39 wangechagua pesa badala ya uhai. Hata hiyo, watu wenye umri mkubwa walionekana kuwa wanathamini uhai zaidi. Ni asilimia 13 pekee ya watu walio na umri wa kati ya miaka 50 hadi 59 na asilimia 11 ya walio na umri unaozidi miaka 60 ambao wangekubali kuuza mwaka mmoja wa maisha yao.