Mti wa Krismasi Ulitumiwa Kabla ya Ukristo
Mti wa Krismasi Ulitumiwa Kabla ya Ukristo
KATIKA sehemu nyingi ulimwenguni pote, mti wa kijani-kibichi wa Krismasi huonekana kuwa ishara ya sherehe za sikukuu na biashara. Mti huo umekuwa ishara ya kidini tangu mwanzo wa historia ya wanadamu.
Hilo linaonekana wazi katika Jimbo la Bohuslän lililoko pwani ya magharibi ya Sweden na katika jimbo la karibu la Østfold huko Norway. Katika majimbo hayo, michoro zaidi ya 75,000 iliyochongwa kwenye miamba imepatikana katika maeneo 5,000 hivi. Wataalamu wa vitu vya kale wanasema kwamba mingi ya michoro hiyo ilichongwa kati ya mwaka wa 1,800 na 500 hivi K.W.K. *
Michongo hiyo yenye kustaajabisha inafunua mambo fulani kuhusu imani ya watu walioishi zamani sana kabla ya kuzaliwa kwa Yesu wa Nazareti. Kwa mfano, watafiti fulani wanasema kwamba zamani za kale katika maeneo ambayo sasa ni Sweden na Norway, miti ya kijani-kibichi kama vile misonobari ilitumiwa kama ishara takatifu.
Kwa nini watu walioishi mbali kwenye maeneo ya pwani ya kaskazini ya dunia walichonga michoro ya miti ya misonobari kwenye miamba? Wasomi fulani wanasema huenda sababu moja ni kwamba miti hiyo haikupatikana kwa urahisi katika kipindi cha kabla ya Ukristo wakati michoro hiyo ilipochongwa. Inaeleweka ni kwa nini mti unaoendelea kuwa na rangi ya kijani-kibichi au “hai” huku miti mingine ikinyauka wakati wa majira ya baridi ulionwa kuwa fumbo.
Katika tamaduni nyingi ulimwenguni, miti imekuwa ishara ya uhai, ustahimilivu, na umilele. Jambo hilo linatusaidia kuelewa ni kwa nini michoro inayofanana na misonobari ilichongwa kwenye miamba katika maeneo ya Bohuslän na Østfold karne nyingi kabla ya mti huo kupatikana kwa wingi huko.
Kitabu Rock Carvings in the Borderlands, kilichochapishwa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Hazina za Kitaifa ya Sweden, kinasema hivi: “Michoro ya miti iliyochongwa kwenye miamba inaonyesha kwamba mapema kuanzia Enzi ya Shaba, maeneo ya Skandinavia kusini yaliunganishwa kidini na kitamaduni na sehemu ambayo kwa sasa ni bara la Ulaya na sehemu kubwa ya bara la Asia. Watu ambao walitegemea ukulima na ufugaji walifuata dini na kosmolojia (kuchunguza kuhusu mpangilio wa kiasili wa ulimwengu). Waliabudu miungu ileile ingawa majina ya miungu hiyo ilitofautiana.”
Kijitabu The Rock Carving Tour, kilichochapishwa na Jumba la Makumbusho la Wabohuslän kilisema hivi: “Wachongaji hawakutaka kuchonga michoro kuhusu maisha ya kila siku tu. Tunaamini kwamba huenda sanamu zao zilikuwa
aina fulani ya sala au dua kwa miungu.” Kijitabu hicho kinaendelea kusema: “Imani yao ilihusu hasa mambo kama vile mzunguko wa milele wa maisha, nguvu za uzazi, kifo, na kuzaliwa upya.”Ikieleza kuhusu mkusanyo wa pekee wa sanaa ambazo zilichongwa zamani kabla ya sanaa ya uandikaji kuanza huko Ulaya kaskazini, kitabu Nationalencyklopedin, ensaiklopedia ya kitaifa ya Sweden, kinasema hivi: “Kuwepo kwa picha nyingi zinazoonyesha mambo ya ngono kunaonyesha jinsi madhehebu ya uzazi ilivyokuwa muhimu katika dini ya watu walioishi katika maeneo ya Kaskazini wakati wa Enzi ya Shaba.”
Inaonekana kwamba desturi zilizohusisha mti huo zilienea na kukubalika katika sehemu nyingi. Encyclopædia Britannica inasema hivi kuhusu mti wa Krismasi: “Kuabudu miti lilikuwa jambo la kawaida kati ya wapagani wa Ulaya na waliendelea na zoea hilo baada ya kuwa Wakristo.” Ibada hiyo iliendelezwa katika desturi nyingine kutia ndani “desturi . . . ya kuweka mti wa Krismasi kwenye mwingilio au ndani ya nyumba wakati wa sikukuu zinazofanywa katikati ya majira ya baridi kali.”
Desturi za kale zilizohusisha mti huo zilianza kuwa maarufu katika mwaka wa 1841, wakati ambapo familia ya kifalme ya Uingereza ilitumia msonobari uliopambwa katika sherehe yao ya Krismasi. Leo mti wa Krismasi unajulikana ulimwenguni pote, na miti hiyo, iwe halisi au bandia, inanunuliwa sana. Kwa sasa, michoro iliyochongwa kwenye miamba huko Skandinavia inatoa ushahidi wa kimyakimya kwamba mti wa Krismasi hauna chanzo cha Kikristo.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Baadhi ya maeneo yenye michoro hiyo iliyochongwa kwenye miamba huko Bohuslän imetiwa katika Orodha ya UNESCO ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni.
[Blabu katika ukurasa wa 12]
Miti iliyochongwa kwenye miamba inaonyesha kwamba ibada ya kipagani ya mti wa Krismasi ilianza kabla ya wakati wa Kristo
[Picha katika ukurasa wa 13]
Miti iliyochongwa kwenye miamba huko (1) Torsbo, (2) Backa, na (3) Lökeberg, Sweden
[Hisani ya Picha]
Courtesy Stiftelsen för dokumentation av Bohusläns hällristningar