Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtu Mwenye Udadisi Anayekumbukwa Katika Historia

Mtu Mwenye Udadisi Anayekumbukwa Katika Historia

Mtu Mwenye Udadisi Anayekumbukwa Katika Historia

● Ungependa watu wakumbuke nini kukuhusu? Watu watakumbuka nini wanapofikiria kukuhusu? Kwa sababu ya kuhangaikia sana jinsi watakavyokumbukwa, watu wengi hujaribu kujijengea jina kwa kuwa magwiji wa sayansi, siasa, michezo, na sanaa. Lakini namna gani ikiwa ungekumbukwa hasa kwa sababu ya maswali uliyouliza?

Miaka 500 iliyopita, mwanamume mmoja huko Amerika ya Kati aliuliza maswali mengi yenye kuamsha fikira. Alikuwa chifu aliyeitwa Nicarao, na inaonekana kwamba jina “Nikaragua” lilitokana na jina lake. Kabila la watu wake, nchi alimoishi, na ziwa lao kubwa, yote yaliitwa kwa jina lake.

Watu wa kabila la Nicarao waliishi katika kipande cha ardhi kilichokuwa kati ya Bahari ya Pasifiki na Ziwa kubwa la Nikaragua. Muda mfupi baada ya Columbus kugundua Mabara ya Amerika, Wahispania walienda kutembelea eneo hilo. Kapteni Gil González Dávila aliongoza jeshi lake kutoka eneo ambalo leo linaitwa Kosta Rika, kuelekea kaskazini na kuingia eneo la Nicarao mwaka wa 1523 W.K.

Hebu wazia jinsi watu hao walivyokuwa na wasiwasi walipokuwa wakisafiri eneo wasilolijua. Walifurahi kama nini walipokutana na Chifu Nicarao! Walikaribishwa kwa ukarimu kama ilivyo desturi ya watu wa Nikaragua hadi leo na walipewa zawadi mbalimbali kutia ndani dhahabu nyingi sana.

Nicarao alitaka kupata majibu ya maswali ambayo alikuwa amejiuliza kwa muda mrefu. Maswali mengine yalizuka alipotembelewa na Wahispania. Waandishi wa matukio wanasema kwamba alimwuliza Kapteni González maswali yafuatayo:

Umewahi kusikia kuhusu ile gharika kubwa iliyoharibu wanadamu na wanyama wote? Je, Mungu ataleta tena gharika duniani? Ni nini hutukia baada ya kifo? Jua, mwezi, na nyota husonga katika njia gani? Vitu hivyo vimening’inia jinsi gani angani? Viko umbali gani angani? Jua, mwezi, na nyota zitaacha kuangaza lini? Upepo hutoka wapi? Ni nini husababisha kuwe na joto au baridi, nuru au giza? Kwa nini urefu wa siku hutofautiana mwaka mzima?

Ni wazi kwamba Nicarao alikuwa na hamu ya kujifunza kuhusu ulimwengu wa asili uliomzunguka. Maswali yake yanaonyesha mengi kuhusu imani yake ya kidini. Yanafunua kwamba alikuwa na mapendezi na mahangaiko ambayo watu wengi leo wanayo. Kwa kuwa Nicarao na watu wake walijua kuhusu gharika kubwa, hilo linatukumbusha kuhusu masimulizi yaliyo katika Biblia.—Mwanzo 7:17-19.

Hata ingawa kuwasiliana na pepo na kutoa dhabihu za wanadamu kama matambiko yalikuwa baadhi ya mambo yaliyokuwa yamekita mizizi katika utamaduni wa watu wa Nicarao, alihangaikia mwenendo na maisha ya watu wake. Maswali yake yanaonyesha kwamba kiasili watu wanaongozwa na dhamiri. Kuhusiana na jambo hilo, mtume Paulo aliandika hivi: ‘Dhamiri yao huwatolea ushahidi na, katikati ya fikira zao wenyewe, wanashtakiwa au hata kutetewa.’—Waroma 2:14, 15.

Leo, sanamu ya Chifu Nicarao imesimamishwa kama kumbukumbu karibu na mahali ambapo inadhaniwa alikutana kwa mara ya kwanza na wavumbuzi Wahispania. Udadisi wake uliofanya afikirie kwa uzito kuhusu maisha na ulimwengu uliomzunguka, unaweza kuwa mfano mzuri kwetu kuiga.—Waroma 1:20.

[Ramani katika ukurasa wa 21]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Nikaragua

AMERIKA KUSINI

BAHARI YA ATLANTIKI