Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Alpenhorn—Muziki Unaotoka Kwenye Mti

Alpenhorn—Muziki Unaotoka Kwenye Mti

Alpenhorn​—Muziki Unaotoka Kwenye Mti

KWA karne nyingi, wakazi fulani wa Milima ya Alps ya Uswisi wametumia kifaa fulani cha pekee ili kuwasiliana kinachoitwa alpenhorn. Huenda kisionekane kuwa kinafaa kwa ajili ya mawasiliano​—baadhi ya vifaa hivyo ni mara mbili ya kimo cha watu ambao huvipiga. Hata hivyo, alpenhorn inaweza kubebwa kwa mkono. Baadhi ya vifaa hivyo vinaweza kutenganishwa na kuwa vipande kadhaa vinavyoweza kuingizwa katika sanduku. Mtu anaweza kusikia mlio wa alpenhorn akiwa umbali wa kilomita 10 upande ule mwingine wa mabonde ya Milima ya Alps!

Kutengeneza Alpenhorn

Kwa kuwa misonobari inayopatikana milimani ndiyo hutumiwa kutengeneza alpenhorn, inafaa kabisa kwamba kifaa hicho kinapatikana kwenye Milima ya Alps ya Uswisi. Hali za kiasili hufanya miti ya msonobari ambayo hukua kwenye milima yenye mwinuko mkali ijipinde kwenye sehemu ya chini.

Baada ya kuchagua mti, mtengenezaji wa alpenhorn huupasua vipande viwili na kukomba sehemu ya ndani kwa kutumia patasi fulani za pekee. Kufanya hivyo kunaweza kuchukua saa 80 hivi! Kisha anapiga msasa sehemu ya ndani ya mti huo ili kuulainisha. Kisha ataunganisha vipande hivyo kwa gundi na kuvifunga pamoja kwa nguvu kwa kutumia ganda la mbetula. Pia anaunganisha kifaa kwenye sehemu ya chini ambacho kitasaidia kusimamisha alpenhorn inapopigwa. Mwishowe, baada ya kuunganisha kifaa cha kupulizia na kurembesha sehemu ya chini kwa kuipaka rangi au kuichonga, mtengenezaji huipaka aina ya fulani ya vanishi itakayoisaidia kustahimili hali ya hewa ya aina yoyote ile.

Matumizi ya Kitamaduni

Kwa miaka mingi, wachungaji wameipiga alpenhorn kutoka sehemu za juu za malishoni ili kuwajulisha watu wa familia zao walioko chini kwenye mabonde kwamba “mambo yote ni shwari.” Hata hivyo, wao hukitumia hasa kuwaita ng’ombe wao ili wawakamue. Tangu zamani, wakamaji wa Uswisi wameamini kwamba sauti tamu ya alpenhorn huwafanya ng’ombe watulie wanapokamwa.

Wakati wa majira ya baridi kali, wakati ambapo ng’ombe wamefungiwa kwenye mazizi katika mabonde, wachungaji wengi huenda na alpenhorn zao hadi mjini na kuzipiga ili wapate michango. Nyakati fulani zilizopita, alpenhorn ilitumiwa kuwaita wanaume kwenda vitani.

Unaipigaje Alpenhorn?

Huenda unapoitazama alpenhorn kwa mara ya kwanza ukafikiri kwamba ni rahisi kuipiga. Sababu ni kwamba haina mashimo au sehemu za kubadili mlio. Jambo gumu zaidi huwa ni kudhibiti kiasi cha hewa kinachoingia kwenye baragumu hiyo ili sauti inayotakikana itokee.

Baragumu ya alpenhorn hutokeza sauti 12 tu za kiasili. Ingawa huwezi kupiga muziki wa aina zote kwa kutumia kifaa hicho, muziki kadhaa umeandikwa hasa kwa ajili ya kifaa hicho, na mtu mwenye uzoefu anaweza kuupiga kwa ustadi sana.

Watungaji maarufu wametia ndani sauti ya alpenhorn katika okestra zao. Kwa mfano, Leopold Mozart—baba ya Wolfgang Amadeus Mozart—alitunga muziki unaoitwa “Sinfonia Pastorella” kwa ajili ya okestra ili upigwe hasa kwa kutumia aina fulani ya alpenhorn inayoitwa corno pastoritio​. Brahms aliiga sauti ya alpenhorn ya Uswisi kwa kutumia filimbi na baragumu, naye Beethoven, katika muziki wake unaoitwa Pastoral, aliiga sauti ya alpenhorn ili kutokeza hisia za maisha ya malishoni.

Alpenhorn ilitajwa kwa mara ya kwanza katika maandishi huko Uswisi katika mwaka wa 1527, katika kitabu cha uhasibu cha makao ya watawa ya St.Urban. Sasa, zaidi ya miaka 500 baadaye, sauti nyororo ya alpenhorn bado inasikika kwenye maeneo ya malishoni ya Uswisi.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Alpenhorn inaweza kutenganishwa kuwa vipande kadhaa na kubebwa kwa mikono