Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Utafune Tambuu?

Je, Utafune Tambuu?

Je, Utafune Tambuu?

KATIKA mtaa mmoja kusini mwa Asia, mtu mwenye urafiki anatabasamu na kuonyesha meno yake meusi na mdomo uliojaa mate mekundu kama damu. Kisha anatema mate mekundu yasiyopendeza kwenye kijia cha watu wanaotembea kwa miguu. Mtu huyo anatafuna tambuu.

Kuanzia Afrika Mashariki, Pakistan, na India hadi maeneo yaliyo Kusini-Mashariki mwa Asia, Papua New Guinea, na Micronesia, mamia ya mamilioni ya watu hutafuna tambuu​—na hiyo ni karibu asilimia 10 ya idadi ya watu ulimwenguni pote. Wauzaji wa tambuu, wakati mwingine wakiwa pamoja na watoto wao, huiuza sokoni na kando ya barabara. Ili kuwavutia wateja, wauzaji wengine huweka taa zenye kumetameta pamoja na wasichana walio nusu uchi wanaoitwa “warembo wa tambuu” kwenye maduka yao.

Ulimwenguni pote, uuzaji wa tambuu huleta faida ya mabilioni ya dola. Lakini tambuu ni nini? Kwa nini watu wengi hutafuna tambuu? Zoea hilo linaathirije afya yao? Biblia ina maoni gani kuhusu zoea hilo? Na mtu anawezaje kuacha zoea hilo?

Tambuu Ni Nini?

Kile kinachoitwa tambuu ni popoo au kokwa la mpopoo ambao ni mmea unaopatikana huko Pasifiki na Kusini-Mashariki mwa Asia. Neno tambuu linatokana na mmea unaoitwa mtambuu ambao hauna uhusiano wowote na mpopoo. Watafunaji wa tambuu huweka popoo pamoja na chokaa kidogo juu ya jani la mtambuu. Chokaa huchochea kutokezwa kwa alkaloidi inayolewesha. Watafunaji wengine huongeza vikolezo, tumbaku, au sukari ili kuboresha ladha yake.

Mchanganyiko huo huchochea kutokezwa kwa mate mengi na kuyafanya yawe mekundu kama damu. Kwa sababu hiyo, watafunaji hutema mate mara kwa mara hata wanapokuwa ndani ya magari yaliyo mwendoni na wakati mwingine wao huwatemea mate wapita-njia.

Zoea Lenye Madhara

“Popoo zimekuwa zikitafunwa tangu zamani na zimetumiwa hasa kwa sababu za kijamii, kitamaduni, na kidini,” inasema ripoti moja katika jarida Oral Health. “Mara nyingi watafunaji huona zoea hilo kuwa halina madhara na husema kwamba wanajihisi wakiwa na afya, msisimuko, [na] kuhisi joto mwilini . . . Hata hivyo, kuna uthibitisho kwamba zoea hilo lina madhara.” Madhara gani?

Mashirika ya kuzuia matumizi ya dawa za kulevya yanasema kwamba mojawapo ya kemikali zilizo katika tambuu inaweza kufanya mtu awe mraibu. Kwa kweli, watafunaji fulani hutafuna kokwa 50 hivi za mpopoo kwa siku! Muda si muda, meno hugeuka rangi, na huenda wakawa na ugonjwa wa fizi. Jarida Oral Health, linasema kwamba kwa wale wanaotafuna tambuu kwa ukawaida, huenda utando wao wenye ute ulio ndani ya kinywa ukageuka na kuwa na rangi ya kahawia na kunyauka. Huenda pia wakapata makovu mdomoni.

Kutafuna tambuu pia kunahusianishwa na aina fulani ya kansa ya mdomo, ambayo pia inaweza kutokea nyuma ya koo. Visa vingi vya kansa ya mdomo miongoni mwa watu wazima huko Kusini-Mashariki mwa Asia vinathibitisha jambo hilo. Nchini Taiwan, asilimia 85 hivi ya kansa za mdomo huripotiwa kati ya watu wanaotafuna tambuu. Isitoshe, “visa vya kansa ya mdomo nchini Taiwan​—ambayo ni moja kati ya magonjwa 10 yanayosababisha vifo katika kisiwa hicho—vimeongezeka mara nne hivi katika miaka 40 iliyopita,” linasema gazeti The China Post.

Hali iko hivyo sehemu nyingine. Gazeti Papua New Guinea Post-Courier linasema: “Tambuu ambayo wakazi wengi wa Papua New Guinea wanapenda kutafuna, huwaua watu 2,000 hivi kwa mwaka na husababisha matatizo mengine mengi ya afya, linasema Shirika la Kitiba la PNG.” Daktari mmoja ambaye pia huandika makala za kitiba anasema: “Madhara yanayotokana na kutafuna tambuu kwa muda mrefu . . . ni mengi kama yale ya uvutaji sigara,” na yanatia ndani magonjwa ya moyo.

Maoni ya Biblia Ni Nini?

Biblia si kitabu cha kitiba, na hakitaji moja kwa moja utafunaji wa tambuu. Hata hivyo, Biblia ina kanuni nyingi zinazoweza kumsaidia mtu kuishi maisha safi, yenye afya, na yaliyo bora. Fikiria kuhusu mistari ya Biblia inayofuata na maswali yanayozuka.

“Wapendwa, . . . acheni tujisafishe wenyewe kila unajisi wa mwili na roho, tukiukamilisha utakatifu katika kumwogopa Mungu.” (2 Wakorintho 7:1) “Mtoe miili yenu iwe . . . takatifu, yenye kukubalika kwa Mungu.” (Waroma 12:1) Je, mtu anaweza kuwa mtakatifu, au safi machoni pa Mungu ikiwa angeuchafua mwili wake kwa kutafuna tambuu?

“Kupitia kwake [Mungu] tuna uhai.” (Matendo 17:28) “Kila zawadi njema na kila tuzo kamilifu hutoka juu.” (Yakobo 1:17) Uhai ni zawadi yenye thamani kutoka kwa Mungu. Je, mtu anayejihusisha katika mazoea ambayo yanaweza kusababisha ugonjwa anaiheshimu zawadi hiyo?

“Hakuna anayeweza kuwatumikia mabwana wawili.” (Mathayo 6:24) “Sitaruhusu kitu chochote kinitawale.” (1 Wakorintho 6:12) Je, mtu anayetaka kumpendeza Mungu atajiruhusu awe mtumwa wa zoea fulani lisilo safi, na kuliacha limtawale?

“Mpende jirani yako kama wewe mwenyewe.” (Marko 12:31) “Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya.” (Waroma 13:10, Biblia Habari Njema) Je, kweli tutakuwa tukiwaonyesha wengine upendo ikiwa tutakuwa na zoea chafu na lenye kuchukiza la kutema mate mekundu kwenye vijia ambavyo watu wanapitia au sehemu nyingine?

Bila shaka, tunavuna tunachopanda. (Wagalatia 6:7, 8) Hiyo ni sheria ya msingi ya asili. Hivyo, tukipanda mazoea mabaya, tutavuna mabaya. Lakini tukiishi kulingana na matakwa ya Mungu, yanayotia ndani kuwa na mazoea mazuri, hatutavuna tu mambo mazuri bali pia tutapata furaha ya kweli na yenye kudumu. Ikiwa una mazoea ya kutafuna tambuu lakini unataka kuishi maisha mazuri yenye kuthawabisha kwa kufanya yaliyo sawa machoni pa Mungu, unawezaje kuacha zoea hilo? Mbona usisali na kufikiria hatua tatu zifuatazo ambazo zimetumika kwa mafanikio kwa muda mrefu?

Hatua Tatu za Kuacha Zoea Hilo

1. Uwe na sababu inayokuchochea. Ili kushinda zoea baya, unapaswa kuwa na sababu yenye kuchochea kuliko tu kutambua kwamba zoea hilo linadhuru afya yako. Kwa kweli, watu wengi huendelea kutafuna tambuu, kuvuta tumbaku, au kutumia dawa za kulevya hata ingawa wanajua kwamba zoea hilo ni hatari kwa afya na uhai wao. Ili upate kichocheo zaidi, mbona usitumie Biblia kujifunza kumhusu Muumba wako na jinsi anavyokupenda? “Neno la Mungu liko hai nalo lina nguvu,” inasema Waebrania 4:12.

2. Mwombe Mungu msaada. Yesu Kristo alisema: “Endeleeni kuomba, nanyi mtapewa; endeleeni kutafuta, nanyi mtapata; endeleeni kupiga hodi, nanyi mtafunguliwa. Kwa maana kila mtu anayeomba hupokea, na kila mtu anayetafuta hupata, na kila mtu anayepiga hodi hufunguliwa.” (Luka 11:9, 10) Mungu wa kweli, Yehova anapoona jinsi unavyosali kwa unyoofu na kumwomba akutegemeze na kukupa nguvu, hatakupuuza. “Mungu ni upendo,” inasema 1 Yohana 4:8. Mtume Paulo Mkristo alijionea upendo huo. Aliandika hivi: “Kwa mambo yote nina nguvu kupitia yeye anayenipa nguvu.”​—Wafilipi 4:13.

3. Tafuta msaada wa wengine. Watu unaoshirikiana nao wanaweza kuwa na uvutano mzuri au mbaya juu yako. Methali 13:20 inasema: “Anayetembea na watu wenye hekima atakuwa na hekima, lakini anayeshirikiana na wajinga atapatwa na mabaya.” Kwa hiyo chagua marafiki wako kwa hekima! Miongoni mwa Mashahidi wa Yehova, kuna wengi ambao walikuwa na zoea la kutafuna tambuu. Lakini kwa kushirikiana na waabudu wenzao na kujifunza Biblia, walipata msaada waliohitaji ili kushinda zoea hilo chafu.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 24, 25]

WALIACHA ZOEA LA KUTAFUNA TAMBUU

Mwandishi wa Amkeni! aliwahoji watu watano waliokuwa na zoea la kutafuna tambuu lakini sasa wameacha. Hebu soma masimulizi yao.

Ni nini kilichokufanya uanze kutafuna tambuu?

Pauline: Wazazi wangu walinipa tambuu nilipokuwa mtoto mchanga. Hilo lilikuwa zoea katika kijiji chetu katika kisiwa cha Papua New Guinea.

Betty: Baba yangu alinipa tambuu nilipokuwa na umri wa miaka miwili. Nilipokuwa kijana, nilikuwa nikibeba kokwa nyingi sana za mpopoo hivi kwamba ungefikiri kwamba mimi ni mpopoo! Nilikuwa na uraibu mbaya sana hivi kwamba jambo la kwanza nililofanya nilipoamka ni kutafuna tambuu.

Wen-Chung: Nilianza kutafuna tambuu nilipokuwa na umri wa miaka 16. Ulikuwa mtindo wa wakati huo uliomfanya mtu aonekana kuwa mtu mzima, nami nilitaka kuonwa hivyo.

Jiao-Lian: Niliuza tambuu ili kujiruzuku. Ili nifaulu, niliona kwamba ilibidi nionje bidhaa niliyokuwa nikiuza ili nihakikishe kwamba ilikuwa bora. Hilo lilifanya niwe mraibu.

Zoea hilo liliathirije afya yako?

Jiao-Lian: Midomo na meno yangu yalikuwa mekundu kama damu. Ninaaibika kutazama picha nilizopigwa nilipokuwa nikitafuna tambuu. Bado mimi hupata vidonda mdomoni.

Pauline: Nilikuwa nikipata vidonda mdomoni, kuhisi kichefuchefu, na kuharisha.

Betty: Nilikuwa na uzito wa kilogramu 35 tu, uzani mdogo sana kwa mtu mzima aliye na kimo changu. Meno yangu yalikuwa mabovu, na mara nyingi niliyasafisha kwa kutumia bidhaa ngumu ya kusugulia sufuria.

Sam: Nilipatwa sana na ugonjwa wa fizi na kuharisha. Sasa nina jino moja tu! Kusugua meno kwa kutumia bidhaa ngumu ya kusugulia sufuria hakukunisaidia.

Ni nini kilichokufanya uache zoea hilo?

Pauline: Nilisoma katika Biblia kwenye 2 Wakorintho 7:1 kwamba Mungu anataka “tujisafishe wenyewe kila unajisi wa mwili.” Niliamua kujaribu kumpendeza Muumba wangu.

Sam: Nilitaka roho takatifu ya Yehova Mungu iniongoze maishani, kwa hiyo nilisali kwa Yehova anisaidie kushinda kishawishi cha kutafuna tambuu. Alijibu sala zangu. Sijatafuna tambuu kwa miaka 30 hivi.

Jiao-Lian: Nilipokuwa nikisoma Biblia, niliona maneno, “Safisheni mikono yenu, ninyi watenda-dhambi.” (Yakobo 4:8) Maneno hayo yalinigusa sana. Ningewezaje kutumia na kuuza tambuu huku nikijua madhara yake? Mara moja niliamua ‘kusafisha mikono yangu’ kutokana na zoea hilo chafu ambalo huharibu uhusiano wa mtu pamoja na Yehova.

Umefaidikaje kwa kuacha zoea hilo?

Wen-Chung: Nilianza kutafuna tambuu ili nikubaliwe na marafiki wangu. Sasa ninafurahia urafiki wenye thamani zaidi pamoja na Yehova na pia ndugu na dada zangu wa kiroho.

Sam: Sasa nina afya bora kimwili na pia kiroho. Na kwa sababu sipotezi pesa kwa mazoea mabaya, ninaweza kuandalia familia yangu mahitaji yao.

Pauline: Ninajihisi huru na safi. Meno yangu ni meupe na yenye nguvu. Na nyumba na bustani yangu haijai maganda ya popoo na madoa mekundu yasiyopendeza.

Betty: Nina dhamiri safi na afya bora. Mimi ni mwalimu wa shule na mtumishi wa wakati wote.

[Picha]

Betty

Pauline

Wen-Chung

Jiao-Lian

Sam

[Mchoro/​Picha katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Zoea la kutafuna tambuu linaweza kusababisha matatizo hatari ya afya

Meno yaliyogeuka rangi na ugonjwa wa fizi

Makovu ndani ya mdomo

Kansa ya mdomo

[Picha katika ukurasa wa 22]

Popoo zikiwa zimefungwa katika jani la mtambuu