Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Kiarabu Kilivyokuja Kuwa Lugha ya Wasomi

Jinsi Kiarabu Kilivyokuja Kuwa Lugha ya Wasomi

Jinsi Kiarabu Kilivyokuja Kuwa Lugha ya Wasomi

KWA karne nyingi, Kiarabu kimekuwa lugha ya wasomi. Kuanzia karne ya nane W.K., wasomi walioongea Kiarabu wa kutoka miji mbalimbali ya Mashariki ya Kati walitafsiri na kusahihisha maandishi ya kisayansi na ya kifalsafa ya tangu enzi za Ptolemy na Aristotle. Kwa njia hiyo, wasomi walioongea Kiarabu wakahifadhi na kuziboresha maandishi ya wasomi wa kale.

Kitovu cha Mawazo ya Kila Namna

Katika karne ya saba na ya nane Wakati wetu wa Kawaida, familia mbili zilianza kutawala huko Mashariki ya Kati—ya kwanza ikiwa ile ya Umayyad ambayo ilifuatwa na ile ya Abbasid. Kwa kuwa raia wao walioishi Arabia, Asia Ndogo, Misri, Palestina, Uajemi, na Iraki walikuwa wameathiriwa na uvutano wa Ugiriki na India, watawala hao wapya walikuwa wamepata hazina ya elimu ya hali ya juu. Familia ya watawala wa Abbasid ilijenga mji mkuu mpya, Baghdad, nao ukaja kuwa kitovu cha mawazo ya kila namna. Waarabu walikutania hapo na Waajemi, Waarmenia, Wachina, Wagiriki, Wahindi, Wakoptiki, Waturuki, Wayahudi, na Wasogdiana, waliotoka ng’ambo ya Mto Oxus, ambao kwa sasa unajulikana kama Mto Amu Dar’ya, ulioko Asia ya Kati. Walisoma na kujadili mambo ya kisayansi, na kubadilishana mawazo mbalimbali ya kitaaluma.

Watawala wa nasaba ya Abbasid waliokuwa Baghdad waliwatia moyo wataalamu wenye vipawa wachangie maendeleo ya elimu katika milki yao, haidhuru wataalamu hao walitoka wapi. Hatua kwa hatua, jitihada zilifanywa ili kukusanya na kutafsiri makumi ya maelfu ya vitabu kuhusu mambo mbalimbali kama vile kemia, hisabati, hesabu za maumbo, tiba, muziki, falsafa, na fizikia.

Khalifa al-Manṣūr, aliyetawala kuanzia mwaka wa 754 hadi 775 W.K., aliwatuma mabalozi kwenda Bizantiamu kwenye makao ya mfalme ili wakusanye maandishi ya hesabu ya Kigiriki. Khalifa al-Ma’mūn (813-833 W.K.) aliendeleza jambo hilo na kuchochea kazi ya kutafsiriwa kwa vitabu vya Kigiriki katika Kiarabu ambayo iliendelea kwa zaidi ya karne mbili. Kwa hiyo, kufikia mwisho wa karne ya kumi, karibu vitabu vyote vya falsafa na sayansi vya Wagiriki vilivyokuwepo vilikuwa vimetafsiriwa katika Kiarabu. Lakini wasomi Waarabu walifanya mengi zaidi ya kutafsiri tu. Waliandika vitabu vyao wenyewe.

Vitabu vya Waarabu

Watafsiri wengi Waarabu walifanya kazi kwa usahihi na kwa haraka sana. Hivyo, wanahistoria fulani wamedai kwamba huenda watafsiri hao walifahamu mambo waliyotafsiri. Zaidi ya hilo, wasomi kadhaa walitegemea sana habari zilizotafsiriwa ili wafanye utafiti wao.

Kwa mfano, daktari aliyekuwa pia mtafsiri Ḥunayn ibn Isḥāq (808-873 W.K.), ambaye alikuwa Mkristo kutoka Siria, alichangia pakubwa kueleweka kwa uwezo wa kuona. Maandishi yake yaliyotia ndani michoro sahihi ya sehemu mbalimbali za jicho, yalikuja kutumiwa kugundua na kutibu magonjwa ya macho huko Uarabuni na Ulaya pia. Mwanafalsafa aliyekuwa pia daktari, Ibn Sīnā, anayejulikana kwa jina Avicenna huko Ulaya (980-1037 W.K.), aliandika vitabu chungu nzima vilivyohusu mambo mbalimbali kama maadili na mantiki na vilevile mambo ya tiba na metafizikia. Mkusanyo wake wa mambo ya kitiba yaliyojulikana wakati huo, Canon of Medicine, ulitia ndani mawazo ya wanafalsafa maarufu Wagiriki, Galen na Aristotle. Mkusanyo huo uliendelea kuwa kitabu cha msingi cha kanuni za kitiba kwa karibu miaka 400.

Watafiti Waarabu walipenda mbinu ya kisayansi ya kufanya utafiti ili kuthibitisha nadharia, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya kisayansi. Hilo liliwafanya waupime tena mzingo wa dunia na kusahihisha kazi za kijiografia za Ptolemy. “Walithubutu pia kuchambua maandishi ya Aristotle,” anasema mwanahistoria Paul Lunde.

Maendeleo katika elimu yalionekana katika njia nyingi, kama vile ujenzi wa vidimbwi vya maji, mifereji, na magurudumu ya kupigia maji, na baadhi ya vitu hivyo vinapatikana hadi leo. Maandishi mapya kuhusu kilimo, upandaji wa mimea, na sayansi ya uhifadhi wa udongo na mimea iliwawezesha wakulima kuchagua mimea iliyofaa maeneo hususa, na hivyo kuboresha mazao.

Katika mwaka wa 805 W.K., Khalifa Hārūn ar-Rashīd alifungua hospitali ya kwanza kabisa katika milki yake kubwa. Muda si muda, kila jiji kubwa katika milki yake likawa na hospitali.

Vituo Vipya vya Masomo

Miji kadhaa huko Uarabuni ilikuwa na maktaba na vituo vya masomo maalumu. Huko Baghdad, Khalifa al-Ma’mūn alifungua taasisi ya kutafsiri na kufanyia utafiti iliyoitwa Bait al-Hikma, jina linalomaanisha “Nyumba ya Hekima.” Wafanyakazi wake walitia ndani wasomi waliolipwa mshahara. Inasemekana kwamba maktaba kuu mjini Cairo ilikuwa na mabuku zaidi ya milioni moja. Wakati huohuo, Córdoba, ambao ulikuwa mji mkuu wa Hispania wakati wa utawala wa familia ya Umayyad, ulikuwa na maktaba 70, zilizowafanya wasomi na wanafunzi kutoka maeneo yote ya Uarabuni waende huko. Kwa zaidi ya karne mbili, jiji la Córdoba lilikuwa kituo maarufu cha elimu.

Huko Uajemi, mfumo wa hesabu za Wagiriki ulipatanishwa na ule wa India, ambako wanahisabati walikuwa wamebuni mfumo wa kutumia nambari sufuri na hesabu za vipeuo (positional notation). Katika mfumo huo wa kuandika nambari, nambari mojamoja huwa na thamani kulingana na mahali ilipoandikwa na mahali ambapo nambari sufuri imewekwa. Kwa mfano, nambari moja (1) inaweza kuwa na thamani ya moja, kumi, mia moja, na kadhalika. Mfumo huu “ulirahisisha kazi ya kufanya hesabu za kila aina na hata kutokeza mfumo wa aljebra,” akaandika Lunde. Wasomi Waarabu pia walipiga hatua kubwa katika nyanja ya hesabu za maumbo, hesabu za trigonometria, pamoja na usafiri wa baharini.

Wakati ambapo elimu ya kisayansi na hisabati ilikuwa imefikia kilele huko Uarabuni, sehemu nyingine za ulimwengu hazikupendezwa na elimu. Jitihada sawa na hizo zilikuwa zikiendelea barani Ulaya katika Enzi za Kati, hasa kwenye makao ya watawa, ili kuhifadhi maandishi ya wasomi wa kale. Hata hivyo, jitihada hizo hazikuwa na mafanikio sawa na yale ya Uarabuni. Hata hivyo, mapema katika miaka ya 1900, mambo yalianza kubadilika wakati tafsiri za wasomi Waarabu zilipoanza kupenya pole kwa pole katika Nchi za Magharibi. Hatimaye, tafsiri hizo zilizidi kupenya na kuongoza kwenye kile kipindi cha mwamko wa kisayansi barani Ulaya.

Naam, historia inaonyesha wazi kwamba hakuna taifa au jamii ya watu inayoweza kujisifu kwamba ndiyo imeleta maendeleo yaliyopo katika elimu ya kisayansi na mambo mengine. Jamii za leo zilizo na elimu nyingi zimepata mambo mengi kutokana na jamii za kale zilizowahimiza watu kufanya utafiti, zikachambua mambo ambayo wasomi wengine walikuwa wameandika, na kuwachochea wataalamu kufanya uchunguzi zaidi.

[Ramani katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

▪Uvutano wa Umayyad

□Uvutano wa Abbasid

HISPANIA

Córdoba

BIZANTIAMU

Roma

Constantinople

Mto Oxus

UAJEMI

Baghdad

Yerusalemu

Cairo

ARABIA

[Picha katika ukurasa wa 27]

Mchoro wa jicho wa Ḥunayn ibn Isḥāq

[Picha katika ukurasa wa 27]

Ukurasa kutoka kwenye kitabu cha Avicenna “Canon of Medicine”

[Picha katika ukurasa wa 28]

Wasomi Waarabu katika maktaba moja huko Basra, 1237 W.K.

[Hisani]

© Scala/​White Images/​Art Resource, NY

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]

Eye diagram: © SSPL/​Science Museum/​Art Resource, NY; Canon of Medicine: © The Art Gallery Collection/​Alamy