Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Kuwa rais kunamsukuma mtu aone uhitaji wa kusali.”​—BARACK OBAMA, RAIS WA MAREKANI.

Walipoulizwa wachague njia ya kuonyesha uzalendo wao, asilimia 56 ya Waargentina wenye umri wa kati ya miaka 10 na 24 walisema kwamba wangependa kuvalia jezi ya timu ya kandanda ya taifa.​—LA NACIÓN, ARGENTINA.

Matokeo ya utafiti fulani yalidokeza kwamba “inakadiriwa kwamba asilimia 33 ya chakula kinachozalishwa ulimwenguni pote kwa ajili ya wanadamu hupotea au kutupwa, na hiyo ni kama jumla ya tani bilioni 1.3 kwa mwaka.”​—SHIRIKA LA CHAKULA NA KILIMO LA UMOJA WA MATAIFA, ITALIA.

“Siku hizi, vita na ripoti za vita zimeenea ulimwenguni pote, kwa hiyo jeshi la nchi yetu lazima liwe tayari siku zote kuwalinda watu wake na kila kitu ambacho tunaona kuwa ni kitakatifu kutokana na maadui wanaotoka nchi nyingine.”​—PATRIARCH KIRILL, MKUU WA KANISA OTHODOKSI LA URUSI.

Kiwango cha juu kabisa cha aksidenti za magari kilichoripotiwa kwa kampuni moja ya bima nchini Ujerumani katika mwaka wa 2010, kilionyesha kwamba aksidenti hizo zilitokea kati ya saa moja na saa mbili asubuhi. “Mojawapo ya njia muhimu zaidi ya kuzuia aksidenti ni kuwa na wakati wa kutosha wa kusafiri unapoelekea kazini asubuhi,” anasema ofisa wa kampuni hiyo.​—PRESSEPORTAL, UJERUMANI.

Viongozi Wachanga Huko Malasia

Kipindi maarufu cha mashindano kwenye Televisheni nchini Malasia kinalenga kumsaka imamu mzuri, au kiongozi wa dini ya Kiislamu. Kipindi hicho kinaitwa “Imam Muda,” au “Kiongozi Mchanga” na kinarekodiwa huko Kuala Lumpur. Washiriki, walio na umri wa kati ya miaka 18 hadi 27, kutoka katika malezi mbalimbali, huchujwa mmoja baada ya mwingine hadi abaki mmoja tu. Zawadi ambazo mshindi anapewa zinatia ndani pesa na gari jipya, lakini mshindi pia anaajiriwa kazi ya imamu, analipiwa karo ya kusomea nchini Saudi Arabia, na kukatiwa nauli ya kwenda hija huko Mecca. Washiriki ni lazima wajue vizuri madaraka ya imamu, wawe na uwezo wa kujadili mambo ya kidini na matukio ya kisasa, na kukariri vifungu vya Kurani. Aliyebuni kipindi hicho anasema kwamba lengo lake hasa ni “kuwavuta vijana” kwenye Uislamu.

Kukosa Busara Kwenye Mtandao

Watu wengi wanaotumia vituo vya mawasiliano hawaoni kwamba kutoa habari zao za siri kutakuwa na madhara baadaye. Hata hivyo, kutokuwa na busara kwenye Intaneti kunaweza kukuletea madhara mengi baadaye maishani. Kulingana na mwalimu mkuu wa shule ya sekondari anayeitwa Timothy Wright, aliyenukuliwa katika gazeti la Australia, Sydney Morning Herald, “teknolojia ya kisasa imefanya neno moja tu ambalo halikufikiwa vizuri, uchongezi, picha isiyofaa au kufichua mambo ya siri ya mtu mwingine yabaki daima katika rekodi na mtu yeyote anayetaka anaweza kuyasoma kwenye kituo cha mawasiliano.” Hilo linamaanisha kwamba “makosa yanayofanywa na mtu akiwa na umri wa miaka 15 bado yanaweza kupatikana na mwajiri miaka 10 baadaye,” anasema Wright.