Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Vinavutia?

Kwa Nini Vinavutia?

Kwa Nini Vinavutia?

NI NJIA gani za mawasiliano zilizoonyeshwa hapa chini ambazo wewe umetumia katika mwezi uliopita?

Mazungumzo ya uso kwa uso

Barua au kadi iliyoandikwa kwa mkono

Simu

Barua-pepe

Ujumbe mfupi wa simu

Ujumbe mfupi kupitia kompyuta

Kupiga gumzo kupitia video

Kituo cha mawasiliano

Hakujawahi kuwa na njia nyingi za kuwasiliana kama ilivyo leo, kila njia ikiwa na faida na ubaya wake. Fikiria mifano kadhaa:

MAZUNGUMZO YA USO KWA USO

Faida: Unaweza kuona ishara za mwili na za uso, na kusikia hisia katika sauti.

Ubaya: Lazima wahusika wote wawepo ili kuzungumza.

BARUA AU KADI ILIYOANDIKWA KWA MKONO

Faida: Inaonyesha unapendezwa kibinafsi na mwenzako.

Ubaya: Inachukua muda kuandika na kumfikia mhusika.

BARUA-PEPE

Faida: Inaweza kuandikwa na kumfikia mhusika haraka.

Ubaya: Mara nyingi hisia hazionekani​—na ni rahisi kueleweka vibaya.

Kisha kuna vituo vya mawasiliano, ambavyo wengine wanasema ndiyo njia bora zaidi ya kuwasiliana. Kuna mamia ya vituo vya mawasiliano, na kituo maarufu zaidi​—Facebook—​kina washiriki milioni 800 hivi! “Ikiwa Facebook ingekuwa nchi,” inasema Time magazine, “ingekuwa nchi ya tatu kwa ukubwa, baada ya China na India.” Vituo vya mawasiliano ni nini, na kwa nini vimekuwa maarufu sana?

Kituo cha mawasiliano ni Tovuti inayowawezesha washiriki kusambaza habari zao kati ya marafiki ambao wamechagua. “Ni njia nzuri sana ya kuwasiliana,” anasema Jean, mwenye umri wa miaka 21. “Vituo vya mawasiliano pia ni njia inayofaa ya kuwaonyesha watu wengine picha za safari au matukio mengine.”

Mbona mtu asiandike barua? ‘Inachukua muda mrefu sana,’ huenda wengine wakasema​—na itakugharimu sana ikiwa unahitaji kutoa nakala ya picha nyingi. Mbona basi mtu asipige simu? Pia, kufanya hivyo kunachukua muda​—hasa kwa sababu lazima umpigie mtu mmojammoja na huenda wengine wasiwe nyumbani au wasiwe na wakati wa kuzungumza wakati wewe una wakati wa kuzungumza. Namna gani kutuma barua-pepe? Danielle, mwenye umri wa miaka 20 anasema hivi: “Siku hizi hakuna mtu anayejibu barua-pepe, na hata wanapofanya hivyo, huenda ikachukua majuma mengi kabla ya kupata majibu. Lakini ninapotumia kituo cha mawasiliano, ninapachika tu maelezo yangu kuhusu mambo ninayofanya, na marafiki zangu wanapachika maelezo kuhusu siku yao. Sisi sote tutapata habari mara moja tunapoingia kwenye Tovuti hiyo. Ni rahisi sana!”

Hilo halimaanishi kwamba mazungumzo kwenye kituo cha mawasiliano huwa ni ya upuuzi mtupu. Kwa mfano, msiba unapotokea​—kama tetemeko la nchi na tsunami iliyopiga sehemu fulani za Japani Machi 11, 2011—​watu wengi hutumia vituo vya mawasiliano ili kufahamu hali ya wapendwa wao.

Fikiria kisa cha Benjamin, anayeishi nchini Marekani. Anasema hivi: “Watu hawangeweza kutumia simu baada ya tsunami iliyotokea nchini Japani. Rafiki yangu aliniambia kwamba alikuwa ametuma barua-pepe kwa rafiki yetu huko Tokyo, lakini hakuwa amepata majibu. Mara moja nikachukua simu yangu ya mkononi na kufungua Intaneti na kwenda kwenye ukurasa wa rafiki yetu katika kituo cha mawasiliano. Papo hapo, niliona ujumbe mfupi aliokuwa ameandika akisema kwamba alikuwa salama na angetueleza mengi zaidi baadaye.”

Benjamin anaendelea kusema hivi: “Ili niwasiliane na rafiki zangu waliomfahamu na ambao hawakuwa na akaunti katika kituo cha mawasiliano, nililazimika kutuma ujumbe mmoja baada ya mwingine kupitia barua-pepe. Ilinichukua muda mrefu kupata anwani zao na kuwaandikia wote. Katika muda wa siku chache nilipokea majibu kadhaa. Mtu mmoja alijibu baada ya majuma mawili! Watu hao walikuwa wakipokea barua-pepe nyingi sana hivi kwamba ilikuwa vigumu sana kujibu zote. Wakati mwingi sana ungeokolewa kwa kutumia vituo vya mawasiliano. Kila mtu angejulishwa kilichokuwa kikiendelea baada ya dakika chache tu!”

Kwa wazi, kuna faida za kutumia vituo vya mawasiliano. Lakini je, kuna hatari zozote? Ikiwa ndivyo, ni hatari gani hizo, na unaweza kuziepukaje?

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 5]

INATUMIWA JINSI GANI?

1. Pachika ujumbe kwenye ukurasa wako.

2. Wote walio kwenye orodha yako ya marafiki wanapokea ujumbe huo wanapoingia kwenye kurasa zao​—na wewe unapokea ujumbe wao unapoingia kwenye ukurasa wako.