Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Teknolojia ya Mawasiliano

Teknolojia ya Mawasiliano

Teknolojia ya Mawasiliano

● Fikiria kisa hiki cha kuwaziwa. Kwa muda mrefu watu walikuwa wakimdhihaki Sam kwa sababu alikataa kukubali kutumia teknolojia mpya, ambayo ni njia rahisi ya kuwasiliana na watu wa familia na marafiki. Kila mtu, hata watoto wa Sam wanaobalehe walisema kwamba walitaka kutumia teknolojia hizo mpya. Sam alimwambia hivi binti yake mwenye umri wa miaka 16 kwa mzaha, “Laiti watu wangekuwa wakizungumza uso kwa uso kama zamani!”

Kisha Sam akaanza kubadili maoni yake. Aliwafikiria watu ambao hakuwa amewaona au kuzungumza nao kwa miaka mingi. Alifikiria kuhusu watu wa familia yake ambao walionekana kuwa na shughuli nyingi hivi kwamba hangeweza kuwasiliana nao. ‘Nikitaka kuendelea kuwasiliana na watu hao wote,’ Sam akajiambia, ‘huenda nikahitaji kuanza kutumia njia hiyo mpya.’ Kisa hicho kilitokea katika maeneo ya vijijini huko Marekani katikati ya karne ya 20. Mwishowe, Sam, ambaye kwa muda mrefu hakutaka kutumia teknolojia mpya, alikuwa anafikiria kuwa na simu.

Tusonge mbele kufikia mwaka wa 2012. Mjukuu wa Sam anayeitwa Nathan, ametoka tu kuzungumza kwenye simu na marafiki wake wa karibu, Roberto na Angela, ambao walikuwa wamehamia nchi fulani ya mbali. ‘Walihama zaidi ya miaka kumi iliyopita!’ Nathan anajiambia, huku akishangaa jinsi wakati hupita upesi.

Kwa miaka mingi, Nathan ameridhika kuwa akiwapigia simu mara kwa mara watu wa familia na marafiki ambao wamehamia maeneo ya mbali. Hata hivyo, sasa inaonekana kwamba kila mtu​—kutia ndani watoto wa Nathan wanaobalehe—​anawasiliana kupitia vituo vya mawasiliano.

Watu wanamdhihaki Nathan kwa sababu amekataa kuanza kutumia teknolojia hiyo mpya. Anasema hivi: “Ninakosa sana siku zile ambazo watu walizungumza kwenye simu na ungeweza kusikia sauti ya mwenzako.” Lakini sasa Nathan anaanza kubadili maoni. ‘Nikitaka kuendelea kuwasiliana na watu hao wote,’ anajiambia, ‘huenda nikahitaji kuanza kutumia njia hiyo mpya.’

Je, umewahi kuhisi kama Nathan? Kiasili, wanadamu wanapenda kuwasiliana. (Mwanzo 2:18; Methali 17:17) Kwa kuwa watu wengi sana wanafanya hivyo kupitia vituo vya mawasiliano, unapaswa kujua nini kuhusu teknolojia hiyo?