Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uhandisi wa Kisilika wa Nyigu

Uhandisi wa Kisilika wa Nyigu

Je, Ni Kazi ya Ubuni?

Uhandisi wa Kisilika wa Nyigu

● Nyigu wamesifiwa kwa wahandisi stadi. Kwa nini ufafanuzi huo unafaa?

Fikiria hili: Nyigu hujenga na kudumisha maskani yake kwa kutumia karatasi ya pekee sana, ambayo yeye mwenyewe huitengeneza. * Mdudu huyo hukusanya nyuzinyuzi kutoka kwa mimea na miti iliyokauka mahali popote pale anapozipata​—kwenye magogo, vigingi vya ua, vigingi vya kupitishia nyaya za simu, au mbao za nyumba. Kisha, anatafuna vipande-vipande hivyo vilivyo na sukari nyingi ya mbao, na kuongeza mate yake yanayonata yenye protini nyingi. Mchanganyiko huo hutokeza nta inayokauka na kufanyiza karatasi nyepesi, thabiti, na isiyoraruka kwa urahisi. Kwa kuongezea, mate hayo yanafanya karatasi hiyo iwe na uwezo wa pekee wa kutokeza na kufyonza joto, na hivyo kusawazisha hali ya joto ndani ya sega kunapokuwa na baridi.

Nyigu hujenga sega lake “funda baada ya funda.” Mwishowe, mwavuli wa karatasi usiopenyeza maji ulio na vyumba vidogo-vidogo vyenye pembe sita hutokezwa—umbo hilo la pembe sita hufanya maskani hiyo iwe thabiti na isichukue nafasi kubwa. Nyigu wanaoishi maeneo yaliyo na mvua nyingi huongeza mate mengi kwa sababu ya uwezo wa mate hayo wa kuzuia maji kupenya ndani. Zaidi ya hilo, wadudu hao huchagua kwa makini eneo ambalo linaweza kuwa kinga nzuri. Kisha, wanajenga masega chini ya kinga hiyo yakining’inia huku yakishikiliwa na bua au kikonyo cha jani. Vilevile, nyigu hawachafui mazingira, tofauti kabisa na njia ambazo wanadamu hutumia kutengeneza karatasi ambazo huchafua hewa, maji, na udongo!

Inaeleweka ni kwa nini wachoraji wa ramani za ujenzi na watafiti wanachunguza sega la nyigu ili wabuni vifaa madhubuti zaidi vya kujengea vilivyo vyepesi, thabiti, vinavyopindika kwa urahisi, na vinavyoweza kuoza.

Una maoni gani? Je, mdudu mwenye ubongo mdogo unaolingana na chembe mbili za mchanga alibuni ustadi wa kujenga makao yake na kutengeza karatasi kwa kutumia akili yake mwenyewe? Au ustadi wake wa kutumia kemikali na uhandisi wake wa hali ya juu ni uthibitisho wa kwamba alibuniwa?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Spishi kadhaa za nyigu hujenga masega ya karatasi. Vyumba vyake hutumiwa kuhifadhia mayai, yanayoangua viwavi baadaye.