Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Utukufu” wa Nyota

“Utukufu” wa Nyota

“Utukufu” wa Nyota

JE, UMEWAHI kustaajabu unapotazama maelfu ya nyota usiku katika anga lisilo na mawingu? Ulipotazama nyota hizo zikimetameta, huenda uligundua kwamba zinatofautiana kwa mnga’o na hata rangi. Biblia inasema hivi kwa usahihi: “Nyota hutofautiana na nyota kwa utukufu.”​—1 Wakorintho 15:41.

Kwa nini nyota hutofautiana kwa utukufu au mnga’o? Kwa mfano, kwa nini nyota fulani ni nyeupe na nyingine ni za bluu, manjano, au nyekundu? Kwa nini nyota humetameta?

Kiini cha nyota huwa na moto mwingi wa nyuklia ambao hutokeza nishati nyingi sana. Nishati hiyo huenea hadi kwenye matabaka ya nje ya nyota, ambapo inanururishwa angani kama nuru inayoonekana au miale isiyoonekana. Huenda ukashangaa kujua kwamba nyota zenye joto jingi huwa na rangi ya bluu, na zile zisizo na joto jingi huwa na rangi nyekundu. Kwa nini zinatofautiana kwa rangi?

Nuru inaweza kusemwa kuwa mtiririko wa chembe zinazoitwa fotoni, ambazo pia hutenda kama mawimbi ya nishati. Nyota zenye joto jingi hutoa fotoni zenye nishati nyingi ambazo zina mawimbi mafupi yanayopatikana kwenye upande wa rangi ya bluu katika spektra ya rangi. Tofauti na hilo, nyota zisizo na joto jingi hutokeza fotoni zenye nishati chache ambazo zinapatikana kwenye upande wa rangi nyekundu katika spektra ya rangi. Jua letu liko katikati ya spektra ya rangi kwa sababu linatokeza kiasi kikubwa cha nuru yenye rangi ya kijani na manjano. Kwa nini basi halionekani kuwa na rangi ya kijani? Linatokeza pia nuru nyingi iliyo na rangi zile nyingine zinazoweza kuonekana katika spektra ya rangi. Kwa sababu hiyo, jua huonekana kuwa jeupe linapotazamwa kutoka angani.

Angahewa ya Dunia Hubadili Rangi ya Jua

Angahewa huchuja mwangaza tunaoona kutoka kwa jua, na hilo hubadili rangi ya jua kwa kiwango fulani ikitegemea ni wakati gani. Kwa mfano, wakati wa adhuhuri, kwa kawaida jua huwa na rangi ya manjano nyangavu. Lakini wakati jua linapochomoza na wakati linapotua, huenda likaonekana kuwa na rangi ya machungwa au hata rangi nyekundu. Mabadiliko hayo husababishwa na molekuli za gesi, mvuke wa maji, na chembechembe ndogo katika angahewa ya dunia.

Kwa sababu ya vitu vinavyofanyiza angahewa, mwangaza wa jua wa bluu na urujuani hutawanywa na kutokeza anga maridadi la bluu kwenye siku isiyo na mawingu. Kwa kuwa rangi ya bluu na urujuani zimetawanywa kwa njia hiyo, mwangaza wa jua unaoonekana adhuhuri huwa wa rangi ya manjano. Lakini wakati jua linapokuwa chini kabisa kwenye upeo, mwangaza wake hupenya kwenye angahewa kupitia pembe kali kabla ya kutufikia. Kwa sababu hiyo, mwangaza wa jua hupitia sehemu kubwa ya angahewa ambayo hutawanya zaidi rangi ya bluu na kijani. Hivyo, jua linapotua, huenda likaonekana kuwa na rangi nyekundu nyangavu au nyekundu iliyoiva.

Anga la Usiku Lenye Rangi Nyingi

Uwezo wa macho yetu huathiri sana jinsi tunavyoona anga wakati wa usiku. Macho yetu hupokea mwangaza kupitia aina mbili za chembe—cone na rod. Chembe za cone huwezesha jicho kutofautisha rangi mbalimbali, lakini huacha kufanya kazi kunapokuwa na mwangaza hafifu. Kwa upande mwingine, ingawa rod hazitofautishi rangi, zinapokea mwangaza kwa njia nzuri zaidi. Kwa kweli, chini ya hali zinazofaa zaidi, rod inaweza kutambua fotoni moja au chembe hafifu sana ya mwangaza! Chembe zetu za rod zinakuwa na uwezo mzuri wa kuona zinapoelekezwa kwenye mawimbi mafupi ya mwangaza yanayopatikana upande wa rangi ya bluu katika spektra ya rangi. Kwa sababu hiyo, tunapotazama nyota zenye mwangaza hafifu, huenda tukaona zile za bluu na si zile nyekundu. Jambo la kupendeza ni kwamba kuna vifaa ambavyo hutusaidia kuona vitu ambavyo macho yetu hayawezi kuona.

Darubini huongeza uwezo wetu wa kuona vitu vilivyo mbali angani wakati wa usiku kama vile nyota, vikundi vya nyota, nyotamkia, na mawingu yenye kujiviringa. Hata hivyo, uwezo wetu wa kuona unaathiriwa kwa kiasi fulani na angahewa. Jambo hilo limetatuliwa na Darubini ya Angani ya Hubble, au HST, inayozunguka dunia. Chombo hicho kilichotengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu kinaweza kuona vitu vilivyo na mwangaza hafifu sana ambavyo hatuwezi kuona kwa macho yetu! Darubini hiyo imepiga picha maridadi sana za vitu vilivyo mbali sana angani, kutia ndani makundi ya nyota, mawingu ya vumbi na gesi yanayoitwa nebulae.

Lakini sasa kuna darubini mpya ambazo ni bora na zinapita uwezo wa HST kwa njia fulani. Kwa mfano, darubini hizo zina uwezo wa kurekebisha picha zilizopotoshwa kwa sababu ya msukosuko wa angahewa na hivyo kuwezesha wataalamu wa nyota kuona picha safi sana kuliko zile zilizopigwa kwa darubini ya Hubble. Mfano mmoja ni Kituo cha Kuchunguza Nyota na Sayari cha W. M. Keck katika kisiwa cha Hawaii, ambacho kina darubini inayotiwa Keck I, mojawapo ya darubini kubwa zaidi ulimwenguni. Kwa kutumia darubini hiyo, mtaalamu wa nyota, Peter Tuthill, wa Chuo Kikuu cha Sydney, Australia, aligundua mawingu ya vumbi yaliyotoka kwenye mfumo wa nyota mbili zilizokuwa zikizunguka katika kundi la nyota la Mshale (Sagittarius), ambalo kulingana na maoni yetu linaonekana kuwa karibu na kitovu cha kikundi chetu cha nyota kinachoitwa Kilimia.

Kadiri wataalamu wa nyota wanavyotazama mbali angani, ndivyo wanavyopata nyota na makundi zaidi ya nyota. Kuna nyota ngapi angani? Tunaweza kukisia tu. Lakini Muumba wetu, Yehova Mungu hahitaji kukisia. “Anahesabu idadi ya nyota; zote anaziita kwa majina yake,” inasema Zaburi 147:4.

Nabii Isaya alisema maneno kama hayo. Alieleza mengi zaidi ya hayo kwa kusema kwa usahihi wa kisayansi kwamba anga letu limetokezwa kwa nguvu za Mungu zisizo na kifani. “Inueni macho yenu juu, mwone,” akaandika Isaya. “Ni nani ameviumba vitu hivi? Ni Yeye anayelileta jeshi lake kulingana na hesabu, ambaye zote anaziita kwa jina. Kutokana na wingi wa nguvu zenye msukumo, yeye pia akiwa hodari katika nguvu, hakuna hata moja kati ya hizo inayokosekana.”​—Isaya 40:26.

Isaya ambaye aliishi miaka 2,700 hivi iliyopita, alijuaje kwamba ulimwengu ulitokana na nguvu za Mungu zisizo na kifani? Kwa kweli, hakukugundua jambo hilo yeye mwenyewe! Badala yake, aliandika yale ambayo roho ya Yehova ilimwongoza kuandika. (2 Timotheo 3:16) Kwa hiyo, yeye pamoja na waandikaji wengine wa Biblia walifanya jambo ambalo hakuna vitabu vya kisayansi au darubini inaweza kufanya. Walimtambulisha Yule ambaye huzipa nyota uzuri na utukufu wake.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 16]

KWA NINI NYOTA HUMETAMETA?

Nyota humetameta, au huonekana ni kana kwamba zinabadili mnga’o na mahali zilipo, kwa sababu ya msukosuko katika angahewa la dunia. Ili kuelewa jambo hilo, wazia madoa madogo ya nuru kwenye sakafu ya kidimbwi cha kuogelea. Inakuwaje wakati mawimbi madogo yanapopita juu ya nuru hiyo? Yanametameta kama nyota zinavyofanya. Hata hivyo, nuru kubwa haziwezi kumetameta kwa njia hiyo. Sayari ni kama nuru hizo kubwa, si kwa sababu ni kubwa kuliko nyota, bali kwa sababu ziko karibu zaidi na dunia na kwa hiyo zinaonekana kuwa kubwa.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 17]

RANGI: HALISI AU BANDIA?

Huenda umeona picha maridadi zenye rangi za makundi ya nyota, nebulae, na nyota zilizopigwa kwa kutumia Darubini ya Angani ya Hubble (HST). Lakini je, rangi hizo ni halisi? Kusema kweli, rangi hizo zimetokezwa upya kwa kutumia utaalamu wa kisanii na kisayansi. Picha zinazopigwa kwa kutumia HST hazina rangi na zinapitishwa kwenye vifaa vinavyochuja rangi. Wataalamu wa nyota na wataalamu wa picha hutumia teknolojia ya kisasa na mifumo ya kompyuta kutokeza picha tunazoona, na nyakati nyingine wanatokeza rangi ambazo wanaamini zinakaribia kabisa rangi za asili za vitu vya angani. * Nyakati nyingine wataalamu wa nyota hutokeza picha zenye rangi bandia kimakusudi ili vitu fulani vionekane wazi zaidi ili vifanyiwe uchunguzi wa kisayansi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 21 Tunapotumia darubini kutazama vitu vilivyo na mwangaza hafifu kwenye anga la usiku, chembe zetu za cone hazifanyi kazi, kwa hiyo tunaona kwa kutumia chembe za rod pekee, ambazo haziwezi kutambua rangi.

[Picha]

Bila rangi

Nyekundu

Kijani

Bluu

Picha inayotokezwa baada ya kuchanganya rangi zote tatu

[Hisani]

J. Hester and P. Scowen (AZ State Univ.), NASA

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nyota inayoitwa V838 “Monocerotis”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Makundi ya nyota yaliyochangamana Arp 273

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

NASA, ESA, and the Hubble Heritage (STScI/AURA) -ESA/Hubble Collaboration

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

V838: NASA, ESA, and H. Bond (STScI); Arp 273: NASA, ESA, and the Hubble Heritage Team (STScI/AURA)