Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Unapenda Kula Uyoga?

Je, Unapenda Kula Uyoga?

Je, Unapenda Kula Uyoga?

KATIKA Misri ya kale, Mafarao waliona uyoga kuwa mlo mtamu sana. Chakula hicho kikaja kuonwa kuwa kinastahili kuliwa tu na familia ya kifalme. Waroma walisema kwamba uyoga ni chakula cha miungu na ni wakati wa matukio muhimu tu ambapo walikula uyoga. Wagiriki wa kale waliamini kwamba uyoga uliwafanya wapiganaji wao wawe na nguvu kwa ajili ya vita.

Hata hivyo, leo uyoga si chakula cha watu wenye cheo kikubwa tu. Watu ulimwenguni pote hufurahia kula uyoga! Namna gani wewe? Ikiwa unapenda kula uyoga, je unajua unachokula? Je, uyoga ni mnyama, mboga, au kitu kingine? Uyoga hukuzwaje? Je, ni chakula chenye lishe? Na ukiona uyoga wa mwituni, unapaswa kufanya nini?

Mimi na mke wangu tulisafiri kutoka Sydney, Australia hadi kwenye mji maridadi wa Mittagong, kwenye nyanda za juu za New South Wales, ili kupata majibu ya maswali hayo. Tuliyapata wapi? Katika shamba la uyoga la Noel Arrold.

Kukuza Uyoga

Noel, Mwaustralia aliye na mwili mkubwa, ni mtaalamu wa biolojia na mkulima stadi wa uyoga. Alichunguza jinsi uyoga unavyokuzwa katika nchi kadhaa kabla ya kurudi Australia ili akazikuze kwa ajili ya biashara. “Uyoga ni kuvu, jamii ya viumbe vinavyotia ndani ukungu,” anaeleza. “Hapo awali wanabiolojia walifikiri kwamba kuvu ni mimea, lakini sasa tunafahamu kwamba kuvu ni tofauti sana na mimea.

“Kwa mfano, kuvu hazitokezi chakula chao kupitia usanidi-mwanga kama mimea mingine inavyofanya. Kuvu zinaweza kukua gizani. Miili ya kuvu hutokeza vimeng’enya vyenye nguvu ambavyo hubadili mbolea kuwa virutubisho vya msingi, na kuvifyonza kama chakula. Utaratibu huo wa kipekee wa kumeng’enya hufanya kuvu kuwa tofauti na wanyama. Kwa kuwa kuvu si mimea na si wanyama, sasa wanabiolojia wanaweka kuvu katika kikundi cha pekee—himaya ya kuvu.”

“Mwituni, uyoga uliokomaa hutokeza mamilioni ya chembe ndogo sana ambazo huchangamana na chembe za uyoga mwingine na kukua,” Noel anaendelea. “Chembe hizo . . . zinapotua katika eneo lenye unyevu na lililo na chakula kingi, zinaweza kukua. Watu wanaokuza uyoga kwa ajili ya biashara wanajaribu kufanya hivyo chini ya hali zilizodhibitiwa ili kuongeza kiasi cha uzalishaji na ubora wa uyoga unaotokezwa.”

Tunapoendelea na matembezi yetu, Noel anaeleza kwamba kila aina ya uyoga huhitaji hali za kipekee ili kukua. Kwa mfano, uyoga ulio na rangi nyeupe, au button, ndiyo aina maarufu zaidi ya uyoga, na hukuzwa vizuri zaidi kwa kutumia mbolea. Aina nyingine hukua vizuri zinapotiwa katika mifuko iliyo na mimea iliyooza, katika chupa zilizojaa nafaka, juu ya magogo ya miti, au juu ya unga wa mbao ulioshindiliwa. Kati ya maelfu ya aina za uyoga zinazojulikana, ni aina 60 hivi tu zinazokuzwa kwa ajili ya biashara.

Noel hukuza uyoga katika eneo fulani la reli ya zamani inayopita chini ya ardhi karibu na Mittagong. Anatuambia hivi: “Hili ni eneo lenye baridi, unyevu, na linafaa kabisa kwa ajili ya kukuza uyoga.” Tukiwa hapo tunaona mifuko, vyungu, na chupa zilizojaa maelfu ya uyoga zilizo na maumbo na ukubwa tofauti-tofauti. Aina fulani zinatukumbusha waridi; nyingine zinafanana na mayungiyungi au mpangilio maridadi wa maua au miavuli mifupi minene. Mandhari hiyo yenye kuvutia ilikuwa yenye kupendeza sana!

Tamu na Inafaa na Milo Mingi

“Watu wengi wanapenda uyoga lakini huenda wasijue jinsi ya kutayarisha mlo wa uyoga,” anasema Noel. “Hata hivyo, ni rahisi kupika. Watu fulani hukatakata uyoga ili wale pamoja na vyakula vya kukaanga, mchuzi, na saladi, au wanapika uyoga ukiwa mzima. Mimi binafsi hufurahia kula uyoga aina ya oyster ulionyunyizwa chembechembe za mkate na kukaangwa kwa mafuta. Uyoga unaoitwa shiitake una ladha kama ya nyama na ni tamu unapoliwa pamoja na mayai yaliyokaangwa.”

Uyoga ni chakula chenye lishe na mtu anaweza kupata protini, nyuzinyuzi, madini, na vitamini nyingi. Aina 2,000 hivi zinajulikana kuwa na faida za kitiba. Kulingana na makala moja ya kitiba, madini yanayotolewa katika uyoga yana matumizi zaidi ya 100 ya kitiba, kutia ndani kutibu kansa, mchochota wa ini, UKIMWI, ugonjwa wa Alzheimer, na kiwango cha juu cha kolesteroli.

Hata hivyo, inaweza kuwa hatari sana kula uyoga wa mwituni. Aina fulani za uyoga kutia ndani ule unaoitwa death cap (Amanita phalloides), unafanana sana na aina zinazoweza kuliwa, lakini ni hatari sana. Kwa hiyo, hakikisha kwamba unakumbuka jambo hili: Usile uyoga mwituni isipokuwa mtaalamu wa uyoga anakuambia ni sawa kufanya hivyo! Bila shaka, aina za uyoga zinazokuzwa kwa ajili ya biashara zinaweza kuliwa. Ni chakula kitamu ambacho wakati fulani kililiwa tu na familia za kifalme!

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

USHIRIKIANO KATI YA UYOGA NA VITU VYA ASILI

Uyoga wa mwituni hukua katika misitu yenye baridi, unyevu, na giza, ambako inageuza miti iliyokufa, mimea, na samadi ya wanyama kuwa udongo wenye mbolea nyingi. Uyoga mwingine hushirikiana pamoja na miti. Uyoga hufaidika kutokana na mbolea inayotolewa na mizizi ya mti, huku mti ukipata virutubisho vinavyofyonzwa na uyoga.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

MAMBO UNAYOPASWA KUJUA KUHUSU UYOGA

• Hifadhi uyoga katika karatasi ya plastiki au mfuko ndani ya friji. Usiziweke karibu na vitu vilivyo na harufu kali kwa kuwa uyoga hufyonza harufu.

• Ikiwa utakula uyoga zikiwa mbichi, pangusa kwa kutumia kitambaa kilicho na unyevu au uzimiminie maji upesi na kuzipangusa kwa kitambaa kikavu. Usiache uyoga zilowe maji.

• Unapopika uyoga, tumia brashi laini kuondoa uchafu wowote ulio juu.

• Usiambue ngozi ya uyoga—ngozi yake ni tamu na ina lishe.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Uyoga unakuzwa katika chumba hiki ambacho kiwango cha joto kimedhibitiwa

[Picha katika ukurasa wa 22]

Aina fulani za uyoga zinafanana na maua maridadi

[Picha katika ukurasa wa 23]

Uyoga pamoja na “hummus,” spinachi, vitunguu saumu, na vitunguu vya majani

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Courtesy of the Mushroom Information Center

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Top: Courtesy of the Mushroom Information Center; bottom: Courtesy of the Australian Mushroom Growers Association