Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Tangu mwaka wa 1862 “rekodi zilipoanza kuwekwa, ndoa zinapungua kwa kiwango kikubwa sana nchini Uingereza na Wales.”​—SHIRIKA LA TAKWIMU ZA KITAIFA, UINGEREZA.

Zaidi ya nusu ya wasimamizi wa makampuni madogo ya kibinafsi huko Marekani “wanashuku kwamba wafanyakazi wao wataiba kitu fulani chenye thamani [kutoka kwa kampuni] katika kipindi cha mwaka utakaofuata.”​—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, MAREKANI.

Mwaka ulikuwa haujaisha tangu wenye mamlaka nchini China walipoanza “kampeni” ya kufunga vituo vya ponografia na tayari “walikuwa wamefunga vituo zaidi ya 60,000 vya ponografia,” kiliripoti Kitengo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ponografia na Vichapo Visivyo halali.​—CHINA DAILY, CHINA.

“Zaidi ya watu milioni 215​—au asilimia 3 ya idadi ya watu duniani​—sasa [wanaishi] nje ya nchi walimozaliwa.”​—HAZINA YA KIMATAIFA YA MAENDELEO YA KILIMO YA UMOJA WA MATAIFA, ITALIA.

“Kati ya wanafunzi 19 wanaojiua kila siku huko India, sita kati yao [hufanya hivyo] kwa sababu ya kuogopa kuanguka mitihani.”​—INDIA TODAY INTERNATIONAL, INDIA.

Mbinu ya Kuwanasa Wachezaji wa Kamari

Kwa wastani, mtu mwenye uraibu wa kucheza kamari nchini Ujerumani hupoteza fedha mara kumi zaidi ya yule ambaye hana uraibu huo. Kwa hiyo, watu wenye uraibu wa kucheza ndio hasa “wateja muhimu katika biashara hiyo,” linasema jarida Süddeutsche Zeitung. Ili wapate faida kubwa, wenye biashara ya kamari huunda michezo na kubuni mashini zao kwa njia ambayo inachochea na kuendeleza uraibu. Kadiri mashini zinavyofanya kazi upesi, ndivyo mchezaji anavyoshindwa kujizuia na hivyo kuwa mraibu. Mbinu hizo za kupata wateja zinafanikiwa—inasemekana kwamba asilimia 56 ya mapato yanayotokana na mashini za kamari hutoka kwa watu wenye uraibu. Katika kasino, mbinu hizo hufaulu kwa asilimia 38; na asilimia 60 katika michezo ya Intaneti.

Wakati Mzuri wa Kumwona Hakimu

Je, mambo madogo yanaweza kuathiri maamuzi ya kihukumu? Utafiti mmoja unaonyesha yanaweza. Kundi la watafiti lilichanganua maamuzi zaidi ya 1,000 yaliyotolewa na mahakimu walio na uzoefu nchini Israel kwamba watu wapewe vifungo vya nje. Utafiti huo ulionyesha kwamba baada ya hakimu kula chakula cha mchana au vitafunio, asilimia 65 ya hukumu alizotoa zilikuwa nzuri na zilipungua hatua kwa hatua na kukaribia asilimia sufuri, halafu zikaongezeka kwa ghafula tena na kurudi asilimia 65 baada ya kipindi cha mapumziko kilichofuata. Watafiti walifikia mkataa kwamba si kila mara hukumu hutegemea ukweli wa mambo wala sheria bali “inaweza kupotoshwa na mambo mengine ambayo hayapaswi kuathiri maamuzi ya kisheria.”