Tatizo la Hasira
Tatizo la Hasira
Mwanamume mmoja aliyeagiza sandwichi (vipande vya mkate vyenye jibini, nyama na vitu vingine katikati) katika mkahawa mmoja alipandwa na ghadhabu alipoona kwamba chakula chake kimechukua muda mrefu. Aliingia kwenye mkahawa huo, akamtisha mfanyakazi mmoja, akamsukuma kwenye meza, na kumpiga kofi. Kisha mwanamume huyo mwenye hasira akachukua mkate wake na kuondoka.
SISI sote hukasirika mara kwa mara. Hasira ni sehemu ya hisia zetu kama vile tu upendo, tumaini, wasiwasi, huzuni, na woga. Hasira iliyodhibitiwa inaweza kuonyeshwa kwa njia inayofaa na inaweza kuwa na faida. Kwa mfano, hasira inaweza kuwa na faida ikiwa itamfanya mtu aazimie kushinda vizuizi au matatizo fulani.
Kama kisa kilicho hapo juu kinavyoonyesha, hasira ina madhara pia. Watu fulani hupandwa na hasira kali haraka na mara nyingi zaidi kuliko wengine. Wanapochokozwa, huenda wakafoka au kumshambulia mtu. Kwa kufanya hivyo, hasira yao inawadhibiti, badala ya wao kuidhibiti. Mtu ambaye hawezi kudhibiti hasira yake husemwa kuwa “anachemka kwa hasira,” na kufanya hivyo ni hatari. *
Watu wenye matatizo ya hasira hujiumiza wenyewe na wengine pia. Mtu mwenye tatizo la hasira anaweza kulipuka kwa hasira kwa sababu ya mambo madogo sana na kutenda kwa jeuri, na hilo linaweza kutokeza madhara. Fikiria mifano ifuatayo:
Mwanamume mmoja aliyekuwa akitembea pamoja na rafiki zake barabarani alipigwa risasi shingoni wakati mmoja wa rafiki zake alipomgonga mtu fulani kimakosa kwa mkoba aliokuwa amebeba.
Mwanamume mwenye umri wa miaka 19 alimpiga na kumwua mtoto wa miezi 11 wa mchumba wake. Mwanamume huyo alikuwa akicheza mchezo wa video wenye jeuri alipopandwa na hasira kwa sababu mtoto alishika kibonyezo fulani na kufanya mwanamume huyo ashindwe katika mchezo huo.
Ripoti kama hizo kutoka sehemu zote ulimwenguni zinaonyesha kwamba idadi ya watu wenye matatizo ya hasira inaongezeka. Kwa nini idadi hiyo inaongezeka?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Broshua Boiling Point—Problem Anger and What We Can Do About It inasema kwamba mtu “anayechemka kwa hasira” anakabiliana kwa njia isiyofaa na hasira na hilo linaweza kusababisha matatizo yenye kuendelea katika maisha yake kutia ndani kufikiri kwake, hisia, tabia, na mahusiano yake na watu wengine.
[Sanduku katika ukurasa wa 3]
Hasira ni moja kati ya hisia zetu za kawaida. Kwa hiyo, nyakati nyingine kuonyesha hasira iliyodhibitiwa kunafaa. Hata hivyo, makala hizi zinazungumzia hasira isiyofaa inayoweza kutudhuru sisi na wengine kihisia, kimwili, na kiroho.