Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tunda la Manjano la Armenia

Tunda la Manjano la Armenia

Tunda la Manjano la Armenia

● Matunda ya aprikoti yamekuzwa kwa maelfu ya miaka barani Asia na Ulaya. Wazungu waliamini kwamba kiasili tunda la aprikoti lilitoka nchini Armenia na ndiyo sababu wakaanza kuliita tofaa la Armenia.

Kufikia sasa, karibu aina 50 tofauti-tofauti za aprikoti hukuzwa huko Armenia. Matunda hayo huwa tayari kuvunwa katikati ya Juni hadi mwisho wa Agosti. Mchanga wenye rutuba wa volkano na jua la kutosha huko Armenia hufanya matunda ya aprikoti yawe na utamu wa pekee ambao hufanya watu wengi waseme kuwa ndiyo matamu zaidi ulimwenguni.

Aina zinazojulikana zaidi za matunda hayo huwa na ukubwa sawa na plamu ndogo na yanaweza kuwa na rangi ya dhahabu nyangavu au rangi nzito ya machungwa. Maganda yake ni kama mahameli na nyama yake ni ngumu, haina umajimaji mwingi, na inaweza kuwa tamu au chungu. Wengi wamesema kuwa aprikoti huwa na ladha inayofanana na ile ya pichi na plamu.

Wakulima wa aprikoti wametokeza aina “nyeusi” ya tunda hilo lakini si aprikoti halisi. Badala yake, ni aprikoti iliyopandikizwa kwenye plamu. Tunda hilo lina rangi iliyoiva ya zambarau—karibu na nyeusi—ngozi ngumu na nyama ya rangi ya manjano.

Kabla ya kuchipusha majani, mti wa aprikoti huchanua maua meupe yenye harufu nzuri, yanayojichavusha yenyewe. Maua yake hufanana na yale ya miti ya pichi, ya plamu, na ya cheri. Kwa ujumla, miti hiyo husitawi katika maeneo yenye baridi kali na pia joto kiasi, kwa kuwa inahitaji kipindi cha baridi kali ili ichanue maua na kuzaa vizuri. Basi hali ya hewa ya Armenia inafaa kabisa!

Matunda ya aprikoti ambayo hayajakaushwa yana manufaa mengi kwa afya. Kwa mfano, matunda hayo ni chanzo bora cha beta-carotene na vitamini C. Watu wengi wanajua matunda ya aprikoti ambayo yamekaushwa. Hiyo ni kwa sababu yanapochunwa yanaweza kupondeka kwa urahisi na kuoza haraka. Ndiyo sababu katika sehemu fulani za dunia, ni rahisi kupata matunda ya aprikoti yaliyokaushwa kuliko yale ambayo hayajakaushwa. Jambo linalopendeza ni kwamba hata matunda ya aprikoti yaliyokaushwa yana madini mengi na huongeza nyuzinyuzi na madini ya chuma mwilini. Kwa kuongezea, yanaweza kutumiwa kutengeneza kileo cha brandi, jemu, au maji ya matunda.

Kwa kuongezea, miti ya aprikoti hutumiwa kutengeneza michongo maridadi ya vitu vya mbao na pia inatumiwa kutengeneza duduk, zumari maarufu nchini Armenia, ambayo nyakati nyingine huitwa zumari ya aprikoti. Kwenye maduka na masoko katika eneo la Yerevan, mji mkuu wa Armenia, watalii wanaweza kupata michongo ya kuwasaidia kukumbuka eneo hilo iliyochongwa kutokana na mti wa aprikoti.

Ikiwa unaishi katika eneo la dunia ambako unaweza kupata matunda ya aprikoti ambayo hayajakaushwa, kwa nini usiyaonje? Bila shaka utafurahia tunda hilo tamu lenye rangi ya manjano.