Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mkonga wa Tembo

Mkonga wa Tembo

Je, Ni Kazi Ya Ubuni?

Mkonga wa Tembo

● Watafiti wanatengeneza mkono wa roboti ulio mwepesi na unaoweza kunyumbulika kwa urahisi. Msimamizi wa idara ya ubuni katika kampuni inayotengeneza mkono huo anasema kwamba mkono huo mpya “hauwezi kulinganishwa na chochote kinachotumika viwandani.” Walitoa wapi wazo hilo? Msimamizi huyo anasema, “Tuliiga jinsi mkonga wa tembo unavyofanya kazi.”

Fikiria hili: Mkonga huo wa tembo wenye uzito wa karibu kilo 140 unasemekana kuwa “ndicho kiungo muhimu na chenye matumizi mengi zaidi duniani.” Kiungo hicho chenye matumizi mengi hutumiwa kama pua, mrija, mkono, au kiganja. Kwa kutumia mkonga huo, tembo anaweza kupumua, kunusa, kunywa, kukamata, au hata kupiga kelele kama ya tarumbeta inayoumiza masikio!

Lakini si hayo tu. Mkonga wa tembo una nyuzinyuzi 40,000 za misuli zinazouwezesha kujipinda kuelekea upande wowote ule. Tembo anaweza kuinua sarafu ndogo kwa kutumia ncha ya mkonga wake. Wakati huohuo, tembo anaweza kutumia mkonga wake kuinua vitu vyenye uzito wa kilo 270 hivi!

Watafiti wanatumaini kwamba kuiga uwezo wa mkonga wa tembo kutawawezesha kutokeza roboti zenye uwezo mkubwa zaidi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani. “Tumebuni roboti mpya kabisa ya kuwasaidia wanadamu,” anasema mwakilishi wa kampuni iliyotajwa awali, “roboti ambayo kwa mara ya kwanza itawawezesha wanadamu kufanya kazi pamoja na mashine kwa njia nzuri na bila hatari yoyote.”

Una maoni gani? Je, mkonga wa tembo ulitokezwa na mageuzi? Au ulibuniwa?