Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wataalamu wa Nyota wa Enzi za Kati

Wataalamu wa Nyota wa Enzi za Kati

Wataalamu wa Nyota wa Enzi za Kati

KATIKA muda wote wa historia watu wamepigwa na butwaa wanapotazama jua, mwezi, na nyota. Kwa kuchunguza mahali ambapo vitu hivyo vya angani vipo na jinsi vinavyosonga, watu wameweza kutambua jinsi siku, miezi, na miaka inavyosonga.

Waarabu walikuwa kati ya watu wengi waliochunguza anga la usiku. Kipindi cha usitawi wa sayansi katika Mashariki ya Kati kilianza katika karne ya tisa W.K., na wataalamu wa nyota wenye kuzungumza Kiarabu katika enzi hiyo walionwa kuwa magwiji wa elimu ya nyota. Mambo waliyovumbua yalisaidia sana katika kusitawi kwa elimu hiyo yenye kuvutia. Acheni tuone jinsi hilo lilivyotukia.

Waanzilishi wa Elimu ya Nyota

Katika karne ya saba na ya nane W.K., Uislamu ulienea kutoka Arabia kuelekea Afrika Kaskazini, Hispania, na pia kuelekea upande wa mashariki kufikia Afghanistan. Wasomi katika eneo hilo lote waliiga mbinu za kufanya utafiti wa kisayansi zilizotumiwa huko Uajemi na Ugiriki, ambazo hasa zilikuwa zimeathiriwa na mbinu za Babiloni na Misri.

Kisha, katika karne ya tisa, maandishi muhimu ya kisayansi yalitafsiriwa katika Kiarabu, kutia ndani maandishi ya Ptolemy, mtaalamu wa nyota aliyekuwa Mgiriki. * Watawala wa familia ya Abbasid, ambao milki yao ilienea kuanzia Afghanistan hadi Bahari ya Atlantiki, walipata maandishi ya Kisanskriti kutoka India ambayo yalikuwa na habari nyingi sana kuhusu hisabati, elimu ya nyota, na nyanja nyingine za kisayansi.

Waislamu waliiona elimu ya nyota kuwa yenye thamani sana. Kwa nini? Sababu moja ilihusiana na ibada yao. Waislamu wanaamini kwamba wanapaswa kutazama upande wa Mecca wanaposali, na wataalamu wa nyota wangeweza kufahamu upande ambao Mecca iko wakiwa mahali popote. Kufikia karne ya 13, misikiti fulani iliwaajiri wataalamu wa nyota, au muwaqqit, ambao waliwasaidia waabudu wao kusali kwa wakati ambao waliona kuwa inafaa. Wakiwa na habari hiyo, wataalamu hao wa nyota wangeweza pia kutambua tarehe za sherehe na desturi za kidini, kama vile kipindi cha kufunga wakati wa mwezi wa Ramadhani. Isitoshe, wangeweza kuwasaidia watu wanaoelekea Mecca ili kuhiji wajue safari yao ingechukua muda gani na ni njia gani ambayo ingewafaa zaidi.

Ufadhili wa Serikali

Kufikia mapema katika karne ya tisa, kila msomi huko Baghdad alipaswa kusomea elimu ya nyota. Khalifa al-Ma’mūn alianzisha kituo cha kuchunguza vitu vya angani katika jiji hilo, kisha akajenga kingine karibu na Damasko. Wanajiografia na wanahisabati wake walichanganua, wakalinganisha, na kupatanisha habari waliyopokea kutoka kwa wataalamu wa nyota wa Uajemi, India, na Ugiriki. Vituo vya kuchunguza vitu vya angani vilijengwa pia katika majiji mengine ya Mashariki ya Kati. *

Wasomi waliofanya kazi ya katika vituo hivyo walipata matokeo mazuri ikilinganishwa na jinsi hali zilivyokuwa wakati huo. Kwa mfano, mapema katika 1031, Abu Rayhan al-Bīrūnī alisema kuhusu uwezekano wa kwamba sayari hufuata njia yenye umbo la yai zinapozunguka, badala ya kuzunguka katika njia ya mviringo.

Kuipima Dunia

Kuenea kwa Uislamu kulichochea upendezi katika kutokeza ramani na usafiri wa baharini. Wachoraji wa ramani walijitahidi sana kuchora ramani sahihi zaidi, na mara nyingi walifaulu. Akiwa na lengo la kupima kwa usahihi zaidi digrii za latitudo za ramani ya dunia aliyokuwa akitokeza, khalifa al-Ma’mūn alituma vikundi viwili vya wachunguzi katika jangwa la Siria. Wakiwa na vifaa vya kuchunguza latitudo, kila kikundi kilielekea upande wake hadi kilipoona Nyota ya Kaskazini ikiwa imeanguka au imeinuka kwa digrii moja. Walifikia mkataa kwamba umbali ambao wamesafiri unalingana na digrii moja ya latitudo, au 1/360 ya mzingo wa dunia. Walipima mzingo wa dunia kuwa ni kilomita 37,369​—na tarakimu hiyo inakaribiana sana na ile sahihi ya kilomita 40,008!

Vituo vya kuchunguza vitu vya angani vilivyokuwa huko Mashariki ya Kati vilikuwa na vifaa vya hali ya juu​—vyombo vya kuchunguza latitudo kwa kutegemea mahali jua, mwezi, sayari nyingine, na nyota zilipokuwa (astrolabe), vyombo vya kupimia pembe za kimo (quadrant), vyombo vinavyopima umbali wa jua au nyota kutoka kwenye upeo wa macho (sextant), saa za kivuli (sundial), na vifaa vingine vya kuchunguza na kupima vitu angani. Baadhi ya vifaa hivyo vilikuwa vikubwa sana. Wajenzi wa vifaa hivyo walijiambia kwamba ikiwa kifaa ni kikubwa basi kitapima kwa usahihi zaidi.

Matokeo ya Kazi ya Wataalamu wa Nyota wa Kale

Magwiji hao wa elimu ya nyota walitimiza mambo yenye kustaajabisha. Waliyapatia makundi ya nyota majina na kuandika wakati yaliyopoonekana, wakapatia nyota majina, wakatokeza kalenda sahihi zaidi, wakapima wakati wa kupatwa kwa jua, na wakaendelea kusahihisha chati zilizokuwa zikionyesha mwendo wa vitu vya angani. Wakati wowote, iwe mchana au usiku, wangeweza kutambua mahali ambapo jua, mwezi, na sayari tano zinazoweza kuonekana zilikuwa—ujuzi wenye manufaa sana katika usafiri wa baharini. Wangeweza pia kujua wakati na kufahamu tarehe kwa kutazama mahali ambapo vitu vya angani vilikuwa.

Nadharia ambazo wataalamu wa nyota wenye kuzungumza Kiarabu walivumbua ili kueleza jinsi sayari zinavyosonga zilikuwa karibu sana kurekebisha kasoro zilizokuwapo katika mfano wa ulimwengu ambao Ptolemy alitengeneza. Kasoro yao ilikuwa kwamba walifikiri sayari zote ziliizunguka dunia badala ya kulizunguka jua. Hata hivyo, walieleza kwa usahihi sana jinsi nyota husonga, na mambo waliyovumbua yalisaidia sana vizazi vilivyofuata vya wataalamu wa nyota ulimwenguni.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Tayari Wagiriki walikuwa wamevumbua kwamba dunia ni mviringo. Walijiambia, ikiwa dunia si mviringo inakuwaje kwamba mtu anaposafiri kuelekea kusini, ile Nyota ya Kaskazini huonekana ikiwa chini angani?

^ fu. 9 Mara nyingi, ujenzi wa vituo hivyo vya kuchunguza vitu vya angani ulitegemea ikiwa mtawala alipendezwa na elimu ya nyota.

[Blabu katika ukurasa wa 17]

Wataalamu wa nyota walirekodi jinsi sayari zinavyosonga katika vitabu vya kila mwaka vilivyoandikwa katika nchi za Kiislamu

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 19]

“KOMPYUTA YA MFUKONI” YA ZAMANI

Astrolabe, ambayo ilibuniwa kabla ya sextant, imesemekana kuwa “kifaa muhimu zaidi katika elimu ya nyota kabla ya darubini kubuniwa.” Wanasayansi wa Enzi za Kati huko Mashariki ya Kati walitumia kifaa hicho kufanya hesabu zilizohusiana na wakati na mahali ambapo vitu vya angani vilikuwa.

Kifaa hicho kilikuwa na mfano wenye kuvutia wa anga likiwa limechorwa kwenye bati la chuma lililong’arishwa. Digrii, au nyakati nyingine saa za siku, ziliandikwa kwenye kiunzi chake cha nje kilichoshikilia bati hilo. Kishale kinachoitwa alidade kilitumiwa kuonyesha mwinuko wa nyota fulani hususa astrolabe ilipoinuliwa. Matokeo yake yalisomwa kwenye kifaa kilicho kama rula.

Kifaa hicho kinachoitwa astrolabe kilitumiwa kutambulisha nyota, kutambua wakati ambapo jua lingechomoza na kutua siku yoyote ile, kutambua upande ambao Mecca ilikuwa, kupima nchi, kupima kimo cha vitu, na kusaidia katika usafiri wa baharini. Ilikuwa “kompyuta ya mfukoni” ya nyakati za kale.

[Picha]

“Astrolabe” ya karne ya 13

Robo ya “astrolabe” ya karne ya 14

[Hisani]

Astrolabe: Erich Lessing/Art Resource, NY; astrolabe quadrant: © New York Public Library/​Photo Researchers, Inc

[Picha katika ukurasa wa 16]

Picha ya karne ya 16 ikionyesha wataalamu wa nyota wa milki ya kale ya Uturuki wakitumia mbinu zilizoanzishwa na Waarabu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Tufe linaloonyesha vitu vya angani, 1285 W.K.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kurasa kutoka kwenye maandishi ya Kiarabu kuhusu makundi ya nyota, yaliyoandikwa na mtaalamu wa nyota ‘Abd al-Raḥmān al-Sufi, karibu 965 W.K.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Pages 16 and 17: Art Resource, NY

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Manuscript: By permission of the British Library; globe: © The Bridgeman Art Library