“Hiyo Ni Pua ya Ajabu!”
“Hiyo Ni Pua ya Ajabu!”
HIVYO ndivyo mara nyingi watu husema wanapoona pua kubwa, inayoning’inia ya tumbili wa kiume anayeitwa proboscis. * Pua ya tumbili fulani wa kiume inaweza kufikia urefu wa sentimita 18—karibu robo ya urefu wa mwili wake. Kwa kuwa pua hiyo hufunika mdomo na kidevu chake, lazima aisukume kando anapokula! Ikiwa ungekuwa na pua kama hiyo, ingening’inia hadi katikati ya kifua chako.
Pua ya tumbili huyo wa kiume ina faida gani? * Watu hutoa maoni tofauti-tofauti. Labda pua yake husaidia kuondoa joto la ziada mwilini au inasaidia kuongeza uzito wa sauti yake. Au huenda ikatoa onyo kwa tumbili wengine wa kiume wa jamii hiyo. Kusema kweli, pua ya tumbili huyo wa kiume aliyekomaa anayesimamia kikundi fulani huvimba na kuwa nyekundu anapokasirika au kusisimka. Huenda pia ikawa kwamba pua yake inahusika katika kuwavutia tumbili wa kike! Hata hivyo, huenda pua hiyo ikawa inatimiza makusudi mengi, labda hata inafanya mambo fulani ambayo hatujui mengi kuyahusu.
Tumbo Kubwa
Tumbili hao wa kiume na wa kike wanatambuliwa pia kwa tumbo lao kubwa. Kwa kweli, huenda uzito wa tumbo lao ukawa robo ya uzito wa mnyama mwenyewe. Kwa sababu hiyo, sikuzote tumbili hao wa kiume na wa kike huonekana kana kwamba ni waja-wazito! Kwa nini wana tumbo kubwa hivyo?
Kama tumbo la ng’ombe, tumbo la tumbili hao limejaa umajimaji fulani ulio na mchanganyiko wa
majani na bakteria. Bakteria hizo huchachisha chakula na kuyeyusha wanga wenye nyuzinyuzi, kutia ndani sumu ya mimea fulani ambayo inaweza kuwaua wanyama wengine. Kwa sababu ya mfumo wao wa ajabu wa kumeng’enya, tumbili aina ya proboscis wanaweza kula majani na matunda yasiyo na sukari na mbegu za mikundekunde, mitende, na mimea mingine—vyakula ambavyo tumbili wengine walio na matumbo ya aina tofauti hawawezi kustahimili.Hata hivyo, mfumo wao wenye nguvu wa kumeng’enya una tatizo. Mnyama huyo hawezi kula matunda yenye sukari, kwa kuwa yatachacha upesi. Matunda hayo matamu hufanya tumbo la tumbili huyo livimbe, hivi kwamba hata anaweza kufa kifo chenye maumivu sana.
Kwa sababu ya kula vyakula vyenye wanga wenye nyuzinyuzi nyingi na tumbo lake lililo tata sana, tumbili wa proboscis anahitaji kutumia wakati mwingi sana kumeng’enya chakula chake. Kwa hiyo, baada ya kula kiamsha-kinywa, tumbili hao hulala—nyakati nyingine kwa saa nyingi—kabla ya kula tena.
Mnyama Anayeshirikiana na Wenzake
Iwe tumbili hao wanakula au kupumzika, mara nyingi wanakuwa katika kikundi. Proboscis wa kiume anayesimamia kikundi fulani huwa na tumbili wanane hivi wa kike na watoto katika familia yake. Watoto wa kiume hufukuzwa kutoka kwenye kikundi hicho wanapokuwa na umri wa kutosha kujitunza. Wao hujiunga na tumbili wengine wa kiume wenye umri kama wao, na kutembea katika vikundi ambavyo vinasimamiwa na tumbili mmoja au wawili wakubwa wa kiume. Kwa mtu asiye na uzoefu, huenda tumbili hao wa kiume wakaonekana kama familia ya tumbili wa kike wanaosimamiwa na tumbili mmoja wa kiume.
Tumbili hao wana tabia fulani ya ushirikiano isiyo ya kawaida—mara nyingi familia moja huchangamana na familia nyingine, hasa jioni wanapokutana mtoni. Wakati huo, tumbili wa kiume atajionyesha kwamba ana nguvu akihisi kwamba tumbili mwingine wa kiume anawaonyesha upendezi tumbili wa kike wa familia yake. Kwa kawaida, tumbili huyo wa kiume—ambaye huenda akawa na uzito wa kilo 20 hivi—anaweza kukunja miguu yake ya mbele na kuinama huku mdomo wake ukiwa wazi na kumkodolea macho mpinzani wake. “Ikiwa hatafanikiwa kumtisha mpinzani wake,” kitabu Proboscis Monkeys of Borneo kinasema, “tumbili huyo wa kiume ataruka kwenye miti ghafula na bila kutazamiwa, mara nyingi kwa kelele nyingi, na mara nyingi ataanguka juu ya matawi yaliyokauka ambayo yatavunjika kwa kelele nyingi na hivyo kuongezea kishindo chake.” Nyakati nyingine wao hupigana, lakini wao hufanya hivyo mara chache sana.
“Mbali na kuonekana kuwa na sura ya ajabu, tumbili wa proboscis hutoa sauti za ajabu sana,” kinasema kitabu kilichonukuliwa hapo juu. Wanyama hao hukoroma, hutoa mlio kama wa honi, hunguruma, na kupiga mayowe, hasa jioni wanapokutana karibu na mito. Kelele hizo zinapoendelea, tumbili wa kike wenye watoto huwalisha na kuosha nyuso za watoto wao bila kelele. Mwishowe, kufikia wakati ambapo msitu unaanza kuwa na giza, wanyama hao huwa wamejichagulia sehemu zenye starehe
kwenye miti—kwa kawaida juu ya miti mirefu karibu na mto—ambapo watalala.Tumbili Wenye Miguu Kama ya Bata
Mbali na pua, tumbili wa proboscis wana kiungo kingine cha ajabu—miguu yao ina utando kama ya bata kwa kadiri fulani. Miguu hiyo huwawezesha wanyama hao kuogelea na kutembea bila tatizo juu ya matope kwenye vinamasi. Bila shaka, vinamasi katika maeneo ya kitropiki huwa na mamba. Katika maeneo ambayo tumbili hao huishi kuna mamba wengi sana. Tumbili hao huepukaje kuliwa wanapoingia ndani ya maji?
Mbinu moja ambayo wao hutumia ni kuingia polepole ndani ya maji na kuogelea wakiwa wamepanga foleni bila hata kupiga maji kwa nguvu. Hata hivyo, mto unapokuwa mwembamba sana, wao hutumia mbinu tofauti. Wao hupanda juu sana kwenye mti, wanavuta kasi kutoka kwenye tawi fulani, huenda mita 9 hivi juu ya maji, na kuanguka juu ya maji kwa tumbo, kisha wanaogelea upesi kadiri wawezavyo kuvuka sehemu iliyosalia ya maji. Hata tumbili wa kike waliobeba watoto hutumia mbinu hiyo. Nyakati nyingine, familia nzima itaruka mara moja ndani ya maji na kuogelea upesi upande ule mwingine! Hata hivyo, adui yao mkuu si mamba.
Wanakabili Hatari ya Kutoweka
Tumbili wa proboscis wamewekwa kwenye orodha ya wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka na huenda kuna maelfu machache tu katika mazingira yao ya asili, na idadi hiyo inaendelea kupungua—hasa kwa sababu ya wanadamu. Wanadamu wanachangia kwa kuwasha mioto, kukata miti, kutalii bila mpango, na kukata miti ili kupanda michikichi inayotokeza mawese. Kisababishi kingine ni uwindaji. Watu fulani huwaua tumbili hao ili kujifurahisha tu. Wengine huwaua ili wapate chakula au ili watengeneze dawa za kienyeji. Kwa kuwa mara nyingi wanyama hao hulala karibu na mito mahali wanapoonekana wazi, ni rahisi sana kwao kuuawa. Kwa kweli, katika eneo fulani lililotembelewa mara nyingi na wawindaji wakiwa katika motaboti, idadi ya tumbili hao ilishuka kwa asilimia 50 katika miaka mitano!
Wanamazingira wanajaribu kuwahamasisha watu kuhusu hatari inayowakabili wanyama hao, na tumbili wa proboscis wanalindwa na sheria huko Borneo. Je, hatua hizo zitafaulu? Tutasubiri tuone. Ikiwa kiumbe huyo atatoweka mwituni, litakuwa jambo lenye kusikitisha sana kwa kuwa tumbili huyo anawavutia watu wanaochunguza vitu vya ajabu! Isitoshe, mnyama huyo hudhoofika anapofugwa.
Bila shaka, tumbili wa proboscis ni mnyama mmoja tu kati ya wengi wanaokabili hatari ya kutoweka. Wengine wengi tayari wametoweka. Jambo lenye kupendeza ni kwamba Mungu anakusudia kuja kuitawala dunia, kuwaondoa waovu, na kuwafundisha watu wake njia bora ya kutunza dunia, makao yao. (Methali 2:21, 22) Yehova Mungu anaahidi hivi: “Hawatasababisha madhara yoyote wala kusababisha uharibifu wowote katika mlima wangu wote mtakatifu; kwa maana dunia hakika itajawa na kumjua Yehova kama vile maji yanavyoifunika bahari.”—Isaya 11:9.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Tumbili anayeitwa proboscis anaishi katika kisiwa cha Borneo. Wenyeji wa kisiwa hicho humwita orang belanda, au “Dutchman.”
^ fu. 3 Tumbili wa kike pia wana pua kubwa ingawa si kubwa kama ile ya proboscis wa kiume.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Tumbili wa “Proboscis” wana pua ya ajabu na tumbo kubwa
[Hisani]
© Peter Lilja/age fotostock
[Picha katika ukurasa wa 13]
Pua ya “proboscis” wa kiume hufunika mdomo wake. Lazima aisukume kando anapokula
[Hisani]
© Juniors Bildarchiv/Alamy
[Picha katika ukurasa wa 14]
Iwe tumbili hao wanakula au kupumzika, mara nyingi wanakuwa katika kikundi
[Hisani]
© Peter Lilja/age fotostock