Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sehemu ya Juu ya Bawa la Mbawakawa wa Namib Linalonasa Maji

Sehemu ya Juu ya Bawa la Mbawakawa wa Namib Linalonasa Maji

Je, Ni Kazi ya Ubuni?

Sehemu ya Juu ya Bawa la Mbawakawa wa Namib Linalonasa Maji

● Watu milioni 900 hivi ulimwenguni pote hawana maji safi ya kunywa. Katika maeneo mengi, ni wanawake na watoto ambao hutembea mbali sana ili wateke maji kisha wanayabeba hadi nyumbani. Shreerang Chhatre, injinia katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts anasema, “Inasikitisha sana kwamba maskini wanalazimika kutumia saa nyingi sana kwa siku kutembea ili tu kujipatia uhitaji wa msingi.” Ili kusuluhisha tatizo hilo, Chhatre na wataalamu wenzake wanachunguza jinsi wanavyoweza kunasa ukungu, na ili wajifunze mbinu za kufanya hivyo wanamchunguza mbawakawa wa Namib.

Fikiria hili: Kila asubuhi ukungu hupita kwenye jangwa la Namib barani Afrika. Mbawakawa wa Namib hutumia nafasi hiyo kuelekeza mgongo wake upande ambao upepo unatoka. * Vinundu vilivyo kwenye sehemu ya juu ya mabawa yake vimefanyizwa kwa vitu vinavyonasa umande. Umande huo hujikusanya na kufanyiza matone makubwa. Matone hayo huanza kutiririka kupitia mikunjo iliyo katikati ya vinundu hivyo hadi kwenye mdomo wa mbawakawa huyo.

Chhatre na wataalamu wenzake wangependa kutumia mbinu kama hiyo kunasa maji kwa ajili ya matumizi ya wanadamu. Bila shaka, wanadamu wanahitaji maji mengi zaidi kuliko mbawakawa wa Namib ili waendelee kuishi. Na kugharimia mradi kama huo si rahisi. Kwa sasa, mbinu ya kunasa matone ya ukungu kwa ajili ya wanadamu “ni mradi ambao bado haujatimizwa,” anasema Chhatre.

Una maoni gani? Sehemu ya juu ya bawa la mbawakawa wa Namib linalonasa maji lilitokezwa na mageuzi? Au lilibuniwa?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Mbawakawa wa aina nyingine wameonekana wakikusanya maji kwa njia hiyo pia.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Matone ya maji hujikusanya na kuteremka hadi kwenye mdomo wa mbawakawa

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Photo: Chris Mattison Photography/photographersdirect.com