Ukosefu wa Haki Huumiza!
Ukosefu wa Haki Huumiza!
MNAMO 2010, Michael aliachiliwa huru kutoka katika gereza moja huko Texas, Marekani baada ya kufungwa kwa miaka 27 kwa shtaka la kumlala kinguvu mwanamke fulani—kosa ambalo hakulifanya. Aliachiliwa huru baada ya uchunguzi wa DNA kuthibitisha kwamba hakuwa na hatia. Uchunguzi huo haukuwepo wakati wa kuhukumiwa kwake. Baadaye, wenye mamlaka waliwapata wale waliohusika katika uhalifu huo, lakini hawangeweza kushtakiwa kwa sababu kulingana na sheria, muda mrefu ulikuwa umepita tangu walipotekeleza uhalifu huo.
Wahalifu wengi hawaadhibiwi. Kwa mfano, nchini Uingereza, “visa vya mauaji ambavyo havijatatuliwa vimeongezeka maradufu katika miaka kumi iliyopita, hilo likizua hofu kwamba polisi na mahakama zimeshindwa kukomesha jeuri yenye ukatili,” inasema ripoti moja katika gazeti The Telegraph.
Mnamo Agosti 2011, polisi wa Uingereza walipambana na uhalifu wa aina nyingine—ghasia huko Birmingham, Liverpool, London, na sehemu nyinginezo. Umati wenye ghasia uliwasha mioto, ukavunja madirisha ya maduka, na kupora, na kwa kufanya hivyo hawakuharibu tu biashara, nyumba, na magari, bali pia waliharibu njia ya watu ya kujipatia riziki. Ni nini kilichowachochea? Kwa wengi ilikuwa pupa. Hata hivyo, wengine walitenda hivyo kwa sababu ya kile walichoona kuwa ukosefu wa haki. Waandishi fulani wa habari walisema kwamba umati huo wenye ghasia huenda ulikuwa wa vijana waliohisi kuwa wamepuuzwa na serikali, ambao waliishi katika mitaa maskini na walioona kwamba hawana tumaini la kufanikiwa maishani.
Ayubu anayetajwa katika Biblia alisema hivi: “Naendelea kulia nipewe msaada, lakini hakuna haki.” (Ayubu 19:7) Vivyo hivyo leo, wengi wanalilia haki, lakini mara nyingi, vilio vyao havisikizwi. Je, kweli kuna mtu yeyote aliye na uwezo wa kukomesha ukosefu wa haki? Au ni jambo la kipumbavu kutumaini kwamba kutakuwa na wakati ujao wenye haki? Ili kupata jibu lenye kuridhisha, ni lazima tuchunguze baadhi ya mambo yanayosababisha ukosefu wa haki.