1. Tumia Busara Unaponunua Chakula
1. Tumia Busara Unaponunua Chakula
ISIPOKUWA uwe unakuza chakula chako mwenyewe, utakinunua sokoni au kwenye maduka makubwa. Utachaguaje na kununua chakula chenye lishe?
● Panga wakati wa kununua.
Baraza Linalotoa Habari Kuhusu Usalama wa Chakula nchini Australia linashauri hivi: “Kwanza nunua vyakula visivyoweza kuharibika haraka. Malizia kwa kununua vyakula vilivyowekwa kwenye friji au barafu.” Pia, nunua vyakula moto kabla tu ya kurudi nyumbani.
● Nunua vyakula vilivyotolewa moja kwa moja shambani.
Ikiwezekana, nunua vyakula vilivyotolewa moja kwa moja shambani. * Ruth, mama ya watoto wawili nchini Nigeria anasema: “Kwa kawaida, mimi huenda sokoni asubuhi na mapema wakati ambapo chakula kimeletwa tu kutoka shambani.” Elizabeth, anayeishi Mexico, pia hununua vyakula sokoni. Anasema: “Nikiwa sokoni ninaweza kununua matunda na mboga zilizotoka moja kwa moja shambani, na ninaweza kujichagulia mwenyewe. Kwa kawaida mimi hununua nyama iliyochinjwa siku hiyohiyo. Nisipoipika yote mimi huhifadhi inayosalia kwenye barafu.”
● Kagua chakula chako.
Jiulize: ‘Je, ngozi ya chakula ninachonunua imechubuka? Je, nyama ina harufu isiyo ya kawaida?’ Ikiwa chakula hicho tayari kimepakiwa, chunguza jinsi kilivyopakiwa. Upakiaji mbaya unaweza kuruhusu bakteria hatari kupenya kwenye chakula.
Chung Fai, anayeishi Hong Kong ambaye hununua chakula chake katika maduka makubwa anasema hivi, “Ni muhimu pia kuangalia tarehe iliyoonyeshwa ya muda wa kutumika kwa chakula kilichopakiwa.” Kwa nini? Wataalamu wanaonya kwamba hata ingawa huenda chakula ambacho kimepitisha muda wa kutumika kwake kikaonekana kuwa sawa, kikawa na ladha nzuri, au kisiwe na uvundo, bado kinaweza kukufanya uwe mgonjwa.
● Pakia chakula vizuri.
Ikiwa utatumia mfuko wa plastiki kubebea chakula, uoshe kwa ukawaida kwa maji moto yenye sabuni. Pakia nyama na samaki katika mifuko tofauti ili zisichafue vyakula vingine.
Enrico na Loredana, wenzi wa ndoa nchini Italia, hununua vyakula vyao karibu na nyumbani. Wanasema, “Kwa kufanya hivyo, hatusafirishi vyakula kutoka mbali na hivyo haviharibiki.” Ikiwa utatumia zaidi ya dakika 30 kufika nyumbani, weka chakula kilichogandishwa au chenye baridi katika mfuko unaohifadhi baridi ili kuhakikisha kwamba hakitapata joto.
Katika makala inayofuata, jifunze jinsi ya kuhakikisha kwamba chakula chako hakikudhuru unapokileta nyumbani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 6 Ona makala yenye kichwa “Njia ya 1—Kula Vizuri,” katika toleo la Amkeni! la Machi 2011.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
WAZOEZE WATOTO WAKO: “Mimi huwafundisha watoto wangu kuangalia muda wa mwisho wa kutumika kwa chakula kilichopakiwa, kama vile vitafunio, kabla hawajavinunua.”—Ruth, Nigeria